Nuru Mwasampeta na
Samwel Mtuwa, Dodoma
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaasa Wanajiosayansi kutathmini
mchango wao katika maendeleo ya nchi, hususan katika maendeleo ya Tanzania ya Viwanda.
Waziri Mkuu Majaliwa
alitoa wito huo tarehe 27/09/2018 alipokuwa akifungua Warsha ya siku Nne ya Wataalamu
wa jiolojia iliyofanyika katika hoteli ya Dodoma jijini Dodoma yenye lengo la
kutathmini mchango wa wanajiosayansi katika maendeleo ya viwanda nchini.
Mkutano huo pia unalenga katika kuwaleta
pamoja wataalamu hao ili kujadili masuala mbalimbali ya sayansi ya dunia na
umuhimu wake kwa jamii.
Akizungumzia umuhimu
wa tasnia hiyo, Majaliwa alisema jiolojia ni sayansi inayogusa kila nyanja ya
maisha ya binadamu ikiwemo kilimo kitokanacho na udongo utokanao na miamba,
maji yapatikanayo ardhini, metali mbalimbali zipatikanazo ardhini kwa ajili ya
matumizi katika viwanda ikiwa ni pamoja na vyanzo vya nishati vinavyohusiana
moja kwa moja na jiolojia kama vile joto ardhi, makaa yam awe, mafuta na gesi
na madini kama vile urani.
Kutokana na umuhimu
huo mkubwa wa jiolojia Majaliwa amewataka watanzania kuendelea kutafuta
utaalamu huo ili waweze kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
“ Nchi yetu
imebarikiwa kuwa na rasilimali za asili nyingi kama vile madini, vito, mafuta
gesi asilia, makaa ya mawe . Tanzania ni moja ya nchi chache duniani
zilizobarikiwa kuwa na rasilimali hizi kwa wingi hivyo kupelekea kila majadiliano
ya mali asili duniani Tanzania kutajwa pia,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa,
kutokana na baraka ambazo nchi imejaliwa na Mwenyezi Mungu, nchi inanufaika
kutoka na michango mikubwa miwili ya jiosayansi ya kwanza ikiwa ni mchango wake
katika sekta ya viwanda, ambapo ili kuweza kufikia Tanzania ya Viwanda tunahitaji
malighafi zizalishwe kwa wingi ili zitumike katika viwanda vinavyoanzishwa
nchini.
Akizitaja malighafi
hizo, Majaliwa alisema ni kama vile
madini ya kinywe (graphite), jasi,
chokaa, kaolini madini ambayo yanahitajika kwa wingikatika kuchochea uzalishaji
wa bidhaa za viwandani.
Aidha, Majaliwa aliwataka
wanajiolojia kuhakikisha kuwa wanaonesha
ni wapi madini hayo yanapatikana ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji
kuweza kuyapata na kuyatumia katika viwanda vyao. “Mnatakiwa mtuambie yako wapi
na yana kiwango gani ili wazalishaji wa bidhaa za viwandani waweze kupata
malighafi hizi kwa urahisi ili kuongeza tija katika viwanda vyetu hapa nchini.”
Majaliwa alisisitiza.
Akizungumzia mchango
wa pili mkubwa wa jiosayansi, Majaliwa alisema ni katika upatikanaji wa maji ya
kutosha nchini. Alieleza kuwa ili kuwa na viwanda vinavyozalisha kwa ufasaha
nchini maji lazima yawepo kwani ni bidhaa muhimu katika kuchangia maendeleo ya
viwanda nchini.
Majaliwa
alitanabahisha kuwa jukumu la wanajiolojia nchini ni kuonesha ni wapi maji
yanapatikana ardhini kutokana na ukweli kuwa maji ya ardhini ni mara 5,000 ya
maji yanayopatikana katika uso wa dunia.
Kwa kuzingatia kuwa
maji yanapatikana popote ardhini aliwataka wataalamu hao kuandaa utaratibu
utakaowezesha kuwa na takwimu za uhakika kuhusu kiwango cha maji, mahali yalipo
na ujazo wake ili kuweza kuvutia uwekezaji wa viwanda kote nchini.
Aidha, alibainisha
mchango mwingine mkubwa wa jiosayansi kuwa ni katika masuala ya nishati ambapo
tutapata mchango kutokana na joto ardhi, rasilimali za gesi asilia ambapo gesi
asilia pia imeshaanza kutumika katika viwanda vyetu nchini. Alisema, tafiti
bado zinahitajika ili ufumbuzi uendelee na gesi yakutosha iweze kugunduliwa ili
kutosheleza mahitaji ya sasa na baadaye ili kufikia malengo hayo na kueleza
kuwa, jukumu hilo linawahusu wanajiolojia.
Akihitimisha hotuba
yake ya ufunguzi, Majaliwa aliwataka wanajiolojia hao kujihoji endapo wanajua
jukumu lao katika uboreshaji wa sekta ya madini, na endapo wao ni sehemu ya
mabadiliko hayo. “Ni matarajio yangu kuwa kwa kushirikiana na Serikali ambayo
tayari imejiimarisha Kisera na kimkakati ili kufikia azma ya viwanda,
itakayokuwa tayari kuonesha uzalendo wenu na kuhakikisha mchango wenu katika
hili unaonekana,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake,
Waziri wa Madini Angelleh Kairuki alikiri kwamba wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano kwa
wanajiolojia ikiwa ni pamoja na kupokea ushauri wa namna bora ya kuendesha na
kuendeleza shughuli za madini nchini.
Aidha, Kairuki
alibainisha kuwa wizara inakusudia na itakuwa mstari wa mbele katika kuanzisha chombo maalumu cha usajili
wa Wahandisi ili kuondoa malalamiko ya
watu yanayotokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kwa kujifanya ni wataalamu
wa miamba na ukweli ikiwa sivyo.
Wizara ya madini
kupitia taasisi zake itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanapokea
mapendekezo yote yanayotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusiana na namna bora
ya uendeshaji sekta ya madini hapa nchini na kuyafanyia kazi.
Kutokana na fursa
kubwa inayopatikana katika sekta ya madini, Kairuki aliwaasa
wanajiosayansi kujikita kwenye uwekezaji unaoendana na taaluma yao kutokana na
uwepo mkubwa wa rasilimali madini nchini ambayo bado hazijaendelezwa na hivyo
kuongeza ufanisi na uwezo wa kiuchumi kwa wanajumuiya hiyo.
Zaidi ya hapo, Waziri
Kairuki, alieleza kuwa wizara yake ipo katika mchakato wa kuiwezesha GST kuwa
na uwezo wa kukusnya taarifa za kina ambazo zitabaini akiba ya mashapo ya
madini mbalimbali yaliyopo nchini.
Uwepo wa taarifa hizo
utasaidia kuwavuta na kuwarahisishia wawekezaji pindi wanapotafuta maeneo ya
utafiti ili wapate leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa na takwimu za
uhakika.
Alibainisha kuwa kasi
hiyo itakwenda sambamba na kupitia upya Sera ya madini ya Mwaka 2009 ili iweze
kuendana na Marekebisho ya sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka
2017 pamoja na kanuni zake za mwaka 2018.
Warsha hii ya
wanajiosayansi yenye kauli mbiu isemayo “ Jukumu la wanajiosayansi katika
kuendeleza sekta ya viwanda” kwa mwaka huu, hufanyika kila mwaka mara moja.
No comments:
Post a Comment