Na Greyson Mwase,
Songwe
Serikali kupitia
Wizara ya Madini imepiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kwa ajili ya
kuchenjulia madini ya dhahabu kutoka mkoa mmoja hadi mwingine na kusisitiza
kuwa haitasita kumchukulia hatua za kisheria mchimbaji wa madini atakayekiuka
agizo hilo.
Agizo hilo limetolewa
leo tarehe 18 Oktoba, 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika
mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Saza kilichopo
wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili
katika mkoa huo yenye lengo la kukagua
shughuli za uchimbaji wa madini,
kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake
Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe,
Samwel Jeremeah, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai
Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman
Kwariko, Maafisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege
Bilagi na Mhandisi Godfrey Nyanda, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya
pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza na
wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa lengo la Serikali kupitia
Wizara ya Madini kupiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kutoka katika mkoa
mmoja kwenda mwingine tangu Juni mosi mwaka huu lilikuwa ni kuhakikisha kila
mkoa unapata mapato stahiki kupitia ujenzi wa mitambo ya kuchenjua madini kwa
kutumia kaboni.
“Kama Serikali
tunataka kuhakikisha kila mkoa unajenga mitambo ya kuchenjua madini badala ya
kwenda kuchenjulia katika mikoa ya jirani kwa kutumia kaboni na kukosa mapato
stahiki,” alifafanua Nyongo.
Alisisitiza kuwa,
Serikali haitasita kutaifisha kaboni itakayokamatwa ikisafirishwa kutoka mkoa
mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kuwachukulia wahusika hatua za
kisheria.
Akielezea mikakati ya
Wizara ya Madini katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini, Nyongo alisema
kuwa Wizara imeshaanza kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini na
kuwataka kuunda vikundi na kuomba leseni ili waweze kufanya shughuli zao za
uchimbaji wa madini kwa kufuata sheria na kanuni za madini.
Aliongeza kuwa,
Wizara ya Madini imeanza kujenga vituo vya umahiri kwa ajili ya kutoa mafunzo
kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu namna bora ya kubaini, kuchimba na
kuchenjua madini na kueleza zaidi kuwa moja ya kituo kinachotarajiwa kujengwa
ndani ya kipindi cha miezi sita kitakuwa katika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.
Aidha, Nyongo
aliwataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanalipa mrabaha na kodi mbalimbali
zinazotakiwa Serikalini na kuwataka maafisa madini nchini kuhakikisha
wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato hayo.
Pia, aliwataka
wachimbaji wadogo wa madini kuepuka uchenjuaji wa madini kwa kutumia zebaki
kwani ina madhara makubwa katika uharibifu wa mazingira na binadamu.
Akielezea namna bora
ya usimamizi wa viwanda vitakavyojengwa kwa ajili ya kuchenjua madini ya
dhahabu kwa kutumia kaboni, Nyongo alisema mbali na kuhakikisha wamiliki
wanakuwa na leseni za uchenjuaji wa madini, wataalam wa mazingira kutoka Wizara
ya Madini watapita na kukagua ili kuhakikisha kuwa viwanda vinajengwa katika
mazingira mazuri ambayo hayatakuwa na athari katika makazi ya wananchi.
Awali wakizungumza
katika mkutano huo kwa nyakati tofauti wachimbaji wadogo waliwasilisha kero
mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maeneo kwa ajili ya kuendesha shughuli
za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, ushuru na tozo nyingi, pamoja na
kutoshirikishwa katika mikataba baina yao na wawekezaji wakubwa wa madini.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini
katika kijiji cha Saza kilichopo wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu
ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa
madini tarehe 18 Oktoba, 2018.
Msimamizi wa
uchimbaji madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Sunshine uliopo katika kijiji cha
Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Evarist Lukuba (kushoto) akifafanua
jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto mbele) mara
alipofanya ziara katika mgodi huo.
Meneja Mkuu wa Mgodi
wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe
mkoani Songwe, Honest Mrema (wa pili kulia mbele) akielezea majukumu ya mgodi
huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na msafara wake mara
alipofanya ziara katika mgodi huo.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara
katika Mgodi wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani
Songwe mkoani Songwe.
Kutoka kushoto, Afisa
Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, na Afisa Madini kutoka Ofisi
hiyo, Godfrey Nyanda, wakinukuu
maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(hayupo pichani) kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa
Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi, (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili
katika Wilaya hiyo kabla ya kuanza ziara yake rasmi.
No comments:
Post a Comment