Na
Asteria Muhozya, Arusha
Serikali imesema
inaangalia uwezekano wa kuondoa kodi ya vifaa vya uongezaji thamani madini ikilenga kuhamasisha shughuli za uongezaji
thamani madini kufanyika nchini.
Hayo yamebainishwa na
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akijibu swali la mwanafunzi wa
Kituo Cha Jemolojia Tanzania (TGC) Rojer Mpele aliyeiomba Serikali kupitia
Naibu Waziri kuangalia namna ya kupunguza kodi ya vifaa hivyo ili kuwasaidia wanafunzi wanaojifunza ukataji na
ung’arishaji madini katika kituo hicho kuweza kujiajiri baada ya kuhitimu.
Nyongo ameongeza
kuwa, tayari Serikali imeanza kufanya taratibu za kupeleka maombi kuhusu jambo hilo katika Mamlaka husika ili
liweze kufanyiwa kazi kwani litahamaisha uwekezaji wa viwanda vya uongezaji
thamani madini nchini ikiwemo kuongeza wigo wa ajira na mapato kupitia sekta ya
madini.
Naibu Waziri Nyongo
amekitembelea kituo hicho kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujifunza
shughuli zinazofanyika kituoni hapo. Kituo cha TGC kipo chini ya Wizara ya
Madini, kinatoa mafunzo ya ukataji na ung’arishaji madini ya vito lengo likiwa
ni kuongeza thamani madini.
Ameongeza kuwa suala
la uongezaji thamani madini nchini ni jambo ambalo ni
kipaumbele cha serikali kutokana na Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya
Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017 na kwamba tayari serikali imezuia
usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na badala yake inahamasisha shughuli
hizo kufanyika hapa hapa nchini kwa kuwa, zitawezesha kuleta ujuzi, ajira,
mapato zaidi ya serikali na kuyaongezea thamani madini hayo nchini kabla
hayajasafirishwa nje ya nchi.
“Bado Wizara inaweka
msisitizo wa shughuli za uongezaji thamani zifanyike hapa nchini. Kwa hiyo
napenda kuwaambia ninyi vijana mnajifunza kitu ambacho ni kipaumbele kwa wizara
na serikali,” amesisitiza Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri
amesema kuwa, serikali kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
(SMMRP) unaotekelezwa chini ya wizara
kutokana na mkopo wa Benki ya Dunia, tayari umeagiza vifaa mbalimbali kwa ajili
ya kuanzisha karakana ya shughuli za uongezaji thamani madini katika kituo
hicho, karakana hiyo inalenga kutumiwa na wahitimu wa kituo husika ili
kwawezesha kujiajiri pindi wanapohitimu mafunzo yao.
“Watakaohitimu hapa
watalipia gharama ndogo sana za mashine watakazokuwa wakizitumia kufanya kazi
zao katika karakana hiyo. Lakini pia, ili kuboresha shughuli za karakana hiyo,
tutaendelea kujifunza kwa nchi nyingine namna wanavyoendesha karakana zao,”
ameongeza Nyongo.
Katika jitihada za
kuendelea kukiboresha kituo husika, Naibu Waziri Nyongo amemtaka Mratibu wa
Kituo hicho, kuandaa Mpango Mkakati wa
namna ya kukiboresha na kukitanua kituo hicho ili kiweze kuwa bora na mfano kwa
nchi nyingine barani Afrika.
“Imefika wakati
ambapo tunataka TGC kuwa chombo ambacho kinatoa ujuzi wa hali ya juu katika
uongezaji thamani madini. Lazima tutoe mafunzo kwa vijana wa kitanzania na tuendelee kuangalia namna ya kuleta ujuzi
au kwa kuwapeleka vijana wetu kujifunza kwa wenzetu na baadaye wawe wakufunzi
katika kituo hiki.
Vilevile, Naibu
Waziri Nyongo amesisitiza kuwa, Serikali kupitia wizara ya Madini itaendelea
kusimamia kwa karibu kuhakikisha kuwa inatekeleza na kutimiza malengo ya
uanzishwaji wa kituo hicho. “Lazima ifike mahali kituo kitoe mafunzo kwa jinsi
ilivyokusudiwa, ameongeza Nyongo.
Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Kituo cha TGC, Eric Mpesa
amesema kuwa, kituo hicho ni kituo pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza
taaluma ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba.
Pia, amesema kuwa,
kituo kinakusudia kutoa mafunzo ya Diploma ya Gem Jewelly technology ambapo mhitimu katika mwaka wa Kwanza
atapatiwa cheti cha NTA Level 4, mwaka wa pili NTA Level 5 na mwaka wa tatu NTA
Level 6.
“Kwa kuwa mafunzo
yanayotolewa katika kituo hiki ni ya muda mrefu na mfupi, taratibu za
kukisajili kwenye Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) zilifanywa na kwa
sasa kituo kimepata usajili wa kudumu wenye Na. REG/SAT/003,” ameongea Mpesa.
Mpesa ameongeza kuwa,
wizara iliamua kuwekeza katika Kituo hicho kwa lengo la kutoa mafunzo ya
kuongeza thamani madini ya vito kwa wadau na wajasiliamali wa madini hayo hapa
nchini.
Ameongeza kuwa,
malengo mengine ni pamoja na kukuza na kuendeleza ujuzi na ufahamu wa kutambua
madini ya vito, kuongeza thamani kipato na ajira kwa watanzania.
“ Hivi sasa kituo
hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya
vito na kinaendesha shughuli za uchongaji wa mawe ya miamba kwa
kutengeneza wanyama, ndege, samaki na
vitu mbalimbali vya mapambo, amesema Mpesa.
Kituo cha Jemolojia
Tanzania (Tanzania Gemological Center-TGC) kilianzishwa mwaka 2003 wakati
serikali ikitekeleza mradi wa Maendeleo Sekta ya Madini (Mineral Sector
Development Technical Assistance – MSD TA) ambao ulitekelezwa kati yam waka
1994 na 2005 kwa mkpo kutoka benki ya Dunia. Wakati huo lengo la kuanzissha
kituo hicho lilikuwa ni kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 1997 kuhusu
uongezaji thamani madini nchini kwa kuanzia na kutoa mafunzo ya uchongaji wa
vinyago vya miamba.
![]() |
Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi juu ya utambuzi wa madini
yaliyokatwa na kunga’rishwa na wanafunzi waliopata mafunzo katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC).
Kushoto ni Mkufunzi katika Kituo hicho
ambaye ni mhitimu katika kituo husika, Doricas Michael.
![]() |
Mmoja
wa Wanafunzi wanaofanya mafunzo ya ukataji na unga’rishaji madini ya vito
katika Kituo ch Jemolojia Tanzania (TGC).
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi kutoka kwa Mjiolojia na Mkufunzi wa Ukataji
na Unga’rishaji wa madini ya vito kutoka katika
Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Ester Njiwa, kuhusu namna mashine ya
kunga’risha madini inavyofanya kazi wakati alipokitembelea kituo hicho.
Mkufunzi huyo aalipata mafunzo kutoka nchini Sri-Lanka.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipata ufafanuzi kutoka kwa Mjiolojia na Mkufunzi wa Ukataji
na Unga’rishaji wa madini ya vito kutoka katika
Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Ester Njiwa, kuhusu namna mashine ya
kunga’risha madini inavyofanya kazi wakati alipokitembelea kituo hicho.
Mkufunzi huyo aalipata mafunzo kutoka nchini Sri-Lanka.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiangalia moja ya Mashine zinazotumika
kufanisi madini ya vito na miamba wakati
alipotembelea Kituo cha jemolojia Tanzania (TGC).
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika picha ya panoja na Wanafunzi wanaopata
mafunzo ya Ukataji na Unga’rishaji wa madini ya vito.
![]() |
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika
picha ya pamoja na Watumishi wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC).
No comments:
Post a Comment