Na Greyson Mwase, Morogoro
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesimamisha shughuli za uchimbaji madini ya kinywe
na vito katika machimbo ya Epanko yaliyopo katika wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro ili Serikali iweke kwanza utaratibu mzuri wa usimamizi wa shughuli za
uchimbaji madini katika eneo hilo kabla ya kuruhusu uchimbaji madini kuendelea.
Biteko
ametoa agizo hilo leo tarehe 10 Julai, 2018 kwenye ziara yake aliyoifanya
katika machimbo hayo yenye lengo la
kukagua shughuli za uchimbaji madini pamoja na kufuatilia utekelezaji wa
mapendekezo yaliyotolewa na Kamati
iliyoundwa na Tume ya Madini kwa ajili ya kuchunguza shughuli za uchimbaji
madini katika machimbo hayo.
Hivi
karibuni, Naibu Waziri Biteko alielekeza Tume ya Madini kuunda kamati hiyo kwa
ajili ya uchunguzi huo na kuwasilisha taarifa
yenye mapendekezo ya namna ya
kuboresha uchimbaji katika machimbo ya Epanko.
Naibu Waziri Biteko mara baada ya kutembelea
eneo hilo na kushuhudia shughuli za uchimbaji madini zikiendelea pasipo kufuata
kanuni za mazingira huku katika baadhi ya maeneo mitambo ikiwa imefungwa kwa
ajili ya kuondolewa, aliagiza wamiliki wa leseni kukusanya vifaa vya uchimbaji
madini chini ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kusimamisha shughuli
za uchimbaji madini ndani ya siku tatu
hadi Serikali itakapojiridhisha juu ya mwenendo wa shughuli za uchimbaji
madini.
Aliendelea
kusema kuwa, katika eneo hilo kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria na kanuni za
mazingira kwa kuchepusha mto Kilombero hali iliyopelekea uharibifu mkubwa wa
mazingira
Alisema
kuwa wachimbaji madini wamekuwa wakitiririsha maji machafu kutoka migodini
kwenda kwenye mto Kilombero ambao ni tegemeo kubwa la wananchi wanaozunguka
eneo la Epanko jambo ambalo linahatarisha afya zao.
Alisisitiza
kuwa wachimbaji madini wengi wamekuwa wakiendesha shughuli zao pasipo kuwa na
vibali vya mazingira kama sheria na kanuni za uchimbaji madini zinavyowataka.
Aliongeza
kuwa kumekuwepo na changamoto ya kutokuwepo kwa uwazi katika mikataba kati ya
wamiliki wa leseni na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini,
mapato na kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa serikalini
Aliongeza
kuwa kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya wamiliki wenye leseni kudhulumiwa
haki zao na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini na kusisitiza
kuwa ni vyema Serikali ikasitisha shughuli zote za uchimbaji madini katika eneo
la Epanko na kuanza ukaguzi wa leseni moja moja ili kuona kama zinakidhi sheria
na kanuni za madini kabla ya kuruhusu shughuli za uchimbaji madini kuendelea.
Katika
hatua nyingine, Biteko alielekeza uanzishwaji wa Ofisi ya Madini katika wilaya ya
Ulanga itakayosimamia kwa karibu mwenendo wa shughuli za uchimbaji madini
katika wilaya hiyo.
Awali
akitoa taarifa ya kamati iliyoundwa kwa ajili ya uchunguzi wa
shughuli za uchimbaji madini ya kinywe
na vito katika machimbo ya Epanko, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof.
Shukran Manya alisema kuwa kamati hiyo ilibaini kuwa uchimbaji madini katika
eneo hilo ulikuwa huuzingatii sheria na kanuni za madini pamoja na mazingira na
kutokuwepo kwa uwazi katika mapato na matumizi katika migodi.
Aliongeza
kuwa kamati ilibaini kutokuwepo kwa mikataba kati ya wamiliki wa leseni za
madini na kampuni zinazoendesha shughuli za uchimbaji madini zilizosajiliwa
kwenye Ofisi za Madini na Halmashauri hali ambayo imekuwa ikisababisha
migogoro ya mara kwa mara.
Alitaja
wachimbaji wanaofanya kazi katika eneo la Epanko kuwa ni pamoja na Peter
Chamtitu, Jonas Mpanduli, Sabinus Chigumbi, Franone & Gems na Paskali Jonas
Mpanduli & Partners ambao wamelipa mrabaha hadi sasa.
Alitaja
wachimbaji wengine ambao hawajalipa mrabaha mpaka sasa kuwa ni pamoja na
Mathias Osward Lunkombe & Partners, John Joseph Ntoga na Protas Osward
Lunkombe, Moshi Saidi Nassoro na Christoms Martin Msakamba na Christoms Martin
Msakamba na Bonifas Julai.
Wachimbaji
wengine ambao hawajalipa mrabaha ni Joseph Kabu Mworia, John Joseph Ntoga na
Franone Mining & Gems Co. Ltd, Joseph Paulo Mwangu & Partners, Mohamedi
Said Magonga & Partners, Interstate Mining Limited na Flora Amadei Lyaupe
& Partners.
Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukran Manya akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa shughuli za uchimbaji
madini ya kinywe na vito katika machimbo ya Epanko mbele ya Naibu Waziri wa
Madini, Dotto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Jackob Kassema pamoja na
watendaji kutoka Wizara ya Madini (hawapo pichani) kwenye ofisi ya Mkuu wa
wilaya kabla ya kufanya ziara katika machimbo ya Epanko yaliyopo wilayani
Ulanga mkoani Morogoro tarehe 10 Julai, 2018.
Kutoka
kulia mbele, Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Katibu Mtendaji wa Tume ya
Madini, Prof. Shukran Manya na Kamishna wa Madini kutoka Tume ya Madini Dkt.
Athanas Macheyeki wakiendelea na ziara katika machimbo ya Epanko yaliyopo
wilayani Ulanga mkoani Morogoro.
Kutoka
kushoto Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Katibu Mtendaji wa Tume ya
Madini, Prof. Shukran Manya na Kamishna wa Madini kutoka Tume ya Madini Dkt.
Athanas Macheyeki wakijadiliana jambo katika ziara kwenye machimbo ya Epanko
yaliyopo wilayani Ulanga mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment