Na Rhoda James, Morogoro
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameiagiza Tume ya
Madini kufuatilia madeni yote ya ada ya mwaka (Annual Rent) na kutoa muda kwa
wahusika ili walipe ada hizo na endapo watashindwa kulipa katika muda
watakaopewa, wapelekwe Mahakamani.
Naibu Waziri Biteko ameyasema hayo Novemba 12, wakati
akifungua mafunzo ya Wahasibu wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kutoka
maeneo mbalimbali nchini wanaohudhuria mafunzo hayo yanayohusu Mfumo wa
Serikali wa Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Mapato (Goverment E- Payment
Gateway – GePG). Mafunzo hayo yanafanyika
katika chuo cha Mazimbu Campus Solomn Mkoani Morogoro.
“Serikali inadai madeni mengi ya ada za mwaka, mfano kuna
mtu moja ana leseni 103 na anaendela kuomba leseni nyingine lakini pia huyo mtu
anadaiwa pesa nyingi za ada ya mwaka,” amesema Biteko.
Naibu Waziri Biteko amesisitiza kuwa lengo la mfumo huo ni
kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupunguza mianya ya
upotevu wa mapato kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi zote za
Serikali.
Pia, Naibu Waziri Biteko ameongeza kuwa, ili kuleta tija
na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, Mfumo wa GePG umeunganishwa
na taasisi zinazotoa huduma za fedha kama vile Simu Benking za NMB na CRDB
pamoja na Kampuni za Simu ambazo zinatoa huduma kupitia matawi, mawakala na
mitandao ya simu lengo likiwa ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali
kwa kutumia mfumo huo.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Biteko amesema kuwa mafunzo
hayo yapo kisheria na yanatokana na kifungu cha 44 cha Sheria ya Fedha ya mwaka
2017 (The Finance Act, 2017) ambapo Wizara iliunganishwa rasmi kwenye mfumo huo
mwezi Septemba, 2017.
Naibu Waziri Madini Biteko ameongeza kuwa, mnamo tarehe 4
Septemba, 2017 Serikali ilitoa Waraka wa Hazina Na. 3 kuhusu kutumia mfumo wa
Serikali wa Kielektroniki katika Ukusanyaji wa Mapato lengo likiwa ni
kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli kuhusu kujengwa kwa mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa
mapato yote ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko amewapongeza
Wahasibu wote kwa kufanikiwa kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 310 katika
mwaka wa fedha 2018/19 na kueleza kuwa, mpaka kufikia tarehe 31 Oktoba, 2018
jumla ya maduhuli yenye thamani ya shilingi bilioni 111 yamekusanywa ambapo ni
asilimia 36 ya lengo ambalo wizara iliwekewa
kwa Mwaka wa Fedha wa 2018/19.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume, Prof. Shukrani
Manya amesema kuwa, Mafunzo hayo ni muhimu kwa Tume ya Madini na kwamba
yataleta fursa mbalimbali kama vile kujifunza na kuboresha utendaji wa wahasibu
katika Tume ya Madini.
Mafunzo kama hayo yalifanyika katika Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo tarehe 28 hadi 31 Agosti, 2017. Kwa mwaka huu,mafunzo haya
yameanza leo Novemba 12 na yanatarajia kukamilika tarehe 15 Novemba, 2018.
Katibu Mtendaji Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya,
akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wahasibu (hawapo pichani)
kutoka Wizara ya Madini nchini leo tarehe 12 Novemba, 2018
|
Naibu Waziri wa Madani, Doto Biteko (kushoto) mara baada
ya kusaini kitabu cha wangeni katika Ofisi ya Mratibu wa Chuo cha Mazimbu
Campus Solomn Maalangu Dkt. Ibrahimu Mjema mkoani Morogoro.
|
Naibu Waziri wa Madani, Doto Biteko (wa pili kulia) katika
picha ya pamoja na Uongozi kutoka Tume ya Madini na Chuo cha Mazimbu Campus
Solomn Maalangu.
|
Wahasimu kutoka Wizara ya Madini nchini wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).
|
No comments:
Post a Comment