Na
Veronica Simba, Kagera
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amewaahidi wananchi wa Kagera kuwa Serikali
inashughulikia kwa umuhimu mkubwa na kwa haraka suala la Soko kwa ajili ya
Madini ya Bati yanayochimbwa wilayani Kyerwa, ili waendelee kunufaika nayo na
nchi ipate faida kama ilivyo kwa majirani zetu wa Uganda na Rwanda.
Alitoa ahadi hiyo
jana, Februari 27 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum
Kijuu, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kazi mkoani humo.
Akizungumza na Mkuu
wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Naibu Waziri Nyongo
alikiri kuwa wachimbaji wa Madini ya Bati hapa nchini, kwa sasa wana wakati
mgumu kutokana na Serikali kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi; hata
hivyo akasema kuwa hali hiyo itakoma hivi karibuni kwa kuwa suala hilo
linashughulikiwa kwa haraka.
Akifafanua zaidi,
Nyongo alisema kuwa Tanzania ilichelewa kujiunga na Mkataba wa Kimataifa
unaowezesha madini hayo kutambuliwa na kununulika kokote, hali iliyosababisha
nchi jirani za Rwanda na Uganda ambazo zimeshajiunga na Mkataba huo, kutumia
fursa hiyo kununua malighafi hiyo muhimu kutoka kwa wachimbaji wa hapa nchini
kwa bei ya chini sana.
Alisema kuwa, ni kwa
sababu hiyo Serikali iliamua kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi mpaka
pale itakapokamilisha taratibu mbalimbali zitakazoiwezesha nchi na wananchi
wote kunufaika ipasavyo kutokana na madini mbalimbali yanayopatikana nchini,
ikiwemo kuharakisha mchakato wa kujiunga na Mkataba huo wa Kimataifa.
“Kwa hiyo, mimi
nikuhakikishie kwamba, suala hilo tunalishughulikia kwa uharaka ili kuhakikisha
nasi kama kama nchi tunatambulika katika Mikataba hiyo ya Kimataifa, ili nasi
tuanze kuuza Bati yetu vizuri. Tunalichukulia suala hili kwa umuhimu wa
kipekee.”
Aidha, Nyongo
aliieleza pia Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama kuhusu suala la utoaji Leseni za
Madini nchini, kwamba utaendelea mapema iwezekanavyo mara tu baada ya Tume ya
Madini itakapoanza kufanya kazi.
“Tume itaanza kufanya
kazi muda wowote kuanzia sasa, mara tu Mheshimiwa Rais atakapofanya uteuzi wa
Mwenyekiti wake. Na itakapoanza kazi tu, zoezi la utoaji na uhuishaji wa Leseni
litaendelea.”
Vilevile, alifafanua
kuwa, kufuatia kufutwa kwa iliyokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania
(TMAA) na kuundwa Tume ya Madini; hakutakuwa tena na Ofisi za Madini za Kanda
bali kutakuwa na Ofisi za Madini za Mikoa.
Kwa upande wa Madini
ya Nickel ambayo pia yanachimbwa ndani ya Mkoa huo, Naibu Waziri alisema kuwa
ni moja ya madini yanayoleta matumaini mapya ya kulinufaisha Taifa kutokana na
umuhimu wake katika Soko la Dunia kwa sasa.
Alisema kuwa, kutokana
na kukua kwa Teknolojia Duniani, Madini ya Nickel yanahitajika sana, hususan
katika nchi zilizoendelea kwa ajili ya kutengeneza Betri maalum za Magari
ambazo zinachajiwa na hivyo kutotumia mafuta.
“Sasa hivi nchi
zilizoendelea wanataka kupunguza matumizi ya mafuta kwenye magari na ukienda
Miji mikubwa ya Ulaya, wanataka kufikia 2040 wasitumie tena mafuta kwenye
Magari yao, badala yake watumie Betri. Nickel ni madini muhimu sana katika
utengenezaji wa Betri hizo na mitambo mingine inayohifadhi chaji za umeme kama
vile kwenye Simu na kadhalika.”
Kuhusu uwekezaji
katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, unaomilikiwa na Serikali kupitia Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO), Naibu Waziri alieleza kuwa Serikali inajipanga
upya kuona ni namna gani Mgodi huo uendeshwe ili kuhakikisha unaleta tija kwa
Taifa na siyo kuleta hasara kama ilivyo sasa.
Alisema kuwa, baada
ya Serikali kubaini kuwa hasara iliyopatikana katika Mgodi huo imesababishwa na
Mgodi kutosimamiwa vizuri, ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasimamisha
kazi wahusika pamoja na kutuma Timu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa kwenda kuhakiki madeni husika.
“Kwa hivyo, tumeamua
kusimamisha shughuli zote pale, tujihakikishie yale madeni. Uchunguzi
unaendelea na baada ya muda tutatoa msimamo wa Serikali kuhusu namna bora ya
kuuendesha ule Mgodi.”
Baada ya kukutana na
kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Uslama ya Mkoa, Naibu Waziri pia alitembelea
Ofisi za Madini za Mkoa na kuzungumza na wafanyakazi.
Naibu Waziri anaendelea
na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo akiwa mkoani Kagera,
anatarajiwa kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini ya Bati, kukagua
maendeleo ya ujenzi wa Viwanda vidogo vya uongezaji thamani Madini hayo pamoja
na kukagua Mradi wa Kabanga Nickel.
No comments:
Post a Comment