Na
Asteria Muhozya, Ludewa
Wizara ya Madini imesema
itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la
Maendeleo ya Taifa (NDC) kuweka msukumo ili kuhakikisha kwamba miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na
ule wa Chuma Linganga inaanza kutekelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa
Januari 16 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua
shughuli za madini mkoani Njombe na kuona
namna ya kutatua changamoto zinazohusu Wizara
ya Madini katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema miradi hiyo
ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo Taifa linatarajiwa kunufaika kwa kiasi
kikubwa, hivyo kutokana na umuhimu wake, wizara ya madini itashirikiana na
wizara hiyo kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili hatimaye miradi hiyo ianze
kutekelezwa kwa kuwa imechukua muda mrefu.
Aliongeza kuwa, ni
miradi mikubwa ambayo taifa linatarajiwa kunufaika nayo kupitia ajira
na kuongeza pato la nchi huku akiyataja madini ya chuma kuwa moja ya malighafi muhimu kwa uchumi wa Tanzania ya viwanda na kusema kuwa, kama taifa, linautolea macho
mradi huo na kwamba serikali imedhamiria kuutekeleza.
Aliongeza
kwamba, katika Serikali ya Awamu ya Tano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Magufuli anayo imani kubwa
kuwa miradi hiyo itaanza
huku serikali ikitegemea kupeleka
maendeleo kwa wananchi kupitia
miradi husika.
“Wizara yetu ndiyo inatoa leseni za madini na tayari
tulishatoa leseni ya Makaa ya mawe mchuchuma kwa hiyo nimefika kuangalia
changamoto ambazo ziko upande wa wizara yetu kuweza kuzitatua ili tutoke hapa.
Miradi hii tumeisikia miaka mingi ni wakati sasa tunataka ianze.” alisisitiza
Nyongo.
Aliongeza
kuwa, ikiwa wizara ndiyo inatoa leseni za madini, inaowajibu wa kujua yule aliyepewa leseni
kama anaifanyia kazi na kuongeza, “Sisi tuliotoa leseni lazima tuangalie
tuliyempa leseni amekwama wapi lakini
pia tujue miradi hii inaanza lini? Makaa
ya mawe na chuma vyote vinahitajika kwa taifa. Tunatambua makaa ya mawe ni
madini ambayo yana tija kwa uchumi kwa nchi,” alisema Nyongo.
Akifafanua zaidi
kuhusu miradi hiyo alisema kuwa, mradi wa Makaa ya Mawe unatarajiwa kuzalisha
umeme ambao mbali ya kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umeme huo
unatarajia kutumika katika kuzalisha madini ya Chuma Liganga.
“Mpango ni Liganga kutumia megawati 250 kwa
shughuli zake za kuzalisha chuma na megawati 350 zitauzwa Tanesco kuzalisha
umeme,” aliongeza.
Akifafanua sababu za
kuchelewa kwa miradi hiyo, alisema ni kutokana na changamoto za kimkataba
ambazo bado ziko katika majadiliano katika ngazi za juu na kuitaja baadhi ya
mikataba hiyo kuwa ni kuwa ni pamoja na
mikataba ya upunguzaji wa kodi.
Aliongeza kuwa,
wizara ya madini ikiwa ni wizara ambayo inasimamia Sheria ya Madini, imelenga
kuhakikisha kwamba miradi hiyo mikubwa inaanza ili hatimaye iweze kuwanufaisha
watanzania na taifa.
Akielezea suala la
fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, alianza kwa kumpongeza Mkuu wa
Wilaya ya Ludewa kwa kutenganisha suala la miradi hiyo na fidia ambapo alisema kwamba taratibu za juu
zikikamilika, wananchi watalipwa fidia
na hivyo kuwataka kuwa na subira na kuwa tayari kupisha utekelezaji wa
miradi hiyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole
Sendeka alimweleza waziri umuhimu wa wizara ya madini kujielekeza kwenye kupata taarifa halisi kuhusu tafiti
zilizofanyika awali kuhusu akiba iliyopo
ya madini ya chuma Liganga na Makaa ya
Mawe mchuchuma.
Aidha,
aliongeza kuwa, mbali na chuma na makaa ya mawe mkoa huo unayo madini
mbalimbali ikiwemo dhahabu ambayo bado haijachimbwa kwa kiasi kikubwa.
Miradi
ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga, inatekelezwa kwa ubia kati ya
Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni ya
Sichuan Hongda Group Ltd, ya China.
Pia,
akiwa mkoani humo, Naibu Waziri alitembelea mgodi wa Kokoko Kokoto wa Nyakamtwe
Quary, ambapo alitoa changamoto kwa mmiliki wa mgodi huo kuongeza kasi ya
uzalishaji na kuwa wabunifu kutumia fursa
za miradi mikubwa ya ujenzi
inayotekelezwa na serikali ikiwemo ya ujenzi wa reli ili kokoto hizo
ziweze kutumika.
Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza Meneja wa mgodi wa Kokoto wa Nyakamtwe
Quary, uliopo mkoani Njombe alipoutembelea
wakati wa ziara yake hivi karibuni. Mhagama ni mmoja wa wanufaika wa ruzuku
iliyotolewa awali na Serikali kwa
wachimbaji wadogo . Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Ruth Msafiri.
Mtaalam
kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mhandisi Paschal Malesa, akimweleza
jambo Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati alipotembelea mradi wa
Liganga uliopo Wilayani Ludewa mkoani Njombe. Naibu Waziri Nyongo alitembelea
kujua maendeleo ya utekelezaji mradi huo ikiwemo kujua changamoto ambazo ziko upande wa Wizara inaweza ili izifanyie kazi kuhakikisha kwamba mgodi
huo unatekelezwa kama ilivyopangwa.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiangalia makaa ya katika mgodi wa Liganga
alipoutembelea hivi karibuni. Naibu Waziri alifanya ziara hiyo kwa lengo la
kujua changamoto za utekelezaji wa mradi huo. Anayemweleza jambo ni Mtalaam kutoka
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mhandisi Paschal Malesa.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akitoka katika Ofisi za Wilaya ya Ludewa tayari kwa ziara ya kutembelea katika mgodi
wa Liganga kwa ajili ya kujionea changamoto za utekelezaji wa mradi huo.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume
ya Madini wakifuatilia kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher
Ole Sendeka. (hayupo pichani) Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth
Msafiri.
Mkuu
wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akimsikiliza akimweleza jambo Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake mkoani humo.
No comments:
Post a Comment