Friday, December 14, 2018

Naibu Waziri Biteko autaka Mgodi wa MMC kuwalipa fidia wananchi


ü Awataka Wachimbaji kuifahamisha Serikali Mikataba wanayoingia

Na Rhoda James, Morogoro

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ameutaka Mgodi wa MMC kuwalipa fidia wananchi wa vijiji vya Mtukule na Mangae Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro waliopisha mgodi huo kufanya shughuli za uchimbaji lakini hawakuwahi kulipwa fidia zao.

Naibu Waziri Doto Biteko alitoa agizo hilo Desemba 10, 2018 alipotembelea Mgodi wa MMC kwa lengo la kukagua shughuli zinazoendelea mgodini hapo pamoja na kwamba mgodi husika uliagizwa kusimamisha shughuli hizo hadi hapo utakapowalipa fidia wananchi wanaodai haki zao.

Biteko alieleza kuwa, tangu Mgodi huu uanze kazi umekuwa ukiendelea na shughuli za uchimbaji pasipo kuwalipa fidia wananchi wanaouzunguka na hivyo, kuuagiza kuwalipa kwanza wananchi ndipo uendelee na shughuli zake.

“Lipeni kwanza fidia na kama uwekezaji wenu ni halali mtaendelea. MMC hakikisheni wananchi wote wanalipwa haki zao na siyo  shilingi Laki Tano niliyoambiwa kwamba wamelipwa,” alisisitiza Biteko.

Vilevile, Naibu Waziri Biteko alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mwalimu Mohamed Utally kufanya uchambuzi ili kujua wananchi wenye haki ya kulipwa ikiwemo kujua ikiwa ardhi hiyo inamilikiwa na wananchi hao ama mgodi, kujua kiasi cha fidia ambacho kila mmoja anatakiwa kulipwa. “Kama uwekezaji ni wa haki, wananchi wapishe uwekezaji huo,” aliongeza Biteko.

Aliongeza kuwa, maendeleo hayawezi kupatikana ikiwa mgodi na wananchi hawaelewani na hivyo kutoa wito kwa wawekezaji kupitia hatua mbalimbali kabla ya kuwekeza ikiwemo kujitambulisha katika ngazi za Serikali ya Kijiji hadi ya Wilaya.

“Na ili Mgodi upate adhabu ni  lazima shughuli zake za uchimbaji zisimame hadi hapo watakapokuwa wamewalipa wananchi fidia yao, alisema Naibu Madini Biteko.

Pia, alimtaka Mkuu huyo wa Wilaya kushirikiana na  Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA) kulifanyia kazi tatizo la barabara linalowakabili wananchi hao kufuatia hatua ya mgodi huo kubadili matumizi ya barabara iliyokuwa ikitumiwa awali na wananchi hao. Tunataka tuondoe ubabaishaji na uongouongo kwenye Sekta ya Madini,” aliongeza.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Madini Biteko ametoa wito kwa Watanzania wote hususan wachimbaji wadogo kuhakikisha kuwa Serikali inatambua mikataba yao wanayoingia na wawekezaji.

Biteko alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa watanzania hawanyonywi na vile vile wawekezaji hawaingii mikataba ambayo sio sahihi jambo litasaidia serikali kutolaumiwa.

“Sisi watanzania tusiwaingize wawekezaji kwenye migogoro. Madhara  yanasababisha  nchi ya Tanzania kuonekana kwamba inawanyanyasa wawekezaji.Fuateni sheria zilizopo,” alisema Biteko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mwalimu Mohamed Utally alihaidi kuwa atayafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa atayasimamia kuhakikisha kuwa kila mwananchi analipwa haki yake.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katika) akikagua mgodi wa dhahabu wa MMC uliopo Wilayani Mvomero mkoani Morogoro, wakati alipotembelea kukagua mgodi huo. 

Mwakilishi wa Mgodi wa MMC upande wa uzalishaji (wa kwanza kulia), akimwelekeza jambo Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) wakati  wa ziara yake ya ukaguzi wa migodi ya dhahabu Mkoani Morogoro.  

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mwalimu Mohamed Utally (kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko wakikagua uwekezaji uliofanywa na Mgodi wa MMC mkoani Morogoro. 

Wafanyakazi wa Mgodi wa MMC wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipofanya kikao kati yao ili kujua utendaji kazi wao katika mgodi wa MMC uliopo mkoani Morogoro. 

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mwalimu Mohamed Utally akiwahutubia wafanyakazi wa mgodi wa MMC uliopo wilayani Mvomero Mkoani Morogoro. 

Wananchi wa Vijiji vya Mtukule na Mangae wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko.

No comments:

Post a Comment