Na Mohamed Saif
Serikali
imesema itawachukulia hatua za kinidhamu watendaji wanaotumia madaraka yao
vibaya kwa kuwanyanyasa wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kujipatia kipato
kinyume na taratibu.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye mkutano na wachimbaji
wadogo wa madini katika machimbo ya Dhahabu ya Kitunda yaliyopo Wilayani
Sikonge, Mkoani Tabora.
Wakielezea
changamoto zinazowakabili, wachimbaji wa machimbo hayo kwa nyakati tofauti walimueleza
Biteko masikitiko yao juu ya unanyasaji wanayofanyiwa na baadhi ya Maafisa wa
Serikali wasiowaaminifu wakiwemo Askari Polisi na Maafisa Madini.
Wachimbaji
hao walisema kumekuwepo na tabia ya kushinikizwa kutoa rushwa ama kugawana
faida kwa vitisho kuwa watazuiwa kuendelea kufanya shughuli zao kwenye maeneo
yao.
“Kuna
baadhi ya Maafisa Madini na Askari Polisi wamekuwa wakitulazimisha nao tuwape
mgawo wa mawe tunayochimba vinginevyo watafukia maduara yetu,” alisema Alfred
Kulwa mmoja wa wachimbaji kwenye machimbo hayo.
Kufuatia
malalamiko hayo, Naibu Waziri Biteko alitoa onyo kwa watendaji wenye tabia hiyo
kuacha mara moja na alimuagiza Afisa Madini kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa
Wilaya husika kuhakikisha wanafuatilia suala hilo na watakaobainika hatua kali
za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“OCD,
tendeni haki, hawa wawe salama. Askari atakayebainika ananyanyasa mchimbaji
madini achukuliwe hatua za kinidhamu haraka bila kuchelewa,” aliagiza Naibu
Waziri Biteko.
Biteko
alisema Afisa yeyote anayehitaji kujishughulisha na biashara ya madini aache
kazi ili ajikite katika biashara hiyo na sio kutumia cheo chake kuwanyanyasa
wachimbaji.
Aliongeza
kuwa hairuhusiwi Mtumishi wa Umma kutumia cheo kujinufaisha. “Marufuku
watendaji wa Serikali ama wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kutumia
madaraka yao vibaya. Kama unataka ingia uchimbe mwenyewe. Serikali hii ya Awamu
ya Tano inatutaka tuondoe manyanyaso,” alisema Biteko.
Biteko
alisema mchimbaji atakayenyanyaswa atoe taarifa Polisi na pia amfahamishe kwa
njia ya simu kuhusiana na manyanyaso hayo ambapo alitaja namba zake za simu ili
kukitokea hali ya sintofahamu wasisite kumfahamisha.
Hata
hivyo, Biteko aliwataka wachimbaji hao kuacha kuwasilisha taarifa za uwongo
ikiwemo kusingiziana na mara zote wasimamie haki ili kuepusha migogoro baina
yao na Serikali.
No comments:
Post a Comment