Aelekeza
soko la madini kuanzishwa mara moja………
Na Greyson Mwase,
Kahama
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ameelekeza soko la madini katika mkoa wa kimadini wa
Kahama ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya Chunya, Musoma, Singida kuanzishwa
mara moja ili kudhibiti utoroshwaji wa madini unaopelekea Serikali kukosa
mapato yake.
Naibu Waziri Nyongo
ameyasema hayo leo tarehe 31 Machi, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa
habari uliofanyika mjini Kahama. Wengine waliokuwepo katika mkutano huo ni
pamoja na Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya
Madini, Ali Saidi Ali, Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian pamoja na wataalam kutoka
Tume ya Madini.
Alisema kuwa, mara
baada ya kufanya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Kahama, alibaini
kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika shughuli za uchenjuaji wa madini huku
akitolea mfano wa kampuni ya Busami inayojihusisha na uchenjuaji wa madini ya
dhahabu.
Alisisitiza kuwa,
alibaini kumekuwepo na udanganyifu kwenye uzito na kiwango halisi cha dhahabu
kwenye madini yaliyopatikana hali inayopelekea Serikali kukosa mapato yake
stahiki.
“Kwa mfano katika
mtambo wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Busami tumebaini kuna
udanganyifu kwenye uchenjuaji, jana baada ya kufika na kuona namna uchenjuaji
wa madini unavyofanyika na kuelekeza wataalam wa madini kuchenjua upya mchanga
uliokuwepo kwenye maji yaliyohifadhiwa, tulibaini kuna madini," alisema
Nyongo
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo alisimamisha shughuli za uchenjuaji katika
kampuni ya Busami na kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mmiliki
wake.
Wakati huo huo, Naibu
Waziri Nyongo alielekeza wamiliki wote wa mitambo ya kuchenjulia madini ya dhahabu nchini
kuhakikisha wanakuwa na mizani na mashine maalum za kupimia madini ya dhahabu
zilizoidhinishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania, na biashara ya madini kufanyika
katika masoko ya madini yaliyoanzishwa na kusisitiza kuwa lazima madini
yajulikane yanapopelekwa na Ofisi za Madini Nchini kuhakikisha zinatuza
kumbukumbu sahihi.
Wakati huo huo Naibu
Waziri Nyongo aliagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kufuatilia
iwapo hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya kampuni inayojihusisha na
uchenjuaji wa madini ya dhahabu Wilayani Kahama ya Jema baada ya kukamatwa
ikifanya udanganyifu hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment