Na Asteria Muhozya, Kiwira
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema ipo fursa kubwa katika
Migodi ya Kiwira na Kabulo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
na tayari Serikali kupitia shirika hilo, imeanza kufufua baadhi ya mitambo mgodini hapo ikiwemo ya kuchakata madini
hayo.
Waziri Kairuki aliyasema hayo
wakati wa ziara yake alipotembelea katika migodi hiyo mwishoni mwa wiki na
kuchukua fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa Kiwira kutokana na uzalendo waliouonesha kuhakikisha kwamba mgodi
huo unafanya kazi tena.
Aliongeza kwamba, migodi ya Kiwira na Kabulo ni migodi inayotegemeana hivyo serikali imedhamiria kuhakikisha
kwamba machimbo ya chini katika mgodi wa
Kiwira yananza uzalishaji na ikiwezekana kufikia mwakani uzalishaji kupitia
machimbo hayo ufanyike kwa asilimia 100.
Akizungumzia madai ya wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira, alisema tayari
madeni hayo yamekwishaanza kulipwa kila uzalishaji unapofanyika na kuongeza, “
madeni ya watumishi yataendelea kulipwa kila wakati uzalishaji unapofanyika
hivi ndivyo tulivyokubaliana’’.
Aidha, Waziri Kairuki alimtaka
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, kuona namna ya kutoa motisha kwa
wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira hususan wale wanaokaribia kustaafu ikiwa ni
ishara ya kuthamini michango yao kwa kutumikia mgodi huo kwa uzalendo na moyo
wa kujitolea.
Wakati huohuo, akizungumza katika eneo la machimbo ya Kabulo, alisema
kuwa, mgodi huo ulisimama kwa kipindi kirefu hivyo jitihada za serikali ni
kuhakikisha kwamba unaanza tena kufanya kazi ili kuleta tija kwa taifa ikiwemo
serikali kupata mapato.
Aliongeza kuwa, wizara inafanya mashauriano na Wizara ya Nishati ili
kuna namna ambavyo makaa ya mawe katika machimbo ya Kiwira na Kabulo yanaweza
kutumika kuzalisha umeme utakaoingizwa
katika gridi ya taifa na kueleza,
“tutakapokuwa tayari tutaanza kuzalisha megawati 200,”.
Akizungumzia hali ya uzalishaji
alisema kwamba, katika kipindi
cha mwezi Julai hadi Septemba,2018, mgodi wa Kabulo umezalisha tani Laki Mbili na mbili elfu ambazo ni mara mbili ya kile kilichozalishwa
mwaka jana na kuongeza kwamba, tayari
tani elfu 37 zimesafirishwa nje ya nchi.
Aidha, alisema mkakati wa
wizara ni kuongeza matumizi ya makaa ya mawe
na kuutaja mkakati wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya
majumbani ili kuwezesha matumizi ya makaa ya mawe kutumika majumbani badala ya
mkaa ambao unaharibu misitu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa ((STAMICO),
Kanali Mhandisi Syvester Ghuliku, alisema kuwa shirika hilo limefanya ukarabati
wa mtambo wa kuchenjua makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira ambao umegharimu
shilingi milioni 30 pamoja na kufanya ukarabati wa maabara na kununua vifaa
ambavyo vimegharimu shilingi milioni 12 na kuongeza kuwa, hayo yote yamefanyika
ili kuweka thamani ya madini hayo.
Akizungumzia mipango ya shirika alileza kwamba ni kuendelea kuboresha
miundombinu ya mgodi huo kadri uzalishaji unapofanyika likilenga kuhakikisha
kwamba mgodi huo unarejesha uzalishaji wake kama ilivyokuwa awali.
Akizungumzia hali ya uzalishaji
katika machimbo ya Kabulo alisema wateja
wa makaa hayo wamekuwa ni viwanda vya saruji , viwanda vya uzalishaji , nchi za Kenya na Rwanda na kuongeza kuwa, wateja zaidi
wanatarajia kuongezeka kadri uzalishaji unavyoendelea na kuongeza.
Akizungumzia manufaa kwa wananchi wa Kabulo alisema wananchi
wanaozunguka migodi hiyo wamenufaika kwa kupata ajira ndogo ndogo na pia
wanatarajia kunufaika pale mradi wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya
majumbani utakapoanza.
Aidha, alisema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inanufaika
kutokana na kuwepo kwa mgodi wa Kabulo kutokana na tozo zinazolipwa.
Naye, Meneja uzalishaji na
Msimamizi wa Migodi ya Kiwira na Kabulo
Peter Maha, alieleza kuwa, mgodi huo unatarajia kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya wateja wakiwemo wateja wa zamani ambao walikuwa wakipata
makaa hayo kutoka mgodi huo na kuongeza
“ Hata viwanda vipya sasa vitakuwa na
uhakika wa nishati kutokana na makaa tunayoyazalisha hapa,”
Nao, wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira wakizungumza katika kikao baina
yao na Waziri Kairuki, waliitaka serikali kuhakikisha inaufufua mgodi huo
kutokana na manufaa yake kwa taifa na
hususan katika kipindi hiki ambacho kipaumbele cha serikali ni kuwa na Tanzania
ya Viwanda na kuongeza, yapo manufaa makubwa kwa taifa kupitia madini ya makaa
ya mawe ikiwa mgodi huo utarejesha shughuli zake za uzalishaji kama ilivyokuwa
hapo awali.
Pia, waliitaka wizara isaidie kuhakikisha kwamba inakifufua kituo za
zamani cha kuzalisha umeme mgodini hapo wakati ikijipanga kujenga kituo kipya kutokana
na kwamba, endapo nishati hiyo itazalishwa moja kwa moja mgodini hapo itasaidia
kupunguza gharama za uzalishaji.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akipata
ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (
STAMICO), Kanali Mhandisi Syvester Ghuliku wakati wa wa ziara yake alipotembelea mgodi wa Makaa ya
Mawe wa Kiwira.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza
Mtaalam kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakati alipotembelea eneo
la Kabulo ambapo shughuli za uchimbaji makaa ya mawe zinafanywa. Waziri Kairuki
alitembelea eneo hilo ili kujionea shughuli hizo za uchimbaji.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika
picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira
|
No comments:
Post a Comment