Na Greyson Mwase,
Songwe
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wa madini wanaoendesha shughuli zao za uchimbaji wa
madini ya chokaa na ujenzi katika kijiji
cha Nanyala kilichopo katika Wilaya ya Mbozi iliyopo mkoani Songwe kuendelea na
shughuli zao wakati wakisubiri suluhu
ya mgogoro baina yao na kiwanda cha
saruji cha Mbeya.
Naibu Waziri Nyongo
aliyasema hayo leo tarehe 17 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza katika mkutano
na wachimbaji wadogo uliofanyika katika
kata ya Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya
siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa
madini.
Katika ziara yake
Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, John Palingo, Afisa Madini Mkazi
katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za
Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Afisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini
Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi, vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya
pamoja na waandishi wa habari.
Nyongo alifafanua
kuwa, awali maelekezo yalitolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya
kutaka viongozi kutoka katika mikoa ya Mbeya na Songwe kukaa pamoja na
kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa ardhi kati ya
wakazi wa Songwe na Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji nje ya
mahakama jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa sasa.
Alielekeza viongozi
kutoka katika mikoa husika kuhakikisha wanashughulikia mgogoro wa ardhi kati ya
mikoa miwili na kiwanda cha saruji cha Mbeya kwa wakati huku wananchi
wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini wakiendelea na shughuli zao
kama kawaida katika maeneo husika.
Aliendelea kusema kuwa,
jukumu kuu la Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ni kuhakikisha wanatoa
leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini na
kusisitiza kuwa leseni ya uchimbaji wa madini ni tofauti na hati ya ardhi kwa kuwa inahusisha madini
yaliyopo chini ya ardhi.
“Ningependa ieleweke
kuwa, leseni ya madini inampa mtu kibali cha kuchimba madini yaliyopo chini ya
ardhi ambayo ni tofauti na hati ya ardhi, hivyo wachimbaji wa madini wana haki
ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini wakati suala la mgogoro wa
ardhi likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika,” alisisitiza Nyongo.
Akielezea taratibu za
kuchimba madini mara baada ya kupata leseni, Naibu Waziri Nyongo alisema mara
baada ya mchimbaji kupata leseni ya uchimbaji wa madini anatakiwa kufika katika
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadaye kutambulishwa katika Ofisi ya Kijiji ili
kukutanishwa na wananchi na kufanya makubaliano ya ulipaji fidia kabla ya
kuanza shughuli rasmi za uchimbaji wa madini.
Alisisitiza kuwa, ni
lazima wawekezaji wote katika shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha kuwa
wanajitambulisha na kufanya makubaliano na wananchi kabla ya kuanza rasmi kwa
uchimbaji wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka maafisa madini katika mikoa ya Mbeya na
Songwe kuendelea na zoezi la kuainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa
madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa leseni ili uchimbaji wao uweze kuleta tija
kwenye uchumi wa nchi.
Aidha, aliongeza kuwa
katika maeneo ambayo ni ya hifadhi au vivutio vya utalii leseni zake zifutwe
ili kuhakikisha rasilimali za maliasili zinalindwa na kuongeza pato kwenye
uchumi wa taifa.
Wakati huohuo Nyongo
aliwataka wachimbaji wa madini kuhakikisha kuwa wanalipa kodi mbalimbali ili fedha hizo ziweze kutumika katika uboreshaji wa huduma nyingine za jamii kama
vile elimu, afya, miundombunu ya barabara.
Pia, Nyongo aliwataka
wachimbaji wa madini kuorodhesha kodi na tozo mbalimbali ambazo wanaona ni
nyingi na kuziwasilisha katika Wizara ya Madini, ili Wizara iangalie namna ya
kuzipunguza na wapate faida zaidi kwenye uchimbaji wa madini.
Awali wakizungumza
katika nyakati tofauti wachimbaji hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mgogoro wa ardhi baina yao na
kiwanda cha saruji cha Mbeya, uharibifu wa mazingira unaofanywa na
baadhi ya wachimbaji na ukosefu wa
maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kulia mbele) na Meneja wa Kiwanda cha chokaa cha Lime
Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani Songwe, Fredy
Msindo (kushoto mbele) pamoja na msafara
wakiendelea na ziara katika eneo la kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya
ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Songwe yenye lengo la kusikiliza na
kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 17 Oktoba, 2018.
Meneja wa Kiwanda cha
chokaa cha Lime Africa kilichopo katika Kata ya Nanyala Wilayani Mbozi Mkoani
Songwe, Fredy Msindo (katikati) akielezea shughuli zinazofanywa na kiwanda
hicho kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na msafara wake.
Kutoka kushoto Afisa
Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini kutoka Ofisi ya
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Afisa Madini anayesimamia
wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko wakinukuu maelekezo yaliyokuwa
yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika
mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kata ya Nanyala wilayani
Mbozi mkoani Songwe .
Sehemu ya wachimbaji
wa madini ya chokaa na ujenzi kutoka katika kata ya Nanyala wilayani Mbozi
mkoani Songwe, wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)
No comments:
Post a Comment