Na Greyson Mwase,
Nzega
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula leo tarehe 06 Desemba 2018 ametatua mgogoro
uliodumu kwa muda mrefu kati ya vikundi viwili vilivyokuwa vinajishughulisha na
shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Mwamikola lililopo
Wilayani Nzega mkoani Tabora.
Vikundi hivyo ni
pamoja na kikundi cha Mwaguguli Mining Society na kikundi cha Mwamikola Gold
Mining Society ambapo mgogoro wao ulitokana na mwingiliano wa maombi ya leseni
za uchimbaji mdogo wa madini.
Profesa Kikula
aliyekuwa Wilayani Nzega kwa ajili ya kutatua mgogoro huo aliambatana na
watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Dk.
Athanas Macheyeki, Meneja wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Zephania
Maduhu na Mwanasheria kutoka Tume ya Madini, Hadija Ramadhani.
Wengine waliokuwepo
katika ziara hiyo ni pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi
Makolobela, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Onesmo Kisoka, Vyombo vya Ulinzi
na Usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Mara baada ya kufanya
mazungumzo na pande zote mbili kwa pamoja, Profesa Kikula alitoa maelekezo
kulingana na sheria ya madini kwa kusema
kuwa maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society hayakustahili kupewa
leseni kwa kuwa yameombwa kabla ya leseni iliyokuwepo kumaliza muda
wake kinyume na Kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na
Marekebisho yake ya Mwaka 2017.
Profesa Kikula
aliongeza kuwa ombi la kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society linastahili
kupewa leseni kwa vile liliombwa baada ya leseni ya awali kumaliza muda wake na kuongeza kuwa, baada ya
maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society kukataliwa kupewa leseni,
kulingana na Sheria ya Madini kikundi husika kinaweza kuomba tena eneo ambalo haliingiliani na eneo la ombi la
Mwamikola Gold Mining Society.
Awali akielezea
historia ya mgogoro huo, Profesa Kikula alisema kuwa mgogoro huo uliopo katika
kijiji cha Mwamikola, Kata ya Mwangoye Wilayani Nzega mkoani Tabora ulitokana
na mwingiliano wa maombi ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini.
Alisema maombi ya
vikundi hivyo kwa ajili ya uchimbaji wa madini yaliombwa katika eneo la
leseni ya utafutaji wa madini ya kampuni
ya Resolute Tanzania Limited iliyotolewa Machi 14, 2014 na kumaliza muda wake
Julai 13, 2018.
Aliendelea kusema
kuwa eneo linaloombewa leseni lilivamiwa na wachimbaji wadogo mwezi Januari, 2017 na kuongeza kuwa Tume ya
Madini ilisimamisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo mapema Agosti mwaka
huu kufuatia kuibuka kwa mgogoro baada
ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao.
Aliendelea kueleza
kuwa Septemba 13 mwaka huu, Tume ya Madini ilituma wataalam wake kufanya
ukaguzi katika eneo la mgogoro na kuonekana kuwa mgogoro husika ulitokana na
wachimbaji waliovamia eneo hilo kugawanyika na kuunda vikundi viwili ambavyo
vimeomba leseni ndogo ya uchimbaji wa madini.
Profesa Kikula
aliendelea kufafanua kuwa, kikundi cha Mwaguguli Mining Society kiliwasilisha
maombi yake ya leseni tatu za uchimbaji mdogo wa madini Julai 13, 2018 huku kikundi cha Mwamikola
Gold Mining Society kikiwasilisha maombi ya leseni ya uchimbaji mdogo wa madini
katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora katika eneo lililokuwa
linachimbwa wakati wa uvamizi Agosti 06, 2018.
Alisisitiza kuwa
ilionekana sehemu ya eneo la maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society
inaingiliana na eneo la ombi la kikundi cha Mwamikola Gold Mining.
Katika hatua nyingine,
Profesa Kikula alisema Serikali kupitia Tume ya Madini ipo tayari kusaidia
vikundi vyote katika maombi mapya ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini kwa
haraka ili waweze kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini na kujipatia
kipato huku Serikali ikipata mapato yake stahiki.
Alimwagiza Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi Makolobela kuhakikisha anasaidia kwa
haraka vikundi husika katika upatikanaji wa leseni mpya za uchimbaji mdogo wa
madini ili waendelee na shughuli za uchimbaji wa madini na kukuza uchumi wao
uliokuwa umesimama kutokana na usitishwaji wa shughuli za uchimbaji wa madini
katika eneo husika kutokana na mgogoro.
Wakizungumza katika
nyakati tofauti mara baada ya maamuzi kutolewa na Serikali kupitia Tume ya
Madini, viongozi wa vikundi husika waliipongeza Tume ya Madini kwa utatuzi wa
mgogoro kwa kuwa walikuwa wameathirika kiuchumi mara baada ya shughuli za
uchimbaji wa madini kusimamishwa kutokana na mgogoro husika.
Naye Mfadhili wa
kikundi cha Mwaguguli Mining Society, Shukrani Chacha mbali na kuridhika na
kupongeza uamuzi uliotolewa na Tume ya Madini aliomba wachimbaji kutoka katika
kikundi cha Mwamikola Mining Society kuzika tofauti zao na kuanza upya
ushirikiano ili kila kikundi kinufaike na rasilimali za madini.
Aliongeza kuwa
mgogoro uliodumu kwa kipindi kirefu haukuwa na tija kwenye uzalishaji badala
yake ulipelekea uchumi katika kijiji cha Mwamikola kudorora na kusisitiza kuwa
anaamini mara baada ya kuanza upya kwa shughuli za uchimbaji wa madini uchumi
utakua kwa kasi.
Naye Mwenyekiti wa
kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society, Princh Kissoro aliongeza kuwa
utatuzi wa mgogoro umewapa ari mpya ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini
katika eneo husika mara baada ya kupata leseni mpya za uchimbaji mdogo wa
madini.
Wakati huo huo Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi Makolobela alisema kuwa atahakikisha
vikundi husika vinawasilisha maombi yao upya na kupatiwa leseni ndani ya muda
mfupi ili waendelee na uchimbaji wa madini.
Makolobela aliwataka
wachimbaji wadogo katika mkoa wa Tabora kuomba leseni kwa kufuata sheria na
kanuni za madini na kusisitiza kuwa ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano
muda wowote kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akizungumza na wachimbaji wadogo wa
madini ya dhahabu katika kijiji cha
Mwamikola kilichopo katika Wilaya ya
Nzega mkoani Tabora
|
No comments:
Post a Comment