Na Greyson Mwase,
Dodoma
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amewataka maafisa madini nchini kuwasilisha kwake
haraka maana halisi ya mawe yanayochimbwa na kukatwa kama ni madini ghafi au ni
mali ghafi kabla ya kutoa maamuzi juu ya usafirishwaji wake nje
ya nchi.
Aliyasema hayo jana
tarehe 06 Oktoba, 2018 mara baada ya kukamilisha ziara yake katika Mgodi wa
Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika eneo la Itiso mkoani Dodoma
ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Chamwino yenye
lengo la kukagua shughuli za uchimbaji
wa madini, kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji wa madini pamoja na wananchi wanaozunguka migodi.
Katika ziara yake
Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya
Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la
Chinolwa, Joel Makanyaga, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Joshua
Nduche, vyombo vya ulinzi na usalama vya
Wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Alifafanua kuwa
Sheria Mpya ya Madini ilitoa zuio la usafirishwaji wa madini ghafi nje ya nchi
ili kuzuia mianya ya utoroshwaji wa madini nje ya nchi.
“Kabla ya Sheria hii
mpya ya Madini, kulikuwa na utoroshwaji mkubwa wa madini nje ya nchi hali
ambayo iliikosesha Serikali mapato yake,
lakini mara baada ya utekelezaji wa Sheria Mpya ya Madini tumeshuhudia ongezeko
kubwa la mapato kutokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini,”
alisema Nyongo.
Naibu Waziri Nyongo
aliendelea kusema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mbali na
wachimbaji wa madini hususan wachimbaji
wadogo kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri, Serikali inataka kupata
mapato stahiki kwa ajili ya uboreshaji wa sekta nyingine muhimu.
Alisema mara baada ya
kupokea changamoto ya kuzuiwa kwa usafirishwaji wa mawe yaliyochimbwa na
kukatwa na Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga, aliridhishwa na juhudi
zinazofanywa na mgodi huo na kusema kama Serikali inaangalia namna ya kumsaidia
mmiliki wa mgodi huo lakini baada ya kujiridhisha kama ni malighafi badala ya
madinighafi.
“Lazima tuhakikishe
Sheria inasimamiwa ipasavyo, iwapo itabainika kuwa mawe yanayochimbwa na
kukatwa ni malighafi basi tutatoa uamuzi wa kuyaruhusu kusafirishwa nje ya nchi
na Serikali kupata mapato yake,” alisisitiza Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine
akizungumza katika nyakati tofauti katika ziara hiyo, Nyongo aliwataka
wachimbaji wadogo nchini wasio rasmi kuunda vikundi na kuomba leseni za
uchimbaji madini ili waweze kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni za madini.
Aliendelea kusema
kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imetenga maeneo maalum yaliyofanyiwa
utafiti kwa ajili ya kugawiwa kwa wachimbaji wadogo.
Aidha, aliwataka wamiliki
wote wa leseni kuendeleza maeneo yao kama Sheria ya Madini inavyowataka na kusisitiza watakaoshindwa kuendeleza
maeneo yao leseni zao zitafutwa na maeneo yao kugawanywa kwa ajili ya
wachimbaji wadogo.
Naye Mbunge wa
Chilonwa kupitia Chama cha Mapinduzi, Joel Makanyaga akizungumza katika ziara
hiyo alimshukuru Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea machimbo hayo na kufafanua
kuwa iwapo wachimbaji hao watawezeshwa na Serikali bidhaa za ujenzi
zinazotokana na mawe zitaongezeka na kusaidia hususan katika ujenzi wa jiji
jipya la Dodoma.
Alisema kuwa mahitaji
ya vifaa vya ujenzi ni makubwa katika ujenzi wa jiji la Dodoma na kuendelea
kusema kuwa mapato yatokanayo na uchimbaji na ukataji wa mawe yanatarajiwa
kuongezeka hivi karibuni.
Awali akiwasilisha
changamoto za Mgodi wa Mawe Mkurugenzi wa Mgodi huo, Sisti Mganga alisema kuwa
uwepo wa Sheria ya Madini inayokataza
usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi umeathiri utendaji kazi wa kampuni
kwani wamerundika mawe mengi wakisubiri maelekezo kutoka Serikalini.
Alisisitiza kuwa mawe
yanayochimbwa kukatwa na kung’arishwa katika
machimbo hayo yanajulikana kama malighafi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
na barabara na kuiomba Serikali kuruhusu usafirishwaji wa mawe hayo ili waweze
kuendesha shughuli za uchimbaji na ukataji wa mawe hayo na kulipa mrabaha na
kodi mbalimbali Serikalini.
Aidha Mganga aliiomba
Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi
wa viwanda kwa ajili ya kuchenjua na kuongeza thamani madini ili kuzalisha
ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele) akiendelea na ziara katika machimbo
ya mawe yaliyopo katika eneo Itiso Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akiangalia moja ya mawe yanayochongwa
na Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti
Mganga katika eneo la Itiso lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma katika
ziara yake ya siku moja katika machimbo
yaliyopo katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero
mbalimbali kwenye shughuli za uchimbaji madini tarehe 06 Oktoba, 2018.
No comments:
Post a Comment