Monday, April 1, 2019

Hatukunufaika na madini, haikuwa ajenda ya Kitaifa–Spika Ndugai


Na Asteria Muhozya,

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugani, amesema awali, Taifa halikunufaika na rasilimali madini kwa kuwa sekta hiyo haikuwa ajenda ya Kitaifa.

“Madini yaliachwa kwa wabunge ambao rasilimali hiyo inapatikana kwenye maeneo yao, haikuwa ajenda ya taifa, wengine walizungumzia zaidi masuala yanayowagusa kama korosho, pamba na mambo mengine, nashukuru tumefanya mabadiliko na sasa matokeo yameanza kuonekana,” amesema Spika Ndugai.

Amesema  kwa mwelekeo wa sasa, serikali imefika mahali ambapo manufaa ya rasilimali hiyo yameanza kuonekana kutokana na  mageuzi makubwa yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na kumpongeza kutokana na namna anavyohakikisha rasilimali madini inalinufaisha taifa, na kuongeza, “kilio cha watanzania cha kutokunufaika na madini kimepata mwenyewe, Rais Magufuli amefanya uthubutu”.

Spika Ndugai ameyasema hayo Machi 30, 2019, wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya Wenyeviti wa Kamati nyingine za bunge wanaohudhuria semina ya siku mbili jijini Dodoma, iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa lengo la kutoa elimu ili kupata uelewa wa sekta ya madini.

Amesema, awali, ikijulikana kama Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa ni kazi hata kwa bunge hilo kupitisha Bajeti ya wizara hiyo kutokana na kwamba, sekta zote mbili nishati na madini   hazikuwa zikilinufaisha taifa na kusema, “ kulikuwa na kutokuridhika na sekta zote na hususan madini, kama taifa tulikuwa hatupati haki yetu tuliyoistahili”.

Kufuatia hali hiyo, Spika Ndugai amewataka Wabunge  na wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli  kwa kuwa  mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa utasaidia kusogeza mbele maendeleo ya taifa na watu wake.

Aidha, amewaasa viongozi wote waliobeba dhamana ya kusimamia sekta husika kuhakikisha wanaichukulia dhamana waliyopewa kwa uzito wa kipekee  ili kuliwezesha taifa kufanana na nchi nyingine ambazo zimeendelea kutokana na rasilimali madini.

Pia, amepongeza mabadiliko yanayofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kueleza kwamba anafurahi kusikia STAMICO mpya tofauti na ilivyokuwa awali.

Akizungumzia Kamati mbili zilizoundwa na bunge kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi, amesema kuwa, kamati hizo zilifanya kazi nzuri na kwamba  bunge litaendelea kuishauri serikali  ili kuhakikisha sekta  ya madini inazidi kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Ameongeza kuwa, ripoti hizo zilipokelewa vizuri na serikali na kwamba juhudi zilizochukuliwa zimewezesha uanzishwaji wa masoko ya madini huku STAMICO ikifanya mabadiliko makubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza katika semina hiyo, amesema  sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa taifa la Tanzania na kueleza kuwa, mchango wa taifa umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kueleza kuwa, mwaka 2017, sekta hiyo ilichangia asilimia 4.8 kwenye pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwaka 2015.

Akizungumzia ukuaji wa sekta hiyo amesema umeongeza kwa kasi kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 kufikia 17.5 mwaka 2017, na kusema mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi  ili kufikia lengo la asilimia 10 ya mchango wake ifikapo mwaka 2025.

Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanywa mwaka 2017,  na usimamizi wa Rasilimali Madini, amesema umewezesha ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za madini kutoka Shilingi bilioni 194 iliyotarajiwa kukusanywa mwaka 2017/18 hadi shilingi bilioni 301.29 sawa na asilimia 154.999 ya lengo la makusanyo kwa mwaka huo.

“Mhe. Spika, mwenendo wa ukusanyaji maduhuli kwenye sekta hii kwa mwaka 2018/19 ni wa kuridhisha ambapo hadi Februari kiasi cha shilingi 218,650,392 kimekusanywa hii ikiwa ni sawa na asilimia 105.6,” amesema Waziri Biteko.

Ameeleza kuwa, miongoni mwa sababu zilizopelekea mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa mrabaha  kwa baadhi ya madini, kuanzisha kodi  mpya  ya ukaguzi ya asilimia 1; kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini; na kwa kushirikiana na wananchi  na vyombo vya ulinzi na usalama na kuzuia usafirishaji wa madini ghafi ya nje ya nchi ili  viwanda vya kusafishia na kuongeza ubora wa madini vijengwe  nchini.

Akizungumzia usimamizi wa shughuli za madini ya Tanzanite baada ya kukamilika kwa ukuta unaozunguka machimbo ya tanzanite Mirerani amesema udhibiti wa madini hayo umeimarika  na kusababisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na madini hayo.

Ameongeza kuwa, kufuatia juhudi hizo, ukusanyaji wa maduhuli kutokana na uzalishaji wa tanzanite kwa wachimbaji wa Wadogo na Kati uliongezeka hadi kufikia shilingi 1,436, 427, 228.99 kwa mwaka  2018, ikilinganishwa na  shilingi 71,861,970 kwa mwaka 2016.

“Uzalishaji umeongezeka kutoka migodi midogo na ya kati hadi kufikia kilo 781.204 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na kilo 147.7  zilizoripotiwa  kwa mwaka 2017 na kilo 164.6 za mwaka 2016,” amesema Waziri Biteko.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula, ameishukuru Wizara kwa kuandaa semina hiyo kwa wabunge na kueleza kuwa, kamati hiyo itaendelea kupata uelewa kuhusu sekta ya madini.
Mbali na wabunge, wengine wanaoshiriki semina hiyo ni Wenyeviti wa Bodi za taasisi za zilizo chini ya wizara, Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake.


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai akieleza jambo wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini( hawapo pichani). 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai (wa pili kulia) akiteta jambo na Waziri wa Madini Doto Biteko (wa pili kushoto)na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula (wa kwanza kulia). Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila. 

Baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalam wa Wizara ya Madini. 

Baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalam wa Wizara ya Madini. 

Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Madini, Wenyeviti wa Bodi ya Taasisi  chini ya wizara na Wataalam kutoka wizarani na  taasisi zake wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Semina iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kwa  Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya wabunge wa kamati nyingine (hayupo pichani). 

Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Madini, Wenyeviti wa Bodi ya Taasisi  chini ya wizara na Wataalam kutoka wizarani na  taasisi zake wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Semina iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kwa  Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na baadhi ya wabunge wa kamati nyingine (hayupo pichani).

No comments:

Post a Comment