Monday, February 26, 2018

Mkutano mkubwa wa wadau wa madini wafanyika Mwanza


Ø Waazimia hakuna tena utoroshaji wa madini

Ø Wapendekeza Soko la pamoja kwa madini ya dhahabu

Ø Kamati yaundwa kuandaa taratibu

Na Veronica Simba, Mwanza

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameongoza Mkutano mkubwa wa wadau wote wa madini katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa uliojadili namna ya kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa pamoja na udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Mkutano huo uliofanyika jana Februari 25 jijini Mwanza, uliazimia kwa sauti moja kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi.

Aidha, Mkutano ulipendekeza kuwepo na Mnada au Soko la pamoja la Madini ya Dhahabu ili kuweka mazingira wezeshi na yenye tija kwa wadau wote wa sekta hiyo.

Kufuatia maazimio hayo, Mkutano uliunda Kamati yenye wajumbe 14 kutoka kada mbalimbali za sekta husika, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa sasa wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina na Katibu ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba.

Akiwasilisha Hadidu za Rejea kwa Kamati husika ambayo imeahidi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya siku 30 kuanzia jana Februari 25, Mwenyekiti wa Mkutano ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alizitaja kuwa ni pamoja na kuainisha utaratibu utakaotumika kuanzisha Soko hilo la Dhahabu katika Jiji la Mwanza kama ilivyopendekezwa.

Alitaja kazi nyingine inayopaswa kufanywa na Kamati hiyo kuwa ni kubainisha mbinu zitakazotumika kupata washiriki wa Mnada huo ikiwa ni pamoja na wauzaji na wanunuzi.

Vilevile, alisema Kamati husika itatakiwa kuainisha miundombinu ya Mnada mzima kwa maana ya mpangilio wa wote watakaohusika katika Mnada huo kama vile watu wa kodi, Benki mbalimbali na wengineo. “Kwa ufupi watapaswa kuainisha shughuli zote ambazo zitaendana na Mnada zifanyike vipi.”

Aidha, Kamati imetakiwa kuandaa na kuwasilisha Mkakati utakaobainisha utaratibu mzima au mbinu sahihi zinazopaswa kutumika katika zoezi zima la kuanzia ununuzi hadi upatikanaji wa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi kwa kutumia muda mfupi.

Kazi nyingine ya Kamati husika ni kupambanua faida na hasara za uwepo wa Soko hilo ili kuleta uelewa kwa wadau wote wanaohusika.

Awali, akizungumza katika Mkutano huo, Naibu Waziri alisema kuwa kwa niaba ya Serikali, ameafiki mapendekezo ya wajumbe na utayari wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kutoa eneo katika Jiji lake kwa ajili ya kufanyikia kwa Mnada husika.

“Wazo mlilopendekeza la kuwa na Kituo kimoja nchini cha kuuza Dhahabu ni jema sana. Naliunga mkono. Sisi kama Serikali tutakuwa tukitangaza wanunuzi wakubwa waje kwenye Mnada ili wanunue pale Dhahabu. Tupunguze chaneli ya madalali hapa katikati ili kusudi mkutane na wanunuzi wakubwa uso kwa uso na kufanya biashara,” alibainisha Nyongo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alimhakikishia Naibu Waziri na wadau wote kuwa Ofisi yake iko tayari kutoa eneo zuri na salama kwa ajili ya kuendeshea Mnada husika.

Akizungumza katika Mkutano huo, Rais wa FEMATA, John Bina aliwaasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia haki na wajibu wao kama sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya madini zinavyoelekeza ili kufanikisha maazimio ya Mkutano huo kuhakikisha suala la utoroshaji madini linakoma.

“Sote tumekiri ukweli kwamba tunaiba, hatuchangii mapato, wengine hatujarasimishwa katika sekta, tujiulize tunafanya nini?! Tumejipanga vipi? Lazima tulijue hilo,” alisisitiza.

Awali, akizungumzia lengo la kuandaa Mkutano huo, Kamishna Msaidizi wa Kanda, Mhandisi Samamba alibainisha kuwa ni kutokana na changamoto ambayo imeibuka ya utoroshaji wa madini.

“Kwa hiyo, Wizara kupitia kwa Naibu Waziri wa Madini Nyongo, imeona iitishe Mkutano mkubwa na wadau wote wa uchimbaji ili kujadiliana pamoja tatizo liko wapi na kuja na suluhisho la kudhibiti utoroshaji huu wa madini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.”
Kabla ya kufikia maazimio husika, asilimia kubwa ya wajumbe wa Mkutano huo walikiri kuwa utoroshaji wa madini upo ambapo kwa madai yao, hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na utozwaji wa kodi na tozo mbalimbali stahiki.

Waliiomba Serikali ipunguze kodi na tozo zilizopo ili waweze kumudu kuzilipa na hivyo kuachana na udanganyifu wa aina mbalimbali unaoendelea katika sekta hiyo.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Mhandisi Samamba alifafanua kuwa, suala la kulipa kodi limekuwa ni changamoto kwa wachimbaji wengi kutokana na kushindwa kutunza kumbukumbu zao hivyo kulazimika kulipa zaidi tofauti na wale wanaomudu kutunza kumbukumbu zao ambao hujikuta wanalipa kodi kidogo.

Vilevile, walitaja changamoto ya Soko la uhakika linalosababishwa na wengi wao kutokufahamu bei halisi ya dhahabu na ndiyo sababu wengi wakapendekeza kuanzishwa kwa Soko la Pamoja.

Hivi karibuni, akiwa ziarani Geita, Naibu Waziri alipokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Luhumbi kuhusu masuala ya utoroshaji wa madini ambapo aliahidi kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuitafutia suluhisho changamoto husika.

Aidha, Naibu Waziri alitoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na utoroshaji madini kuacha mara moja vinginevyo, wataadhibiwa vikali pindi wakibainika.

Naibu Waziri anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya madini pamoja na kuzungumza na wananchi.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, akizungumza na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba, akizungumza wakati wa Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina akizungumza wakati wa Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.



Sekretarieti, wakichukua kumbukumbu za Mkutano wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya madini kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakichangia mada wakati wa Mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, uliofanyika jana, Februari 25 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini nchini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya madini kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakichangia mada wakati wa Mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, uliofanyika jana, Februari 25 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini nchini.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wachimbaji wa madini kutoka Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Mkutano ulifanyika jana, Februari 25 na ulijadili upatikanaji wa ufumbuzi wa utoroshaji madini. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela na kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina.

No comments:

Post a Comment