Wednesday, November 22, 2017

Wanaodai fidia mgodi wa Buckreef kuhakikiwa

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef, Peter Zizhou (kulia) akielezea teknolojia ya zamani ya  uchenjuaji wa dhahabu kwa  Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo uliopo mkoani Geita kwa ajili ya kujionea maendeleo ya shughuli zake tarehe 27 Oktoba, 2017. Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akimshukuru  Kaimu Afisa Mtendaji kutoka Kampuni ya  Tanzanian Royalty Exploration, Jeffrey Duval (katikati) mara baada ya kampuni  hiyo kupitia Mgodi wa Buckreef ulioko mkoani Geita kutoa mchango wa madawati 105 yenye thamani ya shilingi milioni saba kwa ajili ya shule ya sekondari moja na shule za msingi nne zilizopo katika kata ya  Busanda wilayani Geita mkoani Geita. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Busanda,  Justa Mabala. 

Mmiliki wa Mgodi wa Busolwa Mining Limited, Christopher Kadeo (wa pili kulia mbele) akielezea shughuli zinazofanywa na mgodi huo kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ( kushoto mbele) mara walipofanya ziara katika mgodi huo.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema Serikali inatarajia kuwasilisha majina ya wananchi 1062 waliofanyiwa  tathmini katika eneo la Kiseme wilayani Geita ili kulipwa fidia  kwa ajili ya kupisha shughuli za uchimbaji madini za Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kufanyiwa uhakiki na kubaini uhalali wa umiliki wake kabla ya kuanza kwa taratibu za malipo.

Waziri Kairuki aliyeambatana na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameyasema hayo mapema leo  katika Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef uliopo wilayani Geita mkoani Geita  mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku moja katika mgodi huo ili kujionea maendeleo  ya mgodi huo na kutatua changamoto zake.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara zake pamoja na Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika migodi ya serikali, binafsi na wachimbaji wadogo katika mikoa ya  Kagera na Geita ili kufahamu kwa undani  mafanikio na namna ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta  ya madini.
Alisema kuwa, kabla ya kuanza kwa ulipaji wa fidia, ni lazima Wizara ya Madini ihakikishe majina ya wanaodai fidia yanafikishwa katika  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na wataalam wa wizara hiyo  ili kuepuka udanganyifu kwenye umiliki wa ardhi.

Aliendelea kusema kuwa katika sekta ya madini kumekuwepo na migogoro mingi hususan katika  madai ya fidia kutokana na wamiliki wengi  wasiokuwa halali kujitokeza na kudai  fidia  hali inayochangia  wawekezaji kushindwa kulipa kutokana na gharama kuwa kubwa.

Katika hatua nyingine, Kairuki alitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lenye umiliki wa asilimia 45 katika mgodi  huo kwa niaba ya  Serikali kuhakikisha linafanya tathmini ya vifaa vyote vinavyotumika katika uchimbaji na uchenjuaji madini pamoja na mikataba  kati yake na mbia wake ambaye ni kampuni ya Tanzam 2000 mwenye asilimia 55.

“Mkumbuke kuwa mmepewa dhamana  na Serikali ya kusimamia mgodi huu, hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa yanaangaliwa huku mkifanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu  ili uchimbaji ulete tija,” alisema Kairuki.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza  katika kikao na  uongozi na wafanyakazi wa mgodi wa  dhahabu wa Busolwa Mining Limited, alisema kuwa Serikali ipo tayari kuwasaidia wachimbaji wadogo ili uzalishaji wao  ulete manufaa kwenye uchumi wa nchi.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wa madini hususan wazawa wanafanya  shughuli zao katika mazingira rafiki na kupata faida kubwa na kutoka kwenye lindi la umaskini

Alisisitiza wachimbaji wa madini kufuata kanuni na sheria katika shughuli zao na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutoa elimu kuhusu kanuni na sheria za madini.

No comments:

Post a Comment