Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi
ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi wamesaini Mikataba Mitatu ya kuanza ujenzi
wa Vituo Saba vya Umahiri pamoja na Jengo la Mafunzo kwa Wachimbaji wadogo
katika Chuo Cha Madini, Dodoma.
Hafla ya utiaji saini
mikataba hiyo imefanyika leo tarehe 9 Julai, 2018, Makao Makuu ya Wizara ya
Madini jijini Dodoma na kushuhudiwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki na
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Akizungumza baada ya
utiaji saini, Waziri Kairuki amesema
kuwa, tukio hilo ni utekelezaji wa ahadi
aliyoitoa wakati akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ambapo alieleza kuwa, Serikali kupitia
Wizara ya Madini itaanza ujenzi wa ofisi saba za madini ili zitumike kama vituo
vya umahiri vya masuala ya madini.
Waziri Kairuki
amezitaja ofisi hizo kuwa ni Mpanda, Songea, Chunya, Tanga, bariadi, Bukoba na
Musoma na kuongeza kuwa, ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ya Chuo Cha Madini
Dodoma kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za madini zinazotekelezwa
na Chama Cha Wachimbaji Madini Wanawake.
“Ujenzi wa Vituo
hivyo unatekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
(SMMRP) ambapo moja ya malengo mahususi ya mradi huu ni kuboresha Sekta ya
madini nchini hususan kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kuwaongezea ujuzi katika
eneo la uchimbaji wa madini na kukuza uchumi,” amesisitiza Kairuki.
Akizungumzia umuhimu
wa vituo hivyo, alisema vimelenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia hususan
katika utafiti wa madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia
teknolojia rafiki kwa mazingira hususan zisizotumia kemikali ya Zebaki.
Ameongeza kuwa, vituo
hivyo pia vitatoa mafunzo ya biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo wa
madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora za
utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji wadogo.
Kuhusu gharama za
ujenzi wa vituo hivyo amesema kuwa ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi Bilioni 11.9.
Akizungumzia sababu
za kuingia Mkataba na SUMA JKT, Waziri Kairuki amesema kuwa, jeshi hilo
limekuwa likijihusisha na kazi mbalimbali
za ujenzi, kujiimarisha kwao nchini, uwezo wao kiufundi katika
kutekeleza miradi mikubwa, gharama nafuu, ubora na kuongeza kuwa, mkataba na
SUMA JKT utaokoa kiasi cha shilingi milioni
249.3 ikilinganisshwa na wakandarasi wengine.
Awali, akizungumza
katika hafla hiyo, Prof. Msanjila amesema kuwa, ujenzi wa vituo hivyo umelenga
kuwasaidia wananchi na zaidi ukilenga wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi amesema
kuwa, Jeshi hilo limejipanga kutekeleza mradi huo ndani ya muda uliopangwa wa
kipindi cha miezi sita na utekelezaji
wake utafanywa kwa weledi.
Kazi ya ujenzi wa
vituo hivyo itasimamiwa na washauri Elekezi
Kampuni ya Y & P Architects ambayo imesanifu majengo ya Chuo Cha Madini Dodoma na Kampuni ya
Interconsult Ltd ambayo imesanifu majengo ya Musoma, Bariadi na Bukoba.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi
Morgan Nyonyi wakisaini Mikataba ya Ujenzi wa Vituo vya Umahiri. Nyuma
wanaoshuhudia ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa kwanza kushoto) na Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (Kulia). Wengine ni wanasheria kutoka Wizara
ya Madini na Suma JKT.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya
Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi Morgan Nyonyi wakibadilishana Mikataba ya ujenzi
wa Vituo vya Umahiri baada ya kusaini.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT, Mhandisi
Morgan Nyonyi wakisaini Mikataba ya Ujenzi wa Vituo vya Umahiri. Nyuma
wanaoshuhudia ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki (wa kwanza kushoto) na Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (Kulia). Wengine ni wanasheria kutoka Wizara
ya Madini na Suma JKT.
No comments:
Post a Comment