Asteria Muhozya na Rhoda James, Geita
Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeanza kufanya mazungumzo na nchi ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili iweze kujenga Kiwanda cha Kuchenjua
madini ya Colbat nchini.
Hayo
yalibainishwa Oktoba 19, mkoani Geita na
Waziri wa Madini wa Tanzania Angellah Kairuki wakati wa kuhitimisha ziara ya
siku Nne ya Waziri wa Madini wa Kongo
(DRC), Martin Kabwelulu aliyoifanya nchini kwa mwaliko wa Waziri Kairuki.
Kairuki
alisema kuwa, nchi ya Kongo ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya Colbat duniani
ambapo asilimia 70 ya madini hayo duniani yanazalishwa nchini humo.
Aliongeza
kuwa, kwa sasa nchi hiyo inayo changamoto ya kusafirisha madini hayo yakiwa
ghafi ikiwemo ukosefu wa umeme wa kutosheleza kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
hivyo.
“Tumekubaliana
kuendelea na mazungumzo na Kongo ili
shughuli za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini hayo ufanyike nchini kwa kuwa tumeshaanza kuwekeza kwenye
Vinu/viwanda vya Kuchenjua na kuyeyusha
madini mbalimbali. Hivyo, tunataka wayasafirishe makinikia ya Colbat hapa na
tuyachenjue hapa,” alisisitiza Kairuki.
Akizungumzia
matumizi ya madini hayo, Kairuki alisema kuwa, madini ya Colbat yanatumika kutengeneza
betri na vihifadhi nishati (capacitor)
ambazo zinahitajika sana hususan, kwenye magari yanayotumia umeme.
Mbali
na makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho, pia Waziri Kairuki alisema kuwa nchi
hizo zimekubaliana masuala kadhaa ikiwemo kuendelea kubadilishana uzoefu wa
usimamizi wa sekta ya Madini ili kuweza kunufaisha wananchi hasa wale
wanaozunguka maeneo ya migodi.
“Nchi
ya Kongo DRC imefurahishwa na hatua za Mkoa wa Geita kwenye usimamizi wa mapato
yatokanayo na madini pia mchango wa migodi kwa maendeleo ya wananchi
wanaozunguka mgodi,”alisema Kairuki.
Vilevile,
alisema kuwa nchi hizo zimekubaliana kuboresha mahusianao ya kimkakati ambapo
Kongo imeahidi kuiunga Mkono Tanzania katika masuala ya Mashtaka dhidi ya
makampuni za uwekezaji.
Pia,
alisema Kongo imeahidi kukitumia Chuo Cha Madini Dodoma (MRI) kupata mafunzo
mbalimbali yanayohusu sekta ya madini yanayotolewa kituoni hapo;
“Kongo
imepanga kuja kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa leseni za madini (cadaster) ambao umebuniwa na kusanifiwa
na watanzania,” alisema Kairuki.
Kairuki
aliongeza kuwa, nchi hizo zimekubaliana kuendelea kuboresha mifumo ya udhibiti
utoroshaji wa madini yanayotoka Kongo na Tanzania kwa manufaa ya nchi zote
mbili.
Aidha,
Waziri Kairuki alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Kongo wenye nia
ya kuwekeza nchini kwenye migodi, viwanda vya uchenjuaji, uongezaji thamani
madini (ukataji, unga’rishaji).
“Lakini
pia tumewakaribisha kutumia bandari yetu kupitisha madini yao pamoja na
kukubaliana kuwa na Mining Forum kati
ya nchi hizi mbili tu ukiachia Forum nyingine
ambazo tumelenga kuziandaa na kushirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali,”
alisema Kairuki.
Aidha, alisema nchi hiyo imeahidi kurudi nchini katika kipindi kifupi kijacho kwa ajili ya
kujifunza zaidi kuhusu namna Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) inavyofanya kazi zake za utafiti
na maabara.
Kwa
upande wake, Waziri wa DRC, Martin Kabwelulu alisema atawatuma Wataalam wake
kurudi nchini kwa ajili ya kujifunza mfumo mpya wa utoaji wa leseni za madini (cadaster) wa Tanzania na kuongeza ni
mfumo mzuri ambao utaliwezesha taifa hilo kusimamia vema rasilimali madini na
kuhakikisha kwamba zinawanuifaisha wananchi wake.
Pia, alisema kuwa nchi hiyo inao ukosefu wa umeme
wa kutosha jambo ambalo linafanya nchi hiyo kusafirisha madini hayo nje yakiwa
ghafi ikiwemo madini ya Colbat na dhahabu na kuongeza kuwa, Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila katika ujumbe wake
amemweleza kuwa, anataka madini yote ya Kongo yasafirishwe kupitia Tanzania.
“Tunataka tusafirishe
madini yetu kupitia bandari ya Tanzania. Lakini pia nimeona njia ya kupitishia
madini yetu kupitia reli ya Kati ya Kigoma –Dar es Salaam ni fupi sana,” alisema
Kabwelulu.
Akizungumzia
mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanywa nchini humo hivi karibuni, alisema
nchi hiyo iliamua kubadili sheria yake kutokana na kutokunufaika kabisa na
rasilimali hiyo hususan kwa wananchi wanaozungukwa na rasilimali hizo na kuongeza kuwa, sheria ya
sasa inapigania zaidi maslahi ya nchi na wananchi wake.
“Nafurahi
nimepokelewa vizuri sana Tanzania, nimejifunza mengi kweli hii ni nchi rafiki.
Sisi tunao uzoefu wa miaka mingi kwenye sekta hii lakini bado hatujanufaika
kabisa,” alisema Kabwelulu.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Mhandisi Robert Luhumbi alisema kuwa, amemwomba Waziri wa Madini wa
Kongo kujenga kiwanda cha Colbat nchini kwa kuwa nchi hiyo iko jirani sana na
mkoa huo na kwamba mkoa huo umejipanga kwa mazingira ya uwekezaji mkubwa.
Akiwa nchini, Waziri
Kabwelulu alipata fursa ya kukutana na Menejimenti ya Wizara ya Madini na
Taasisi zake ambapo pande zote zilibadilishana uzoefu wa namna zinavyosimamia
sekta ya madini, ikiwemo masuala ya uchimbaji mdogo wa madini.
Aidha, Waziri
Kabwelulu na mwenyeji wake Waziri Kairuki walitembelea Mgodi wa Mfano wa Lwamgasa
ambao umejengwa mahsusi kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali
Madini (SMMRP) unaosimamiwa na wizara. Lengo la mgodi huo ni kutoa elimu kwa
wachimbaji wadogo kuhusu uchimbaji sahihi
na uchenjuaji bora wa madini dhahabu. Pia, walitembelea migodi ya
Wachimbaji wa Kati inayomilikiwa na watanzania ya Buswola Mining Ltd na Nsangano Gold Mine mkoani Geita
kujifunza walikotokea katika uchimbaji mdogo hadi kuwa wa Kati na pia
walitembelea mgodi wa Almasi wa Mwadui (WDL) mkoani Shinyanga.
Ziara ya Waziri
Kabwelulu nchini ililenga katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika
masuala ya uendelezaji na usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwemo kuimarisha zaidi
ushirikiano uliopo baina ya hizo mbili, kuangalia fursa za ushirikiano
wa kibiashara na kiuwekezaji kupitia rasilimali madini madini, kubadilishana
uzoefu kuhusu Mabadiliko ya Sheria
za Madini yaliyofanywa na nchi
hizi mbili hivi karibuni pamoja na kudumisha undugu na urafiki baina ya nchi
hizo mbili.
Waziri wa Madini
wa Angellah Kairuki na Mgeni wake Waziri
wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Martin Kabwelulu (Wa tatu
kushoto) wakiangalia madini ya Dhahabu yanayozalishwa na kuchenjuliwa katika
Mgodi wa Nsangano Gold Mine mkoani Geita walipoutembelea mgodi huo.
Waziri wa
Madini Angellah Kairuki na Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo
(DRC) Martin Kabwelulu wakiangalia Kitabu kinachotunza uzalishaji wa madini ya
Almasi katika Mgodi wa Almas Mwadui (WDL) Kitabu hicho kina kumbukumbu za
uzalishaji wa tangu mwaka 1958. Anayeshuhudi ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack.
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki na mgeni wake Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC)
Martin Kabwelulu (wa pili kushoto) wakimsikiliza Mtaalam Mwelezi Martin Sezinga Akiwaonesha mashine mbalimbali
zinazotumiwa katika hatua mbalimbali za uzalishaji na uchenjuaji wa madini ya
dhahabu katika mgodi wa mfano wa Lwamgasa.
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki (kushoto) na Waziri wa
Madini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Martin Kabwelulu
wakiteta jambo baada ya kutembelea mgodi wa Busolwa Mining Ltd unaomilikiwa na
Mtanzania, mkoani Geita.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki na mgeni wake Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC) Martin Kabwelulu pamoja na ujumbe walioambatana nao wa Mkoa wa
Shinyanga wakiangalia namna shughuli mbalimbali za uzalishaji wa madini ya Almasi katika Mgodi wa Almasi Mwadui (WDL)
zinavyofanyika.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki na Waziri wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
Martin Kabwelulu, wakimsikiliza Mtaalam kutoka Mgodi wa Almasi wa Mwadui (WDL)
wakati akiwaeleza namna shughuli za uchimbaji wa madini hayo zinavyofanyika.
No comments:
Post a Comment