Na Nuru Mwasampeta
Waziri wa Madini,
Doto Biteko ameutaka uongozi wa mgodi wa North Mara kutii Mamlaka ya Serikali
kwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na mamlaka za Serikali nchini.
Biteko alitoa kauli
hiyo Jana tarehe 17 mwezi Januari katika kikao kilichoanza kwa utulivu mkubwa
lakini kadri dakika zilivyokuwa zikisonga mbele kiligeuka kichungu na
kuwapelekea wajumbe kutoka mgodi wa North Mara na Bulyanhulu kuridhia kuanza
kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka mgodi huo ambao wamekaa kwa muda mrefu
pasipo kulipwa fidia zao.
Katika kikao hicho,
Waziri wa Madini, Doto Biteko, alianza kwa kuwahoji viongozi wa mgodi wa North
Mara na Bulyankulu juu ya changamoto
kubwa iliyopo katika eneo lao ambapo bila kusita walikiri wazi kuwa ni suala la
malipo ya fidia ya ardhi kwa wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
Akizungumzia
ukiukwaji katika kutekeleza maagizo ya Serikali Waziri Biteko aliwaeleza
wajumbe hao kuwa ili kuonesha wanatii mamlaka ya Serikali walipaswa kuwa
wamechukua hatua kadhaa katika kuelekea kutatua changamoto hiyo.
Biteko alionesha
kusikitishwa na mwitikio unaooneshwa na wawekezaji hao ambao kutoka kikao cha
mwisho kilipokaa na kuafikiana kuanza kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi
wanaozunguka mgodi huo ni miezi minne na hakuna chochote kilichofanyika.
“Hatuwezi kuwa
tunakaa, tunafikia maamuzi ninyi mnayapinga, ni nani yupo juu ya Serikali”
Waziri Biteko alihoji. “Mnajua suala la ardhi ni kubwa sana, mnajua ni
maelekezo ya Rais, sasa Rais ameagiza halafu hakitokei kitu! Mimi sielewi
kabisa. Afadhali watu wangeanza kulipwa unaweza sema sasa hatua za malipo
zinafanyika lakini kuko kimya”aling’aka.
Akizungumzia chanzo
cha mgogoro kuchukua muda mrefu Biteko alisema ni tathmini iliyofanyika kwa
mara ya pili kupelekea kiasi cha fidia
mgodi unaopaswa kuwalipa wananchi kuongezeka kutoka bilioni 1.6 hadi kufikia bilioni 12.
Akifafanua hilo mara
baada ya kuzungumza na mthaminishaji Mkuu wa Serikali (jina halikupatikana) kwa
njia ya simu, Biteko alisema ameelezwa kwamba tathmini inayofuatwa ni ile
iliyofanyika kwa mara ya pili maana hiyo ndiyo current na kukazia kuwa hawawezi
kufuata ya awali kutokana na kwamba muda wa kuwalipa fidia hizo ulipaswa
kutokuzidi miezi sita tangu tathmini kufanyika.
Ilielezwa kwamba,
mara baada ya tathmini kufanywa kwa ajili ya malipo ya fidia, haipaswi kuzidi
miezi sita na baada tu ya tathmini kufanyika; walipaswa kutoa tangazo ili
kusimamisha uendelezaji wa maeneo ili kutokuongeza uwekezaji utakaopelekea
wananchi kulipwa zaidi.
Biteko alieleza kuwa wananchi
wanaomiliki maeneo hayo wakiendelea kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo
yao baada ya miezi sita kutoka tathmini ilipofanyika ni dhahiri kuwa gharama ya
kumlipa fidia mwananchi huyo itaongezeka tu.
Aidha, Biteko
aliwaeleza wajumbe hao kuwa uongozi wa mgodi huo hawazifuati mamlaka husika katika
kutatua changamoto hiyo na kubainisha kuwa mgogoro huo hautatatuliwa na wizara
ya Madini isipokuwa ni watu wenye mamlaka na masuala ya ardhi.
Akijibu hoja ya mmoja
kati ya wajumbe kutoka North Mara aliyejaribu kueleza kuwa kiongozi mkuu wa
masuala ya kisheria katika mgodi huo anayeishi nchini Uingereza ni sharti
aelezwe pindi maamuzi na maagizo yeyote yanapopokelewa katika mgodi ili kufanya
maamuzi yanayokidhi matakwa ya mgodi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof.
Simon Msanjila alihoji endapo north Mara ipo juu ya Serikali?
Prof. Msanjila aliendelea
kwa kusema haiwezekani mtu asiyekuwa na maamuzi katika mgodi kushiriki katika
vikao vinavyojadili na kutoa maamuzi halafu mtu asiyeshiriki katika vikao hivyo
akapinga maamuzi hayo.
“Yaani Waziri atoe
maamuzi halafu mtu aliyeko Uingereza ayapinge that is totally subbodination maamuzi ya mwisho yakishafanywa na Serikali hakuna
serikali nyingine au kampuni yoyote ile iyapinge! Maamuzi yanayotolewa Tanzania
hayawezi kwenda kujadiliwa London sio
Sheria hiyo, ndio maana kampuni lazima iwe imesajiliwa Brella, kwa hiyo mambo
ya kusema mshauri yupo London, South Africa No”. Alikazia Msanjila
“Don’t talk about London or South
Africa tunapoongelea masuala ya Tanzania tunaongea kwa sheria za Tanzania we have nothing to do with London hiyo ni yao” alisisitiza.
Msanjila aliwakumbusha
makubaliano waliyoafikiana katika vikao vya nyuma kuwa yaliyowataka wajumbe wa
vikao vya maamuzi wasiokuwa na nguvu ya kufanya nakutekeleza makubaliano ya
kikao wasishiriki katika vikao hivyo ili kuepuka kupotezeana muda.
Huyu ni waziri,
anamwakilisha Rais, hamuwezi kwenda kuomba ushauri London kwa maagizo yaliyotolewa na waziri, hiyo si sheria. Prof.
Msanjila Alikazia.
Baada ya mahjiano
makali na yaliyochukua muda mrefu kikao kilifikia muafaka na ujumbe kutoka
North Mara kukiri kuwa kutokana ukweli kwamba baadhi ya wananchi waliofanyiwa
tathmini malipo yao hayana shida watakwenda na kuanza kufanya taratibu za
malipo.
Walikiri kuwa mara
baada ya kufika katika vituo vyao vya kazi watakwenda kuendelea na taratibu za
malipo ili kuonesha uungwana na kuionesha Serikali na jamii kuwa wamechukua
hatua kwa makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wakuu wa nchi.
Aidha, walikiri kuwa
wamejifunza kitu kutokana na kikao hicho na kukiri wanaendelea kujifunza kwani
wameona madhara makubwa katika kuchelewesha malipo hayo na kuipelekea kampuni
hasara kwa kulipa zaidi ya mara mbile ya kile walichotakiwa kulipa awali.
Zaidi ya hapo,
wamejifunza juu ya uhalisia wa kisheria upande wa tathmini ya ardhi kuwa huwa hai kwa kipindi cha miezi sita na ikizidi hapo
inafanyika tathmini nyingine lakini pia wamejifunza juu ya taratibu na sheria
za kusitisha shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa kutangaza kusimamisha
shughuli za maendeleo katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini kwa kipindi cha
miezi sita na pia kulipa fidia kwa wakati ili wananchi wakajiendeleze katika
maeneo mengine watakayohamia.
Aidha, Bi Jane
Reuben- Lekashingo alisema kuwa si lengo lao kupinga maamuzi ya serikali ila
wanachelewa kutokana na taratibu za kiutendaji wanaazopaswa kuzifuata ili kukidhi matakwa na taratibu za kampuni katika kutekeleza majukumu yao na
kukiri kuwa sasa watasimamia sheria za nchi na kutekeleza makubaliano
yaliyofikiwa katika vikao vya maamuzi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko, akiwasomea viongozi
wa north Mara baadhi ya taarifa alizonazo
juu ya masuala ya tathmini za fidia ya ardhi zilizofanywa namatokeo yake
pamoja na kile wanachopaswa kuwa wamekitekeleza mpaka siku ya kikao hicho
tarehe 17 Januari, 2019
Katibu Mkuu wa madini, Prof. Simon Msanjila akihoji
uhalali wa Maelekezo ya Seikali kupingwa na viongozi wa Mgodi wanaoishi nnje ya
Tanzania (Uingereza na Afrika Kusini) na wasioshiriki katika vikao vya mamuzi.
Waziri wa Madini, Doto Biteko, akiwasomea viongozi
wa north Mara baadhi ya taarifa alizonazo
juu ya masuala ya tathmini za fidia ya ardhi zilizofanywa namatokeo yake
pamoja na kile wanachopaswa kuwa wamekitekeleza mpaka siku ya kikao hicho
tarehe 17 Januari, 2019
Msaidizi wa Waziri Kungulu Masakala ( wa Kwanza
Kushoto), Wawakilishi kutoka Tume ya
Madini, na Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Sera na Mipango Glads Qambaita
wakiwa katika kikao baina ya Wizara chini ya Waziri wa Madini, Doto Biteko
(hayupo pichani) na uongozi wa mgodi wa
North Mara.
Viongozi wa mgodi wa North Mara nchini wakiwa
katika kikao na Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo Pichani) kilichofanyika
katika ofisi za wizara jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment