Na
Rhoda James, Bukombe
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo nchini kuhakikisha kuwa leseni za
uchimbaji Madini zinazotolewa na Wizara kupitia Tume ya Madini ikiwemo mikataba
ya ubia wanayongia na Kampuni mbalimbali kutokuwa chanzo cha migogoro nchini.
Naibu Waziri Biteko
aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akisuluhisha mgogoro uliokuwepo kati ya
Kampuni ya Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman ambaye
aliilalamikia kampuni hiyo kwa kukiuka mkataba waliojiwekea kati yao.
Akizungumza katika
kikao hicho cha usuluhishi, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa, wachimbaji wadogo
wanapoingia mikataba na kampuni yoyote ile yenye nia ya kuwa na ubia na Mzawa ni lazima
wazingatie na kukubaliana juu ya
mikataba wanayoingia kwa kuwa,
pindi taratibu zinapokiukwa zinaichafua
nchi.
“Mikataba hii mnayoingia mjue ya kuwa nyinyi
mnakuwa ni taswira ya nchi sasa mkikiuka mnakuwa mnaichafua nchi yetu, lazima
mzingatie makubaliano mnayojiwekea nyie wote, mwekezaji na mzawa,” alisema
Biteko.
Aidha, aliainisha
baadhi ya masuala ambayo yanatakiwa kuzingatiwa wakati wa kuingia mikataba na
wabia na kueleza kuwa ni pamoja na
kuangalia uhai wa leseni zao, kusajili mikataba yao kwenye Tume ya Madini,
kuhakikisha kuwa eneo au biashara wanayoingia haina migogoro, wazawa kujua kuwa
wanatakiwa kuwa na asilimia angalau zisizopungua 25 na kuhakikisha kuwa kodi
zote za serikali zinalipwa kwa wakati.
Vilevile, Naibu
Waziri Biteko alimtaka, Othman ambaye ni mlalamikaji kuhusu ukiukwaji wa
mkataba kati yake na Kampuni ya Pamoja Mining Ltd kuhakikisha kuwa wanazingatia
sheria zote ili pande zote mbili ziweze kufanya kazi kwa tija na bila kukwepa kodi za serikali.
Pia, alitumia fursa
hiyo kuzitaka Ofisi za Madini kote nchini kuhakikisha kuwa zinaendelea kutoa
elimu kwa wachimbaji wadogo ili matatizo kama hayo yanayojitokeza sasa
yasiendele kujitokeza kwani ni wajibu wa Wizara kuhakikisha kuwa migogoro baina
ya wachimbaji na wawekezaji inakwisha.
Naye, Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda alimshukuru Naibu Waziri Biteko kwa
kusuluhisha mgogoro huo ambao umedumu kwa kipindi kirefu nakueleza kuwa, ofisi
hiyo itaendelea kuzingatia na kutekeleza maagizo hayo kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kulia) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati ya Kampuni ya
Pamoja Mining Ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum Othman (hawapo pichani) katika
Ofisi ya Halmashauri ya Bukombe. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Geita, Daniel Mapunda.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia mbele) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati
ya Kampuni ya Pamoja Mining ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum katika Ofisi ya
Halmashauri ya Bukombe. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Ofisi ya
Madini Geita na kampuni ya Pamoja Mining
Ltd.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia mbele) akisikiliza mgogoro uliokuwepo kati
ya Kampuni ya Pamoja Mining ltd na Mkazi wa Nyarugusu Salum katika Ofisi ya
Halmashauri ya Bukombe. Wengine katika picha ni Wafanyakazi kutoka Ofisi ya
Madini Geita na kampuni ya Pamoja Mining
Ltd.
No comments:
Post a Comment