Na
Bibiana Ndumbaro, STAMICO
Ziara ya Waziri wa
Madini Angellah Kairuki (Mb) aliyoifanya tarehe 05.11.2018 katika Ofisi za Makao
Makuu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imeleta tija, baada ya Waziri
kuchangia shilingi milioni 24 ili kuongezea nguvu ya kutekeleza mradi Kokoto wa
Shirika hilo; uliopo eneo la Ubenazomozi, mkoani Pwani.
Kairuki alitoa
mchango huo baada ya kuguswa na tatizo la ukosefu wa mitaji ya kutekeleza
miradi, kama lilivyobainishwa katika taarifa ya utendaji kazi ya Shirika hilo iliyowasilishwa
na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku; kwenye
kikao cha pamoja baina ya Waziri, Wafanyakazi na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa
Simon Msanjila.
Fedha hizo
zitaiwezesha STAMICO kufikia bajeti yake ya Shilingi milioni 54 zinazohitajika
kufanya utafiti wa kijiolojia unaolenga kubaini ubora wa mwamba katika eneo la
Chigongwe, ambapo awamu ya kwanza ya mradi wa kokoto wa STAMICO itatekelezwa.
Waziri Kairuki
aliwataka Wafanyakazi kukuza ubunifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa
miradi, huku akiwataka kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuboresha utendaji
kazi wa STAMICO wenye tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Waziri huyo wa Madini
Kairuki na Katibu Mkuu wake Prof. Msanjila, waliipongeza STAMICO kwa kuweka
Menejimenti mpya katika Kampuni yake tanzu ya STAMIGOLD kwani imesaidia
kujiendesha kwa faida, kuimarisha ulipaji madeni na kumudu gharama za
uendeshaji mgodi.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylvester Ghuliku alimshukuru Waziri
Kairuki kwa ziara hiyo na ushirikiano anaoutoa kwa STAMICO ili kuhakikisha
Shirika linakua kwa kasi na kuleta manufaa mapana kwa Taifa na kwa maendeleo ya
Watanzania.
Kanali Mhandisi Ghuliku
alimhakikikishia Waziri kuwa STAMICO imedhamiria kuleta mabadiliko katika
miradi yake kwa kuboresha miundo mbinu ya miradi, mifumo ya uangalizi na
ufuatiliaji na kupunguza gharama za uendeshaji migodi ili kuongeza faida na
tija kwa Taifa.
Akitoa neno la
shukrani, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa STAMICO Meja Luyodrey Masaki amesema
kikao hicho cha pamoja na Mhe. Waziri kimekuwa kichocheo cha uwajibikaji kama
Shirika na kwa mtu mmoja mmoja na amemuahidi kuwa STAMICO itarekebisha
mapungufu yake na kutoa maoni ya maboresho Wizarani, ili kuleta tija kwa
Shirika.
Meja Masaki
alimshukuru Kairuki kwa mchango wake wa Shilingi milioni 24 ambazo zitasadia kutekeleza
mradi wa kokoto wa Ubenazomozi, na hivyo kuwezesha kukidhi mahitaji ya kokoto
katika miradi ya miundombinu ya
barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, sambamba na majengo ya
biashahara, ofisi na makazi.
Mapema mwezi huu Novemba,
Waziri huyo wa Madini aliitembelea STAMICO ikiwa ni ziara yake ya pili kwa
mwaka 2018; iliyolenga kufuatilia utendaji kazi wa Shirika, changamoto zake, mbinu
utatuzi na mwelekeo wa uendeshaji Shirika kwa kasi itakayoleta matokeo chanya
nchini.
No comments:
Post a Comment