·
Atoa
miezi miwili kwa mwekezaji kulipa fidia wananchi
Na Greyson Mwase,
Bunda
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko ametatua mgogoro mkubwa wa siku nyingi uliokuwepo kati ya
wananchi wa kijiji cha Kunanga kilichopo ndani ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara
na kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Lake Victoria kwa kuitaka
kampuni kuhakikisha imelipa fidia kwa
wananchi wote ndani ya kipindi cha miezi
miwili.
Naibu Waziri Biteko
aliyasema hayo leo tarehe 21 Septemba, 2018 mara baada ya kufanya ziara kwenye machimbo
na kusikiliza kero za wachimbaji wadogo kupitia mkutano wa hadhara ikiwa ni
sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Mara na Geita yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini
pamoja kusikiliza na kutatua kero mbalimbali.
Ziara hiyo katika
machimbo hayo inatokana na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa katika mkoa wa Mara kwenye ziara
yake aliyoifanya kuanzia tarehe 05 hadi
07 Septemba mwaka huu ya kumtaka Naibu
Waziri wa Madini kuhakikisha ametatua mgogoro husika.
Katika ziara hiyo,
Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili, Rais wa
Chama cha Wachimbaji Madini Nchini, John Bina, Mwenyekiti wa Chama cha
Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara, Stephan Msseti, Mbunge wa Bunda Vijijini,
Boniphace Getere, Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya, Watendaji kutoka
Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari.
Alisema kuwa, baada
ya kusikiliza maelezo kutoka pande zote mbili alibaini kuwa wanachi walikuwa na
haki ya kulipwa fidia na kumtaka mwekezaji kuhakikisha kuwa anafuata sheria na
kanuni za madini kwa kuhakikisha amefanya tathmini na kuwalipa fidia ndani ya
kipindi cha miezi miwili.
Aliendelea kufafanua
kuwa, zipo taratibu zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji wote kwenye madini
ikiwa ni pamoja na kujitambulisha kwa Wakuu wa Wilaya, Vijiji na wananchi na
kufanya mazungumzo na kuweka makubaliano ya fidia pamoja na kulipa kabla ya
kuanza rasmi shughuli za uchimbaji madini.
“Haiwezekani kamwe
mwekezaji anapewa leseni na Ofisi ya Madini anakwenda moja kwa moja kwa
wananchi tena akiwa na walinzi na kuanza kuwafukuza bila hata kujitambulisha na
kufanya mazungumzo, hii inahatarisha usalama na uhusiano kati ya mwekezaji na
wananchi wa sehemu husika,” alisema Naibu Waziri Biteko.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Mkurugenzi wa kampuni ya uchimbaji wa
dhahabu ya Lake Victoria, Ahmed Magoma na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili kufanya
mkutano na wananchi ili kutafuta mustakabali wa fidia na kumpatia taarifa.
Aidha, alimtaka mwekezaji kuomba kikao na Serikali ya Kijiji
kabla ya siku ya Jumatano ya wiki ijayo ya tarehe 26 Septemba mwaka huu na
kuendelea kumtaka kuhakikisha anashirikiana na wananchi kwa karibu zaidi na
kudumisha mahusiano.
Pia Waziri Biteko
alimtaka mwekezaji kuhakikisha analipa deni la Dola za Kimarekani 46,080 Serikalini ndani ya kipindi cha siku 45 tangu
alipoandikiwa hati ya makosa kama mojawapo ya uvunjifu wa sheria ya madini
pamoja na kanuni zake.
Wakati huohuo, Naibu
Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya kuhakikisha
eneo lililobaki lenye ukubwa wa kilomita za mraba 5.12 lililotolewa na
mwekezaji linagawanywa na kupewa kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Katika hatua nyingine,
akiwa katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko alisikitishwa na kitendo cha
wachimbaji wadogo wa madini kutokulipa mrabaha serikalini hali inayoikosesha
Serikali mapato yake stahiki.
Alielekeza Mkuu wa Wilaya
ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili na Mwenyekiti wa kijiji cha Kunanga, Kisire
Marwa kukaa kwa pamoja na kuchunguza kiasi cha fedha zinazodaiwa kulipwa na
wachimbaji wadogo wa madini katika serikali ya kijiji na matumizi yake na kisha
kutoa taarifa kwa wananchi.
“Wachimbaji hawa
wanadai kuwa wanalipa fedha katika
serikali ya kijiji, kiasi halisi hakijulikani wala matumizi yake, fedha hizi
zinatakiwa ziwanufaishe kupitia uboreshaji wa huduma za jamii,” alisema Biteko.
Aliendelea kusema
kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haipo
tayari kuona mwekezaji au mchimbaji yeyote ananyanyasika na kufafanua kuwa kila
mwananchi ni sehemu ya rasilimali za madini.
Pia, aliwataka
wananchi kutii sheria ya madini pamoja na kanuni zake na kuongeza kuwa wananchi
wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye shughuli za
utafutaji na uchimbaji madini.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Lake
Victoria, Ahmed Magoma akizungumza mara baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa
Naibu Waziri Biteko, aliomba msamaha kwa wananchi wa kijiji cha Kunanga na
kueleza kuwa atatekeleza maelekezo yote ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano
kati yake na wananchi husika ili uchimbaji wa madini ufanyike kwa amani na kila
upande uweze kufaidika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili pamoja
na pongezi kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema kama serikali
watafuatilia kwa karibu mapato na matumizi
ya fedha zinazodaiwa kulipwa katika serikali ya kijiji cha Kunanga na
kuchukua hatua kwa waliohusika na ufujaji wa fedha hizo.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) pamoja na msafara wake wakielekea katika
machimbo ya dhahabu yaliyopo katika kijiji cha Kunanga kilichopo wilayani Bunda
mkoani Mara yanayomilikiwa na kampuni ya Lake Victoria
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Kunanga kilichopo katika wilaya ya Bunda mkoani Mara. (hawapo
pichani)
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kulia) akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wananchi
wa kijiji cha Kunanga kilichopo katika wilaya ya Bunda mkoani Mara
Mkuu Wilaya ya Bunda,
Mwl. Lidia Bupilipili akifafanua jambo kwenye mkutano wa hadhara
No comments:
Post a Comment