Na
Greyson Mwase, Kahama
Ofisi ya Afisa Madini
Mkazi, Mkoa wa Kimadini wa Kahama inatarajia kuanzisha soko la madini mapema
ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kudhibiti
utoroshwaji wa madini.
Hatua hiyo imekuja
kufuatia ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyoifanya mapema
leo tarehe 30 Machi, 2019 katika Wilaya ya Kahama lengo likiwa ni kukagua
shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu, kusikiliza na kutatua
kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara hiyo,
Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji Migodi na
Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali wataalam kutoka Tume ya Madini pamoja
na wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mara baada ya kufanya
ziara katika baadhi ya mitambo ya
kuchenjua dhahabu, Nyongo alifanya kikao na wamiliki wa mitambo hiyo na
kusikiliza kero mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Mara baada ya kusikiliza
kero husika ikiwa ni pamoja na ya kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya
ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Kimadini wa Kahama, Adrea Fabian
kuhakikisha sehemu ya ofisi yake inatumika kama soko la madini ya dhahabu
ambapo wauzaji na wanunuzi watakuwa wanafanya biashara huku serikali ikipata
mapato yake, kauli ambayo ilipokelewa kwa shangwe na wafanyabiashara wa madini
ya dhahabu.
Aliendelea kusema
kuwa kutokuwepo kwa soko la madini katika Wilaya ya Kahama, kunachochea
utoroshwaji wa madini ya dhahabu kwakuwa inakuwa vigumu kwa wauzaji wa madini
hayo kusafiri umbali mrefu hadi Geita kwa ajili ya kwenda kuuza madini hayo.
“Hapa tunataka
kuhakikisha biashara ya madini inafanyika hapa hapa ili kuwarahisishia
wafanyabiashara wa madini ya dhahabu huku Serikali ikipata mapato yake,”
alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine,
Nyongo aliutaka uongozi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa
Kahama kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali kama vile Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mabenki na soko kuanza mara moja.
Aidha, Naibu Waziri
Nyongo aliwataka wamiliki wa mitambo ya kuchenjua dhahabu kuunga mkono juhudi
za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika
kulinda rasilimali za madini kwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini.
Wakizungumza katika
nyakati tofauti wamiliki wa mitambo ya kuchenjulia dhahabu walioshiriki katika
kikao hicho mbali na kumpongeza Naibu Waziri Nyongo wamesema kuwa uwepo wa soko
hilo utawarahisishia sana biashara ya madini kutokana na kuepukana na matapeli
huku serikali ikipata mapato yake stahiki.
Walisema kabla ya
uamuzi huo wamekuwa wakisafirisha madini hadi Geita kwa ajili ya kuuza hali
inayopelekea baadhi yao kuuza kwa watu wasio waaminifu.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kulia) akikagua mashine ya kupima dhahabu
katika kampuni ya Busami iliyopo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ikiwa ni
sehemu ya ziara yake katika mkoa huo ya kukagua shughuli za uchimbaji na
uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe
30 Machi, 2019.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akijadiliana jambo na Kamishna Msaidizi-
Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali (katikati) katika
kampuni ya Busami iliyopo Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Kutoka kulia Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Kamishna Msaidizi- Uendelezaji Migodi na
Madini wa Wizara ya Madini, Ali Said Ali wakisikiliza kero za wamiliki wa
mitambo ya kuchenjulia dhahabu (hawapo pichani) kupitia mkutano maalum
uliofanyika Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment