Thursday, February 7, 2019

Biteko apangua hoja hofu ya wadau kuwekeza nchini


Na Nuru Mwasampeta,

Waziri wa Madini, Doto Biteko amewatoa hofu Wawekezaji wa Nje na kueleza kuwa, Mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, hayana lengo la kuwakandamiza isipokuwa yamelenga katika kuifanya rasilimali madini kuwanufaisha wote, wawekezaji na watanzania.

Aliyasema hayo Januari 4, 2019 katika kikao baina yake na Balozi wa Canada nchini Pamela O’Donnel, ambacho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal.

Akielezea lengo la kuonana na uongozi wa juu wa Wizara, Balozi O’Donnel alisema amefika ili kupata uelewa wa mabadiliko mbalimbali yaliyotokea katika sekta ya madini pamoja na maeneo mengine ili kuwatoa hofu wawekezaji kutoka katika taifa lake wanaopenda kuwekeza nchini.

Pamoja na nia yake ya kupata ufumbuzi kwa masuala ya Sheria ya Madini, Balozi O’Donnel alihoji kuhusu masuala mengine ikiwemo utawala wa kisheria, mikataba ya madini, kodi na tozo mbalimbali pamoja na upatikanaji wa vibali vya kufanya kazi nchini kwa wananchi kutoka nchini Canada.

Akijibu hoja hizo, Waziri Biteko aliwataka wawekezaji kutoka nchini Canada kutokuwa na wasiwasi kwa mabadiliko hayo na kuwataka kutembelea ofisi ya madini ili kupata ufafanuzi wa jambo lolote lenye utata katika kufanikisha nia njema ya kuwekeza nchini. “Tupo kwa ajili yao, wasisite kupata ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu sekta ya madini,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa, mataifa mbalimbali duniani yanafanya mabadiliko katika masuala mbalimbali na kueleza kuwa, si vibaya kwa Tanzania kufanya mabadiliko kwa jambo lolote ambalo lina manufaa kwa taifa.

Waziri Biteko alieleza kuwa, madini ni rasilimali inayokwisha, hivyo ni muhimu madini yanapochimbwa yawaletee faida watanzania  na pindi  yatakapokwisha wajivunie rasilimali madini iliyokuwepo kutokana na maendeleo yaliyoletwa na Madini hayo kama vile barabara bora, shule, ujenzi wa vituo vya Afya na masuala mengine ya maendeleo.

“Sheria ya awali ilikuwa hainufaishi taifa na watanzania ndio maana mabadiliko yanafanyika.Mabadiliko ni kitu kizuri, tunahitaji rafiki atakayesababisha mabadiliko kutokea hivyo hawana haja ya kuogopa, tunawakaribisha kuwekeza” alisisitiza Biteko.

Akifafanua zaidi, Biteko alieleza kuwa, mabadiliko ya sheria ya madini yamekuwa yakifanyika kulingana na sera inayoongoza. Alieleza kuwa tangu kutungwa kwa sheria ya madini mwaka 1998 mabadiliko yamefanyika kwa awamu mbili yaani mwaka 2010 na mwaka 2017 lengo likiwa ni moja tu, rasilimali madini iweze kulinufaisha taifa na Watanzania.

Aidha, alibainisha kuwa mabadiliko ya kisheria yanayotokea katika sekta ya madini yanapitia mchakato wa kutosha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta na hayatokei kwa ghafla kama inavyozungumzwa.

Waziri Biteko alisema serikali imekusudia kuziwezesha benki za ndani kukua na hivyo kuwataka wawekezaji kutunza fedha zao katika benki za ndani na endapo wawekezaji watataka kutunza fedha zao katika benki za nje watumie benki zenye usajili nchini Tanzania.

Kuhusiana na suala la upatikanaji wa vibali kwa wataalamu wa kigeni kufanya kazi nchini, Biteko alifafanua  kuwa, Serikali haizuii wataalamu kutoka nje kufanya kazi nchini isipokuwa kuwepo uwazi na uwajibikaji na Serikali ikijiridhisha na  kubaini kuwa nchini hakuna mtaalamu wa kufanya kazi fulani serikali haitasita kutoa kibali kwa watu kutoka nje ya nchi kuja kufanya kazi nchini.

Kwa upande wa utawala wa kisheria, Biteko alikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaongoza nchi kwa Sheria na taratibu bila kuchagua wala kubagua.

Biteko alitanabaisha kuwa kutokana na ukweli kwamba wapo watu ambao wamejikita katika kuamini mitazamo hasi na hawataki ukweli ni suala gumu kubadili mitazamo yao, na kueleza kuwa, itakuwa rahisi kwa wale watakaokubali ukweli na kubadili mitazamo hasi waliyonayo juu ya serikali ili kwenda sambamba.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema, wawekezaji ni wadau muhimu wa maendeleo na hakuna taifa lolote lililo tayari kuwakatisha tamaa wadau wa maendeleo.

Aidha, alibainisha mambo manne yaliyopelekea Sheria ya Madini kufanyiwa marekebisho ili kukidhi matakwa ya taifa na watu wake kwa ujumla na kusema kuwa mambo hayo ni pamoja na kuongeza mapato kwa taifa kwa kuongeza mrabaha wa madini ya vito na almasi kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 6.

Alisema, suala lingine ni uongezaji thamani wa rasilimali madini inayopatikana nchini ili inaposafirishwa nje ya nchi iwe ya viwango vyenye ubora mkubwa na hivyo kusaidia kuongeza mapato kwa taifa. Aidha, amebainsha kuwa kuna baadhi ya madini kama ya graphite yanayoongezwa thamani kwa asilimia 90 na kusafirishwa nje ya nchi kuongezewa ubora zaidi.

Akifafanua hilo, Nyongo alisema ili kulipelekea taifa kuwa na viwanda vya kutosha, serikali imefanya mabadiliko hayo ili kupata wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchakata madini nchini ili yasafirishwe yakiwa katika viwango bora na kupelekea ongezeko la fedha za kigeni nchini.

Pia, Naibu Waziri Nyongo alizungumzia suala la uwajibikaji wa wawekezaji kwa jamii ya kitanzania na kusema kuwa, ili kuwafanya wawekezaji kuwatumia wazawa katika kufanikisha shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, Sheria mpya imeweka wazi masuala mbalimbali yanayopaswa kufanywa na wazawa na manunuzi ya baadhi ya mahitaji kufanyika ndani ya nchi na si vinginevyo ikiwa ni pamoja na kuajili wazawa.

Mwisho Naibu Waziri Nyongo alizungumzia suala la kuzuia wawekezaji kumiliki leseni wasizozifanyia kazi. Alisema  kuwa, wapo  baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakitumia leseni za madini  kuombea mikopo katika taasisi za kifedha nje ya nchi na baada ya kupata mikopo hiyo wamekuwa  wakiendesha shughuli zao nje ya Tanzania.

Alibainisha kuwa, ili kuwabana wawekezaji hao sheria imekuja ikiweka wazi muda maalum wa mmiliki wa leseni kumiliki leseni hiyo vinginevyo maeneo yanarudishwa serikalini ili kutoa fursa kwa watu wenye nia ya kufanya kazi kuendelea na kazi. 


Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akifuatiwa na Naibu Waziri Stanslaus Nyongo wakiwa katika kikao kifupi na Balozi wa Canada nchini Pamela O’Donnel. Kushoto ni Kamishna wa Madini nchini Mhandisi David Mulabwa. 

Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akiagana na Balozi wa Canada nchini mara baada ya kumaliza kikao baina yao. Katikati ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto), akizungumza jambo wakati wa kikao na Balozi wa Canada nchini Pamela O’Donnel (wa pili kutoka kushoto).
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango (Kulia), katikati ni Katibu wa Waziri Kungulu Masakala wakifuatilia hoja kutoka kwa Balozi wa Canada nchini Pamela O’Donnel (Hayupo pichani)

No comments:

Post a Comment