Na Asteria Muhozya, Dodoma
Waziri wa Madini Angellah Kairuki tarehe Novemba 8, aliongoza kikao cha
kujadili Maendeleo ya Ujenzi wa Vituo vya Umahiri vinavyojengwa maeneo
mbalimbali nchini.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto
Biteko pamoja na Menejimenti ya Wizara ambapo Mkandarasi SUMAJKT na Washauri Elekezi
kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects
zinazosimamia ujezi wa vituo hivyo walieleza kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa
za ujenzi wa vituo hivyo.
Vituo vya umahiri vinajengwa maeneo ya mbalimbali nchini kupitia Mradi
wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya wizara.
Vituo hivyo vinalenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti wa
madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa
mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.
Vilevile, vinalenga katika kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo
wa madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora
za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki alisisitiza kuhusu kuzingatiwa
kwa ubora wakati wa ujenzi wa vituo
husika na kusisitiza Mkandarasi SUMAJKT kukamilisha ujenzi huo katika muda
uliopangwa.
Vituo vya umahiri viko katika hatua mbalimbali za ujenzi na vinajengwa
Bariadi, Bukoba, Handeni, Musoma, Songea, Chunya, Mpanda na Chuo Cha Madini
Dodoma.
Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 11.9 zinazotokana na mkopo wa Benki ya Dunia.
Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao hicho. |
No comments:
Post a Comment