Thursday, August 9, 2018

Serikali yamjia juu mwekezaji katika mgodi wa CANACO,ulipo Magambazi, kwa kukiuka Sheria ya Madini


Na Zuena Msuya, Tanga
Serikali imeiagiza Tume ya Madini Tanzania, kutoa hati ya makosa kwa Kampuni ya Canaco inayomiliki leseni ya Uchimbaji Madini wa Kati  iliyopo katika Kijiji cha Magambazi Wilayani Handeni Mkoani Tanga, na kuzuia mali na mitambo yote iliyopo eneo hilo kutokana kukiuka masharti ya leseni hiyo ya uchimbaji madini ya dhahabu na kwenda kinyume na Sheria ya Madini yam waka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na kanuni za mwaka 2018.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ambapo pamoja na mambo mengine pia aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi katika sakata la utoroshwaji wa Carbon zenye madini ambazo ziliibwa usiku kutoka eneo hilo na kupelekwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata dhahabu kinyume cha utaratibu.
Waziri Biteko alisema kuwa mwekezaji huyo awali alifika katika Wizara ya Madini na kuomba kibali cha kusafirisha carbon tani 2.23 kwenda mkoani Mwanza katika kiwanda cha JEMA AFRICA LTD  kwa ajili ya kuchenjuliwa lakini wakanyimwa kutokana na matatizo yao ya ndani  lakini baadae wakachukua kibali cha kughushi kutoka Dodoma kwa ajili ya kusafirishia carbon kupeleka Mwanza.
“Hawa watu walikuja ofisini ya madini Handeni  kuomba kibali cha  kusafirisha carbon tani 2.23 kwenda Mwanza kwa ajili ya kuchenjuliwa lakini walinyimwa kutokana na sababu zao za ndani zilikuwepo muombaji kutokuwa mmiliki wa leseni ya Canaco lakini cha kushangaza walitorosha carbon tani 2.23 usiku wa manane na kwenda kuchukua  kibali cha kughushi   kutoka  ofisi ya madini Dodoma kinachoonesha carbon tani 1.5 tu”alisema.
Aliongeza “Baada ya kuichakata carbon tani 1.5 Mwanza  kiasi kingine hakijulikani kilipo mpaka sasa haiwezekani jambo hili lichukue muda katika uchunguzi nakuagiza OCD kadri utakavyoona katika harakati zako za kiuchunguzi hawa watu wakamatwe na nawaomba TAKUKURU nao watusaidie katika kuchunguza wa jambo hili” alisema.
Mbali na hivyo pia aliumuelekeza Kamishna wa Tume ya Madini Dkt.Athanas Macheyeka kumpa mwekezaji huyo hati ya makosa (default notice) kwa ajili ya kurekebisha makosa waliyonayo kwenye leseni ya uchimbaji wa madini na kama watashindwa  kurekebisha makosa kwa muda uliotajwa na sheria, leseni yao ifutwe wapewe wawekezaji wengine walio makini.
“Sheria ya madini inamtaka mwenye leseni ya madini achimbe siyo atumie mabaki yaliyochimbwa na wachimbaji wengine ayachenjue……kamishna wa tume ya madini kati ya leo na kesho wape ‘default notice’ kwa ajili ya kurekebisha makosa yao na wasipo rekebisha leseni yao ifutwe watafutwe wawekezaji wengine serious” alisema.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alimuhakikishia Naibu Waziri kutekeleza maagizo aliyoyatoa kwa kuwachukulia hatua kali wawekezaji hao ikiwemo  kuwakamata wahusika.
Alisema kuwa awali baada ya kubaini wizi katika mgodi huo aliunda kamati ya ulinzi na usalama iliyohusisha Afisa madini mkazi,Afisa maendeleo,Afisa misitu na Afisa usalama  ambapo baada ya uchunguzi  kwenye mgodi ,maabara ,makontena pamoja na  kwenda  kwenye maabara za madini Dodoma,Bahi na Mwanza  walibaini carbon hiyo iliibwa na kupelekwa kwatika kiwanda hicho cha JEMA AFRICA LTD.

Katika taarifa ya kamati ya maalum iliyoundwa na Wilaya ya Handeni kufuatia maelekezo ya Naibu Waziri Biteko alipotembelea mgodi huo mapema mwaka huu  ilibaini  makosa tisa  ambayo ni ukiukwaji  wa sheria,kanuni na utaratibu wa kuingia mkataba usiotambulika kisheria kati ya kampuni ya CANACO na TANZANIA GOLD FIELDS,mgodi kutoendelezwa kwa muda uliopangwa kisheria ndani ya miezi 18,kuchenjua madini bila leseni na utumiaji wa kemikali ya Sayanaidi bila ya kibali cha mkemia mkuu wa serikaiai.

Mambo mengine ni kuwepo kwa udanganyifu wa kampuni ya CANACO na TANZANIA GOLD FIELDS kwa kudai kuwapo katika hatua ya majaribio wakati kuna usimikaji wa mitambo ya uchenjuaji bila kibali cha mkaguzi mkuu wa mgodi,kuendesha shughuli za mgodi bila kuwepo na meneja aliyeteuliwa kisheria,kufanya uchenjuaji wa madini  na marudio ya uchimbaji unaosababisha uharibifu wa mazingira bila ya kuwa na vibali vinavyostahiki,kusimika mtambo wa uchenjuaji wa marudio bila ya kuwa na vibali vya mkaguzi mkuu wa mgodi.


Naibu Waziri, Dotto Biteko(Kulia)na Mkuu wa Wilaya ya Handeni ,Godwin Godwe, wakiwa katika kikao kazi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, baada ya Naibu Waziri kuwasili wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uchimbaji madini.

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiwa katika baadhi ya vitendea kazi vya mgodi wa Madini Mali ya kampuni ya Canaco, vilivyozuiliwa kuondolewa eneo hilo hadi pale watakapofuata sheria za uchimbaji madini. 

Naibu Waziri,Dotto Biteko (kulia),Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe (Katikati)wakikagua eneo la mgodi wa Madini, katika kijiji cha Magambazi wilayani Handeni mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment