Na
Asteria Muhozya, Iringa
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo ameamuru kukamatwa kwa Wamiliki wa mgodi wa
Nyakavangala unaomilikiwa na Thomas
Masuka and Partners kufuatia wamiliki hao
kutofautiana juu ya taarifa waliyoiwasilisha kwa Naibu Waziri kuhusu namna
mgodi huo unavyoendeshwa ikiwemo ulipaji wa kodi na mrabaha wa serikali.
Aidha, Naibu waziri
amewataka wamiliki hao kutoa maelezo ya kina kuhusu ni lini watalipa kodi zote
wanazodaiwa na serikali baada ya kuonekana kuwa mgodi huo unadaiwa zaidi ya
shilingi milioni 128 za mrabaha ambazo imedaiwa kuwa, wapo baadhi ya wamiliki
ambao wamekuwa wakikusanya fedha hizo lakini zimekuwa hazilipwi.
Katika ziara yake mkoani
humo, Naibu Waziri alisema kuwa pamoja na kujionea shughuli za uchimbaji katika
migodi ya dhahabu ya Ulata na Nyakavangala, amebaini ukwepaji mkubwa wa kodi
pamoja na mrabaha wa serikali.
Pia, amemtaka Afisa
Madini kutoa maelekezo ya kina kuhusu suala zima la ulipwaji wa kodi na mrabaha
wa serikali, huku akiagiza zoezi hilo pia limuhusishe Afisa Msimamizi wa madini
aliyekuwepo katika kipindi ambacho fedha hizo hazikulipwa.
“Hatutaki ugomvi hapa
kwenye migodi. Tunataka mgodi ufanye kazi. Dhahabu ziuzwe mahali panapoonekana.
Hapa naona hesabu za viroba tu. Mnunuzi wa dhahabu hapa ni nani”, alihoji Naibu
Waziri.
Wakati akizungumza na
wachimbaji katika mkutano wa hadhara, amewataka wachimbaji hao kuchimba kwa
kuzingatia usalama huku akisisitiza
suala la kufuata sheria na taratibu huku
akiwataka kutoa taarifa za uhakika kwa
wale wote wanaokikuka sheria ikiwemo watoroshaji wa madini huku
akisisitiza utoaji taarifa hizo usiwe wa majungu.
Akitolea ufafanuzi
suala la fedha za mrabaha, amesema fedha hizo hazipaswi kuelekezwa katika
masuala mengine na wamiliki wa migodi ikiwemo kutumiwa katika huduma za jamii
badala yake zinapaswa kulipwa
serikalini.
Naye, Mkuu wa Wilaya
ya Iringa Richard Kasesela aliwataka wamiliki hao kukaa chini na kukubaliana
namna ya kulipa kiasi cha fedha ambacho wanadaiwa na serikali huku akimtaka
Afisa kutoka Halmashauri anayehusika na masuala ya usimamizi wa fedha
kuhakikisha kwamba fedha ambazo mgodi huo ulipaswa kuzilipa kama mrabaha
zinapatikana.
Mgodi huo wa
Nyakavangala unamilikiwa na Thomas Masuka kwa ushirikiano na wawekezaji wengine
wazawa wapatao 20. Wakati akiagiza kukamatwa kwao, wamiliki 8 kati ya 20 ndiyo
walikuwa wamehudhuria kikao kati yake na wamiliki hao.
Naibu Waziri Nyongo
alitoa agizo hilo Januari 15 wakat akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani
humo.
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo akijaribu kupandisha Kamba zinazotumika kungia na
kutoka ndani ya migodi katika moja ya mgodi wa dhahabu, Kavangala.
Sehemu ya wachimbaji
wadogo wakifuatilia mkutano baina yao na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo. (Hayupo pichani)
Afisa Madini
anayesimamia Mikoa ya Iringa na Njombe Wilfred Machumu akieleza jambo wakati wa
kikao baina ya Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo na wamiliki wa mgodi wa
Thomas Masuka and Partners. Kulia ni Naibu Waziri Nyongo. Nayefuatia ni
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
Naibu Waziri wa
Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza mmoja wa wawekezaji katika eneo la
Nyakavangala Kazi Kuboma alipofika
katika eneo lake ili kuona namna anavyoendesha shughuli zake uchenjuaji madini. Wengine ni Mkuu wa Wilaya
ya Iringa, Richard Kasesela na Maafisa Madini na Maafisa wa Wilaya.
No comments:
Post a Comment