Ø Biteko asema wachimbaji sasa kuchimba kwa uhakika
Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Taasisi ya
Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) imetakiwa kuandaa ramani zinazoonyesha madini mbalimbali katika
ngazi ya Mikoa na Wilaya ili kuwapa nafuu watanzania wanaofanya shughuli za
uchimbaji wa madini nchini.
Kauli hiyo
imetolewa na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko baada ya kupokea taarifa ya Utafiti wa
Jiokemia katika skeli kubwa na skeli ndogo (Geochemical
Mapping for High and Low Density) uliofanyika nchi nzima kwa ushirikiano
kati ya GST na Taasisi ya Jiolojia ya China.
Naibu Waziri
Doto pia, ameitaka taasisi hiyo kuelekeza nguvu katika kuisaidia serikali
katika kupata matokeo chanya katika shughuli za madini huku ikiongeza thamani ya
kazi kutokana na utafiti huo na kuongeza kuwa, GST inaweza kutumia utafiti huo
mkubwa kuandaa ramani za madini katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
Akizungumzia manufaa ya tafiti huo kwa
Tanzania, amesema baada ya muda si mrefu watanzania wanaofanya shughuli za
uchimbaji watahamia katika uchimbaji wa uhakika na siyo wa kubahatisha kwa kuwa
utafiti huo unaonesha mahali sahihi ambapo shughuli hizo zinaweza kufanywa.
Amesema mbali
na shughuli za madini, utafiti huo pia unaweza kutumika katika sekta za kilimo,
maji na ujenzi wa barabara kwa kuwa unawezesha kutambua aina ya udongo unaofaa
kwa shughuli hizo.
Kutokana na
umuhimu wa utafiti na kazi iliyofanywa na taasisi hizo mbili, Naibu Waziri
Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuitumia taasisi ya GST katika shughuli za
kitaalam ikiwemo kupata taarifa za utafiti zinazohusu sekta ya madini na
kuongeza kuwa, sekta hiyo inao uwezo mkubwa wa kutekeleza wajibu wake.
Aidha, Naibu
Waziri Doto ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya China kutokana na
ushirikiano huo iliyoutoa katika kutekeleza utafiti huo ambao umegarimu kiasi cha Dola za
Kimarekani Milioni 4 na Laki Tano.
Kwa upande
wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jilojia ya China, Profesa Sun Xiaoming
amesema kuwa taarifa ya utafiti iliyowasilishwa ni ya nchi nzima ya Tanzania na
eneo la Mkoa wa Mbeya.
Amesema
utafiti huo umetoa matokeo ya jiokemia ya sampuli 71 nchini kote na sampuli 39
katika mkoa wa Mbeya na kuongeza kuwa utafiti huo utasaidia katika utekelezaji
maendeleo ya shughuli za madini, kilimo na mazingira nchini.
Awali,
akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mathias
Abisai amesema kusudio la ujumbe huo ilikuwa ni kuhakiki kazi iliyofanyika na
kuwasilisha ripoti. Ameongeza kuwa, ripoti hiyo itasaidia kwenye tafiti
nyingine za madini ikiwemo maji na mazingira.
Ameongeza
kuwa, mnamo Mwaka 2009 serikali ya China na Tanzania kwa kutumia taasisi zake
za Jiolojia zilisaini hati ya makubaliano (MoU) kwa lengo la kuanzisha mradi
huo wa miaka mitano ambapo kazi rasmi ya mradi ilianza mwaka 2013 na
kukamilishwa mwaka 2018.
Naye, Kaimu Mtendaji
Mkuu wa GST, Yokobeth Myumbilwa akileza malengo ya utafiti huo amesema kuwa ni
kupata taarifa za utafiti wa jiokemia kwa ajili ya kuandaa kanzidata ambayo
itaainisha uwepo wa taarifa zinazo ainisha uwepo wa aina mbalimbali za madini
,upangaji miji ,pamoja na taarifa hizo kuweza kutumika katika shughuli
mbalimbali katika sekta za kilimo na mazingira.
Naibu Waziri
wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Taasisi ya
Jilojia ya China, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na
Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Naibu Waziri
Doto Biteko akimkabidhi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia ya China, Profesa Sun Xiaoming Cheti cha kutambua
mchango wake na kukamilika kwa utafiti wa Jiokemia uliofanywa nchini.
No comments:
Post a Comment