Na
Asteria Muhozya, Arusha
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amewataka Wafanyabiashara wa Madini nchini kuzaliwa upya kwa
kufuata Sheria, Kanuni na taratibu kwa
kufanya biashara halali ya madini ili kuziwezesha
pande zote yaani Serikali na
Wafanyabishara kunufaika na
rasilimali hiyo.
Waziri Kairuki
ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyabiashara wa madini wa jijini Arusha waliohudhuria mkutano huo ulioratibiwa na Chama Cha Wafanyabiashara wa
Madini Tanzania, (TAMIDA).
Kairuki alisema zama
zimebadilika na hivyo kuwatahadharisha
wale wote wanaofanya vitendo vilivyo kinyume na taratibu na kueleza kuwa, hawatasalimika na mkono wa sheria kwa kuwa
serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba rasilimali madini inawanufaisha
watanzania na taifa.
“Nimekuja hapa
tubatizane. Naomba tuzaliwe upya. Tushirikiane vizuri. Naahidi kuwa balozi wenu
mzuri. Nitatekeleza yale yenye manufaa kwetu sote. Lakini watakaokwenda kinyume,
serikali ina macho yanayoona sana na yenye lenzi za hatari,” alisisitiza
Kairuki.
Kairuki alisisitiza
kuwa, tayari anazo taarifa za kila mfanya biashara wa madini wa jijini Arusha
na kuwataka wote wanaokwenda kinyume kujitafakari upya na kuchukua hatua sahihi kwani anamfahamu kila mmoja.
Alisema, serikali inatambua
na kuthamini mchango wa biashara ya madini katika pato la taifa na katika
kuzalisha ajira na kuongeza kuwa, itaendelea kuweka mazingira mazuri ya
biashara ya madini na kuwataka wale wote waliokuwa wakitenda kinyume ikiwemo
kukwepa kodi kujisalimisha kwake ili kuepuka kuingia katika makosa ya uhujumu
uchumi.
“Kama unadhani
ulikuwa unakwepa kodi, unakwenda kinyume, njoo uniambie. Haitapendeza upate
kosa la uhujumu uchumi, kumbukeni kuwa kosa hilo halina dhamana,” alisisitiza
Waziri Kairuki.
Akizungumzia suala la
utoaji leseni za usafirishaji madini nje ya nchi, alisema serikali italifanyia
haraka suala hilo ili kuleta ufanisi katika biashara ya madini huku akisisitia
kuwa, watakaopatiwa leseni hizo ni wale tu watakaokidhi vigezo.
“ Lakini pia hatukatazi
wageni kuwekeza nchini. Isipokuwa tunataka waje kihalali,” alisisitiza Waziri
Kairuki.
Awali, akisoma risala
ya wafanyabiashara hao, Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel, alisema, TAMIDA
inaunga mkono suala la uongezaji thamani madini kufanyika nchini kwa kuwa
shughuli hizo zitasaidia kuongeza thamani
ya madini, fedha za kigeni kuhamisha teknolojia, kupanua wigo wa ajira na
kufungua viwanda vingi vya uongezaji thamani na hatimaye kuifanya Tanzania kuwa
kitovu cha madini barani Afrika.
Vilevile, alisema
kuwa, chama hicho kinaunga mkono
kutosafirisha madini ghafi ya Tanzanite nje ya nchi na kupendekeza kuwa madini ya tanzanite
yanayozidi gramu 1 yakatwe hapa nchini na kwa yale yaliyo nusu uzito yaongezwe umbile kisha yaruhusishwe
kusafirishwa yakiwa ghafi kwa kuwa bado hakuna ujuzi wa kukata madini katika kiwango hicho.
Akizungumzia ujenzi
wa ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite Mirerani, alisema kuwa, Tamida inaunga
mkono jitihada zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Magufuli na kueleza kuwa, ukuta huo umesaidia kulinda rasilimali na
udhibiti wa madini hayo.
![]() |
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki akipokea taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sam Mollel kwa niaba ya
wafanyabiashara hao.
|
![]() |
Sehemu ya
wafanyabishara wa madini wa jijini Arusha wakifuatilia mkutano baina yao na
Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).
|
![]() |
Sehemu ya
wafanyabishara wa madini wa jijini Arusha wakifuatilia mkutano baina yao na
Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).
|
No comments:
Post a Comment