Na Rhoda James, Geita
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko ameuagiza mgodi wa Nyati Resources ltd uliopo katika kijiji
cha Ngula kata ya Bujula mkoani Geita kutolipa gawio Serikali ya kijiji cha
Ngula kuanzia tarehe 2 Novemba, 2018 ili kutoa nafasi ya uchunguzi kujua ni nani
mmiliki halisi wa eneo hilo la mgodi.
Ametoa agizo hilo
wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 2 hadi 3 Novemba, 2018
iliyolenga kukagua machimbo ya madini katika
Mkoa wa Geita.
Pamoja na ukaguzi
huo, Biteko ameeleza kuwa, ametembelea machimbo hayo ili kutatua mgogoro wa
ardhi uliopo baina ya Kijiji cha Ngula na mkazi wa kijiji hicho Mindi Masasi.
Akizungumza katika
kikao hicho, Biteko ameutaka Mgodi huo wa Nyati Resources ltd kutolipa gawio
kwa kijiji hicho kwa kuwa kuna malalamiko kutoka kwa mkazi wa kijiji hicho
ambaye ni Mindi Masasi.
Biteko ameeleza kuwa
mgodi huo umeanza uzalishaji tangu Desemba, 2017 na umekuwa ukimlipa Mindi
Masasi gawio kwa zaidi ya mwaka kwa kuwa wakati wanaanza uzalishaji wa dhahabu
wamemkuta katika ardhi hiyo ambayo amekuwa akiishi tangu mwaka 1954 lakini sasa
kijiji kinadai kuwa ardhi hiyo ni mali yao na wao ndio wenye haki ya kulipwa
gawio hiyo.
Pamoja na maswali
mengi yanayojitokeza, Biteko amesema ni vyema tuachie mamlaka husika kufanya
uchunguzi kuhusiana na suala hili “Zaidi ya mwaka Masasi amekuwa akilipwa gawio
na mgodi huu, je serikali ya kijiji cha Ngula ilikuwa wapi, mbona serikali ya
kijiji haizungumzii eneo lingine isipokuwa eneo la mgodi,” aliuliza Biteko.
Wakati huo huo Biteko
ameutaka Mgodi wa Nyati Resources ltd kutoa maelezo ni kwa nini tangu mwaka
2017 Desemba walipoanza uzalishaji wa dhahabu wamelipa Mrabaha wa kiasi cha
Shilingi 200,000/- tu wakati mapato yao ni zaidi ya milioni 50.
“Huo ni ukiukwaji wa
ulipaji wa kodi za Serikali, haiwezekani tangu mwaka jana hadi leo mmefanikiwa
kulipa Mrabaha wa laki mbili tu,” alisema Biteko.
Aliongeza kuwa lazima
wazawa kuonesha mfano mzuri wa kulipa kodi ili hata wawekezaji kutoka nje ya
nchi wakija waone umuhimu wa kulipa kodi.
Kwa upande wake
Meneja wa Mgodi wa Nyati Resource ltd, Christopher Nilla amekiri kuwa kweli
kumekuwepo na mapungufu katika ulipaji wa kodi za Serikali lakini na kuahidi
kubadilika na kulipa sawasawa na sheria ya madini na kubainisha kuwa wanamiliki mgodi mwingine ambapo zaidi ya Tsh
milioni kumi zimelipwa serikalini.
Mkazi wa kijiji cha
Ngula, Mindi Masasi (kushoto) akimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko
(hayupo pichani). Katikati ni Mtoto wa Mindi Masasi, Makanika Chalo pamoja na Mwenyekiti wa kata ya
Bujula (jina halikupatikana)
Naibu Waziri wa
Madini, Dotto Biteko akihutubia wananchi wa kijiji cha Ngula na wachimbaji
wadogo wadogo wa mgodi wa Nyati Resources Ltd (hawapo pichani) katika mkoa wa
Geita tarehe 2 Novemba, 2018
Naibu Waziri wa
Madini, Dotto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ngula mara baada ya
kukagua Mgodi wa Nyati Resources Ltd uliopo katika kijiji cha Ngula kata ya
Bujula mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment