·
Watoa
pongezi kwa Mwenyekiti Tume ya Madini
Na
Greyson Mwase, Dodoma
Kikundi cha
wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na
uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo
katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu”
kimepongeza Tume ya Madini kwa kutatua mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu pamoja
na kuwapatia leseni.
Pongezi hizo
zimetolewa leo tarehe 16 Januari, 2019 katika makabidhiano ya leseni ya
uchimbaji wa madini hayo katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma
zilizopo jijini Dodoma.
Kutatuliwa kwa
mgogoro kati ya kikundi hicho na wananchi wa kijiji cha Suguta ni matokeo ya
ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliyoifanya mapema
Septemba 05, 2018 katika machimbo hayo na kukuta kikundi hicho kikiendesha
shughuli za uchimbaji wa madini pasipo kusajiliwa na kutokuwa na leseni ya
uchimbaji wa madini.
Mara baada ya kufanya
ziara katika eneo husika Profesa Kikula alielekeza Mwenyekiti wa Chama cha
Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto, Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na Mkuu
wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius John Ndejembi kuhakikisha kikundi cha
wachimbaji hao kinasajiliwa na kupatiwa leseni ndani ya muda mfupi.
Aidha, Profesa Kikula
alimwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Dodoma (DOREMA), Kulwa
Mkalimoto kuhakikisha mgogoro uliokuwepo kati ya kikundi hicho na wananchi wa
kijiji cha Suguta unamalizika.
Akitoa shukrani hizo
kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa kikundi cha
“Hapa Kazi Tu” Elisha Cheti alisema kuwa ziara ya Profesa Kikula ilipelekea
kuongezeka kwa kasi ya usajili wa kikundi na hatimaye wakafanikiwa kuomba
leseni ya kuchimba madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Dodoma.
Alisema mara baada ya
kupata leseni pamoja na barua ya utambulisho wanatarajia kuanza shughuli za
uchimbaji madini na kulipa kodi na tozo mbalimbali Serikalini.
Naye Mwenyekiti wa DOREMA, Kulwa Mkalimoto mbali
na kuipongeza na kuishukuru Tume ya Madini kwa utoaji wa leseni amekitaka
kikundi kilichopewa leseni kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa
kufuata sheria na kanuni za madini huku kikihakikisha hakuna uharibifu wowote
wa mazingira.
Naye Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano akizungumza wakati wa makabidhiano hayo
alifafanua kuwa, maombi ya leseni ya uchimbaji wa madini ya kikundi husika
yalipitishwa kupitia kikao cha Kamati ya Ufundi ya Tume kilichokaa tarehe 22
Novemba, 2018.
Mwano alitoa wito kwa
wachimbaji wadogo wasio rasmi kuunda vikundi, kusajili na kuomba leseni na
kusisitiza kuwa ofisi yake itahakikisha leseni za madini zinatolewa kwa kasi ili
waweze kuchimba pasipo kusumbuliwa huku wakilipa kodi na tozo mbalimbali
Serikalini.
“Sisi kama Tume,
tunaamini wachimbaji wadogo wana mchango mkubwa sana kwenye ukuaji wa sekta ya
madini; tunaunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Magufuli za kuhakikisha watanzania wote wananufaika na rasilimali za madini,”
alisisitiza Mwano.
Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) akimkabidhi leseni ya madini Mwenyekiti wa
Kikundi cha wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika
machimbo ya Suguta yaliyopo katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma,
kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi Tu”, Elisha Cheti (kushoto)
Kutoka kulia, Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano, Mwenyekiti wa Kikundi cha
wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na
uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika machimbo ya Suguta yaliyopo
katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, kijulikanacho kwa jina la “Hapa Kazi
Tu”, Elisha Cheti na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa
Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya
makabidhiano hayo.
No comments:
Post a Comment