- Kampuni nyingi zazidi kujitokeza kwenye uwekezaji wa madini
Na Greyson Mwase, Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Mei hadi
Septemba mwaka huu, Tume ya Madini, imetoa leseni 7879 ambazo maombi yake
yaliidhinishwa kupitia kikao cha Tume kilichofanyika tarehe 25 Septemba, 2018
kilicholenga kujadili taarifa za Kamati
za Tume na utendaji kazi katika kipindi cha mwezi Mei hadi Septemba, 2018.
Profesa Kikula
ameyasema hayo leo tarehe 04 Oktoba, 2018 kupitia mkutano wa waandishi wa habari
uliofanyika katika Ofisi za Tume ya
Madini zilizopo jijini Dodoma.
Akielezea
kuhusu maombi ya leseni za madini 7879
yaliyoidhinishwa katika kikao cha Tume, Profesa Kikula alieleza kuwa ni pamoja na Leseni za
Utafutaji wa Madini (Prospecting License
- (PL) 263; Leseni Kubwa (Special Mining License – (SML) 03;(ziliidhinishwa ili kupelekwa kwenye mamlaka husika ambayo ni Baraza la
Mawaziri) Leseni za Uchimbaji wa Kati (Mining
License - (ML) 14 pamoja na
leseni 1 ya Sihia (Transfer) ya uchimbaji wa Kati.
Aliendelea kufafanua kuwa, maombi leseni za uchimbaji wa kati 14 yaliyopitishwa kuwa ni
pamoja na kampuni za Dangote Industries
Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chokaa katika eneo la Mtwara; Nazareth Mining Investment Co Limited kwa
ajili ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite)
katika eneo la Ruangwa mkoani Lindi na kampuni ya Sunshine Mining (T) Limited
kwa ajili ya uchimbaji wa madini dhahabu katika eneo la Chunya mkoani Mbeya.
Aliendelea kutaja kampuni nyingine kuwa ni pamoja na Said Seif Abdallah
kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya ujenzi katika eneo la Masasi mkoani Mtwara;
Off Route Technologies (T) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe
katika eneo la Ileje mkoani Mbeya; leseni yenye ubia kati ya Shabani Daud
Ibrahim, Andrew Bollen, Dunstan M. Mongi na Vedastus Mtesigwa kwa ajili ya
uchimbaji wa madini ya dhahabu katika mkoa wa Geita.
Maombi mengine yaliyopitishwa ni pamoja na leseni yenye ubia kati
ya Jumbo Limited, na Ally Mbarak Mohamed
kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) katika eneo la Ruangwa
mkoani Lindi, Jacana Resources (Tanzania) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa
mchanga bahari (mineral sand) katika
eneo la Temeke lililopo jijini Dar es Salaam na P. B. Mining Company kwa ajili
ya uchimbaji wa madini ya fedha,
dhahabu, shaba, zinki na galena katika eneo la Chunya lililopo mkoani Mbeya.
Profesa Kikula alisisitiza kuwa, kikao hicho pia kilipitisha ombi la
kubadili umiliki kutoka kwa Mbarouk Saleh Mbarouk kwenda katika kampuni ya M.
B. Mining (T) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya ujenzi katika eneo la
Morogoro.
Profesa Kikula aliendelea kutaja maombi ya leseni
nyingine zilizopitishwa katika kikao hicho kuwa ni pamoja na Leseni za
Uchimbaji Mdogo (Primary Mining License –
(PML) 6313; Leseni za Uchenjuaji
wa Madini (Processing License) 08 na leseni za Biashara ya Madini
ambapo leseni kubwa (Dealers License)
ni 557;
na leseni Ndogo (Broker’s License) 720.
Katika hatua nyingine Profesa Kikula alisema kuwa,
Mipango ya Ushirikishwaji wa Utoaji wa Huduma na Bidhaa kwa Wazawa katika
Miradi ya Madini (local content plan)
19 ilipitishwa kati ya mipango 26 iliyowasilishwa kutoka katika
kampuni mbalimbali za utafutaji na uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini.
Alielekeza waombaji leseni za madini kuwasilisha
mipango yao kwa wakati ili iweze kupitiwa na kamati husika na kuwezesha leseni
kutolewa mapema.
Pia aliwataka waombaji wote wa leseni za madini
kufuatilia leseni zao kwenye Ofisi za Madini zilizopo mikoani walikoombea
leseni zao na kusisitiza kuwa orodha ya leseni zilizoidhinishwa inapatikana
katika tovuti ya Tume.
Wakati huohuo Profesa Kikula alisema kuwa Tume ya
Madini imejipanga katika kuhakikisha kila mtanzania ananufaika ipasavyo na
rasilimali za madini nchini
Aliongeza kuwa, Tume imeweka mikakati ya
kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwatengea maeneo kwa ajili ya
uchimbaji madini na kuwataka kuunda vikundi na kusajiliwa kupitia viongozi wao
hivyo kuwezesha upatikanaji wa leseni za madini na kufanya shughuli zao pasipo
kikwazo chochote.
“Sisi kama Tume ya Madini tunatambua mchango
mkubwa wa wachimbaji wadogo wa madini na ndio maana tumekuwa tukifanya ziara
katika maeneo ya wachimbaji wadogo na kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja
na migogoro; tunataka wafanye kazi katika mazingira salama kabisa,” alisema
Profesa Kikula.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa
Shukrani Manya akielezea mchango wa Sheria Mpya ya Madini alisema kuwa tangu
kuanza kwa utekelezaji wa sheria mpya iliyoweka ongezeko la kutoka asilimia nne
hadi sita za mrabaha na tozo la asilimia moja la kodi ya ukaguzi wa
madini, makusanyo yameongezeka kutoka
shilingi bilioni 194 hadi shilingi
bilioni 301 kwa mwaka likiwa ni ongezeko la asilimia 55.
Pia, Mkurugenzi wa Leseni na TEHAMA kutoka Tume ya
Madini, Torece Ngole akielezea mikakati ya Tume katika kukabiliana na
changamoto ya migogoro kwenye uchimbaji wa madini inayosababishwa na wachimbaji
wadogo kwa kuvamia maeneo yenye leseni kubwa, alisema kuwa Tume imeshaanza
kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mpaka sasa
imeshatenga maeneo 74
Alisisitiza kuwa Tume imekuwa ikiwaelimisha
wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuunda
vikundi ili waweze kupatiwa maeneo na leseni za uchimbaji madini.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula (katikati) akitoa ufafanuzi alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mtendaji wa
Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Mkurugenzi wa Leseni
na TEHAMA wa Tume ya Madini, Torece Ngole.
|
No comments:
Post a Comment