Na Asteria
Muhozya, Dodoma
Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo amesema wadau wa Sekta ya Madini Kimataifa hivi sasa
wanaelewa umuhimu wa Tanzania kufanya mabadiliko katika Sekta husika yakiwemo
ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017.
“Mhe. Balozi
nashukuru kwa nafasi hiyo isipokuwa nilitamani kupata nafasi zaidi ya kuelezea
uzoefu wetu na mabadiliko katika sekta ya madini,” amesisitiza Naibu Waziri.
Ameongeza
kuwa, wawekezaji wengi hawana tatizo na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka
2017 yaliyofanywa isipokuwa changamoto ipo katika kipengele cha chanzo cha
mtaji kutoka katika benki za ndani suala ambalo amesema wizara imelichukua na
inaifanyia kazi.
Pia, Naibu waziri
amemshukuru Balozi Charters kwa kumwezesha kukutana na wadau mbalimbali wa
sekta ya madini wakati akiwa nchini humo, kwani, wadau hao wameonesha nia ya kuisaidia
Tanzania katika masuala ya uongezaji thamani madini nchini na mafunzo kwa
wataalam wa sekta.
“Tulizungumza
masuala mengi na umuhimu wa sisi kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani
madini kufanyika hapa nchini. Tunasisitiza suala hili kwa kuwa hivi sasa
tumezuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi”, amesema Naibu Waziri
Nyongo.
Kwa upande
wake, Balozi Charter amesema nchi hiyo itaona namna bora ya kufanya ili kuweza
kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo kwa wataalam wa sekta husika lengo likiwa ni
kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia sekta hiyo vizuri.
“Tunayo bajeti
kidogo lakini tunaweza kufanya jambo kwa ajili ya wizara ya madini katika utoaji
wa mafunzo. Ikiwezekana hata kuwaleta wataalam wetu kuja kutoa utaalam huo hapa
nchini,” amesema Balozi.
Aidha, Balozi
huyo ameeleza kuhusu fursa za masomo ambazo zimekuwa zikitolewa nchini
Australia zikiwemo nafasi za mafunzo ya
muda mrefu na mfupi na hivyo kuwataka wataalam wa Tanzania kuomba nafasi hizo pindi zinapojitokeza.
Pia, balozi
huyo ametaka kujua majukumu ya Tume ya Madini mara baada ya tume hiyo
kuanzishwa ambapo Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye naye amehudhuria kikao hicho,
Profesa Idris Kikula amemweleza balozi huyo majukumu yanayosimamiwa na tume
hiyo ikiwemo mikakati ya tume katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta
husika.
Akizungumzia
mabadiliko katika sekta ya madini pamoja na masuala ya uwajibikaji kwa kampuni
za madini kwa jamii, balozi Charter amesema suala hilo ni la msingi kwani hata
katika nchi hiyo masuala hayo yalipewa kipaumbele na kushauri iwapo wizara
inaweza kukutana na wadau kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu masuala
hayo.
Mbali na
mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika mkutano masuala ya madini kwa nchi za
Afrika, kikao hicho pia kimejadili masuala ya leseni za madini, Uwajibikaji wa
kampuni za madini katika jamii zinazozunguka migodi na kuhusu kampuni za madini kutumia kampuni za wazawa
kutoa huduma katika migodi.
Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo akimsikiliza Balozi wa Australia nchini Alison
Charters alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma ambapo wamejadiliana
masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Madini. Wengine ni Mwenyekiti kutoka Tume ya
Madini Prof. Idris Kikula na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini
na Ubalozi huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula
akimweleza jambo Balozi wa Australia Nchini Alison Charters alipomtembelea
Naibu Waziri Nyongo (hayupo pichani) ofisini kwake jijini Dodoma.
Naibu Waziri akifuatilia kikao baina yake na
Balozi wa Australia Nchini, Aliston Charters (hayupo pichani).
No comments:
Post a Comment