Na Rhoda James, Dodoma
Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki ameagiza Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd kukamilisha ujenzi
wa Jengo la Wizara ya Madini ifikapo Januari 4 mwaka 2019.
Ametoa agizo hilo
jana tarehe 4 Desemba, 2018 alipofanya ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa ofisi
za Wizara lililopo Ihumwa Jijini Dodoma akiambatana na viongozi wengine
waandamizi wa wizara.
Kairuki alibainisha
kuwa baada ya sikukuu za mwisho wa mwaka, viongozi wote watatakiwa kuhamia katika
eneo hilo kutokana na ukweli kuwa ifikapo Januari 4 jengo hilo litakuwa
limekamilika.
Aidha, Waziri Kairuki
ameshauri kuwa wakati wanaendelea na maandalizi mengine waendelee na manunuzi
ya vifaa, na vifaa hivyo lazima viwe vya viwango ikiwezekana watumie dealers ambao ni wakubwa na wa uhakika.
Kwa upande wake, Mhasibu
Mkuu wa Wizara, Anthony Tarimo alisema kuwa pesa kwa ajili ya ujenzi huo ipo,
wao wanachohitaji ni kujua mkataba ukoje na guarantee
ili pesa kwa ajili ya ujenzi huo itolewe.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Issa Nchasi ameeleza kuwa wamejiandaa
kikamilifu ili kusimamia ujenzi wa Jengo hilo na atateua watu ambao watafutilia
kwa ukaribu shughuli za kila siku za ujenzi wa Jengo hilo.
Vile vile, Mwakilishi
wa Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd, Mhandisi Hagai Mziray amesema wataanza
maandalizi ya ujenzi wa Jengo la Madini mapema tarehe 5 Decemba, 2018 na
watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanakamilisha ujenzi kwa
wakati.
Mziray ameongeza kuwa
Kampuni yao inao uzoefu wa kutosha katika masuala ya ujenzi kwani wamejihusisha
na ujenzi wa majengo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Manispa ya jiji Dodoma, Hosipitali
ya Makole, Hosipital ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi.
Kwa sasa Wizara ya
Madini inatumia Ofisi za Wakala wa Jiologia Tanzania (GST) zilizopo Mjini
Dodoma.
Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki (wa pili kushoto) akiambatana
na Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini mara baada ya kufika katika
eneo la ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Madini eneo la Ihumwa jijini Dodoma.
Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki (wa kwanza) akiondoka eneo la ujenzi wa Jengo la Madini mara
baada ya kukagua eneo hilo ambalo linakhadiriwa kuwa na hekta 3-4.
Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki (wa pili kulia) akijadili jambo na Manaibu Waziri wa Madini,
Doto Biteko (kulia) na Stanslaus Nyongo (wa tatu kulia) na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini Saimon Msajila (kushoto) wengine katika picha ni Viongozi mbalimbali
wa wizara.
Muonekano wa eneo la
ujenzi wa Jengo la Wizara ya Madini.
No comments:
Post a Comment