Na
Asteria Muhozya, Mbinga
Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo amesema Wizara yake itafanya mazungumzo na Mamlaka zinazohusika na masuala ya barabara ili kuweka mazingira bora ya
miundombinu hiyo kwa lengo la kuwezesha biashara ya makaa ya mawe na
shughuli za uzalishaji makaa hayo kufanyika kwa ufanisi zaidi katika mgodi wa
makaa ya mawe Ngaka, uliopo wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Alisema mgodi huo wa
Ngaka chini ya kampuni ya TANCOAL ndiyo taswira ya uzalishaji makaa ya mawe
nchini hivyo, serikali haina budi kuweka mazingira bora yatakayowezesha kupunguza
gharama za uendeshaji jambo ambalo litapunguza gharama kwa walaji wa nje na
ndani ikizingatiwa kuwa, ni kampuni ya Kimataifa kutokana na kuhudumia wateja
kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Uganda nchi na nyingine.
Kauli ya Naibu Waziri
Nyongo inafuatia changamoto ya barabara iliyowasilishwa kwake na Meneja Mgodi
wa TANCOAL Mhandisi David Kamenya, ambaye alimweleza Naibu Waziri kuwa, ukosefu
wa miundombinu imara ikiwemo madaraja imechangia shughuli za upakiaji makaa
hayo kutokuzidi tani 20 kwa kila gari jambo ambalo linapelekea kuwepo na foleni
kubwa kutokana na uhitaji wa makaa hayo.
Naibu Waziri Nyongo
alifanya ziara mgodini hapo Januari 17 ikilenga kukagua shughuli za madini
mkoani Ruvuma pamoja na kuangalia changamoto mbalimbali ambazo mgodi huo
unakabiliana nazo katika utekelezaji wa shughuli zake.
Pamoja na kuridhia
ombi hilo, Naibu Waziri aliitaka kampuni hiyo kuongeza kasi ya uzalishaji
kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo katika soko la nje na ndani na
kuitaka kutobweteka huku ikitakiwa kuboresha huduma inazotoa ikiwemo kuongeza
vifaa vya kazi.
“Nimeona changamoto
ya barabara. Kama serikali ni lazima tuifanyie kazi changamoto hii ili
kuwezesha uzalishaji zaidi wa makaa. Sisi tutaendelea kutoa leseni kwa wazalishaji
wengine ili kuweka ushindani, hivyo msibeweteke, tunahitaji sana makaa haya kwa
uchumi wa taifa letu kwa kuwa tunayo hazina ya kutosha ya rasilimali hii,”
alisema Nyongo.
Aliongeza kuwa,
kufuatia serikali kuweka zuio la uingizaji makaa kutoka nje, ni lazima kuweka
mazingira bora ya uzalishaji wa madini hayo ikiwemo kuwezesha biashara hiyo na kuutaja mgodi wa makaa ya mawe wa Kabulo
unaomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwa ni eneo jingine
ambalo miundombinu ya barabara ni lazima iboreshwe kuwezesha ufanisi zaidi wa shughuli za uzalishaji
madini hayo.
Alisema kuwa, ili
serikali iendelee kupata mrabaha zaidi kutokana na rasilimali hiyo suala hilo
lazima lichukuliwe kwa uzito ili kuongeza mapato zaidi.
Aidha, akijibu ombi
la kampuni hiyo kutaka kurudishiwa eneo ambalo lilitolewa kwa ajili ya Kiwanda
cha Dangote na Rais John Magufuli, kwa kuwa bado haijanza kuchimba mpaka sasa,
Naibu Waziri Nyongo alizitaka pande zote ikiwemo wizara na kampuni hizo
kukutana Januari 22 mara baada ya kikao cha wadau wa sekta ya madini ili
kujadili suala hilo ili hatimaye shughuli za uzalishaji zianze katika eneo
hilo.
Mbali na hilo,
kampuni hiyo ilimwomba Naibu Waziri kuwezesha upatikanaji wa leseni mbili zilizoombwa na kampuni hiyo ikilenga
kutumia makaa hayo kuzalisha umeme kwa
ajili ya matumizi ya mgodi. Naibu Waziri aliahidi kuwa, kupitia Tume ya Madini,
suala hilo litakuwa limekamilika ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Nyongo aliitaka Halmashauri ya Mbinga kubuni miradi kwa ajili ya
vijana na wanawake yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya makaa ya mawe kwa
ajili ya matumizi ya majumbani na kuachana na matumizi ya mkaa kwa kuwa umekuwa
ukisababisha uharibifu wa mazingira.
Wakati huo huo, akizungumzia
suala la Mrabaha wa serikali wa asilimia
3, alisema usilipwe kwa bei ya maeneo ya uchimbaji bali ulipwe kwa bei ya sokoni. Hivyo,
aliwataka wazalishaji wote na Maafisa wa Tume ya Madini kuhakikisha wanatoza
bei ya sokoni na siyo ya uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja
wa mgodi Mhandisi David Kamenya akizungumzia ubora wa makaa hayo,
alisema kuwa, Makaa ya Ngaka yana ubora wa kimataifa na ndiyo sababu imepelekea kupata wateja
wengi kutoka nchi mbalimbali na kuongeza kwamba makaa hayo yana uwezo wa
kufanya matumizi mbalimbali na kuongeza kuwa, kwa siku kampuni hiyo inapakia
idadi ya magari yapatayo 100.
AKizungumzia malengo
ya baaaye, alisema kuwa, idadi ya mashine ndani ya siku chache zinatarajiwa
kuongezwa na kwamba kampuni imelenga kuzalisha hadi tani 5,000 kwa siku kutoka
3,000 za sasa.
Akizungumzia
uwezeshaji kwa vijana na akina mama, alisema kuwa, tayari kipo kikundi cha wakina
Mama cha Mbarawala ambacho kimewezeshwa na
mgodi huo kwa kupatiwa mafunzo ya
namna ya kuandaa makaa hayo maalum kwa matumizi ya majumbani na kuongeza kuwa,
hivi karibuni kikundi hicho kimepata
Cheti cha ubora kutoka shirika la Viwango nchini (TBS) jambo ambalo litawezesha
kikundi hicho kuuza makaa yake kwa ajili
ya matumizi ya majumbani na hivyo kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na
kukatwa miti.
Pia, Mhandisi Kamenya alimweleza Naibu Waziri
Nyongo kuwa, mbali na kupatiwa mafunzo kikundi hicho pia kimepatiwa mashine
ambayo inauwezo wa kuzalisha tani mbili za makaa hayo kwa saa.
Akishukuru kwa niaba
ya kikundi, Meneja Usimamizi wa Mbarawala, Joyce Haule alisema kuwa, wanaishukuru kampuni hiyo kwa kuwawezesha
na kwamba kikundi kinalenga kuzalisha
tani 10 kwa siku na kuongeza kuwa, hadi sasa tayari kimepata wateja kutoka
maeneo mbalimbali zikiwemo nchi za Rwanda ambao
awali walitaka kwanza kikundi hicho
kuwa na cheti cha ubora wa makaa hayo.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Ishenyi alimweleza Naibu Waziri kuwa, kama Wilaya
itahakikisha kuwa, inashirikiana na mamlaka zinazohusika kuweka mazingira bora
ya kuwezesha mundombinu bora ya barabaraba
ili TANCOAL iweze kufanya shughuli zake kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua
nyingine, akizungumza na Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Prof. Riziki Shemdoe,
ofisini kwake Januari 18, Naibu Waziri alimweleza Prof. Shemdoe umuhimu wa
kuwezesha miundombinu ya barabra kuelekea katika mgodi huo wa Ngaka.
Pia, Naibu Waziri
alimweleza Prof. Riziki kuhusu mipango ya Serikali ya kuwa na vituo kwa ajili
ya biashara ya madini na umuhimu wa mikoa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli
hizo. “ Tunataka kuwa na utaratibu wa kuwa na maeneo ya kuuza na kununua madini
ili kuwa na utaratibu maalumu,”
aliongeza.
Kwa upande wake,
Prof. Shemdoe alimwomba Naibu Waziri kusaidia upatikanaji wa wawekezaji kwa
ajili ya viwanda vya kuchenjua dhahabu mkoani humo na kukumbushia suala la
uchimbaji madini katika Mto Muhuwesi.
TANCOAL ni kampuni
yenye ubia na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambapo
serikali inamiliki hisa kwa asilimia 30.
Baadhi ya magari yakisubiri kupakia makaa ya mawe
tayari kwa kusafirishwa maeneo mbalimbali ndani nan je ya nchi,
|
Sughuli za upakiaji Mkaa ya Mawe zikiendelea
katika Mgodi wa TANCOALtayari kwa ajili ya kusafirishwa maeneo mbalimbali.
|
No comments:
Post a Comment