Na Greyson Mwase, Tunduru
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo tarehe 19 Julai, 2018 amesema kuwa wanunuzi
wa madini aina ya vito kote nchini wasiokuwa na mashine kwa ajili ya kukata na
kung’arisha madini hayo watanyang’anywa leseni kwa kuwa wanaendesha biashara
kinyume na taratibu kama Sheria ya Mpya ya Madini ya Mwaka 2017 inavyofafanua.
Naibu
Waziri Biteko aliyasema hayo katika mkutano wake na wanunuzi wa madini aina ya vito kutoka Wilaya ya Tunduru
uliofanyika mjini Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni kama moja ya sehemu ya ziara
yake katika mikoa ya kusini yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini
zinazofanywa na wachimbaji wadogo, kuzungumza nao pamoja na kutatua changamoto
mbalimbali.
Alisema
kuwa ni kosa la kisheria kwa mnunuzi yoyote wa madini aina ya vito kuendesha
biashara pasipo kuwa na mashine za kukatia na kung’arisha vito.
“Sheria inamtaka mnunuzi ambaye ni mtanzania kuwa na mashine 5 na mnunuzi wa
kigeni kuwa na mashine 30 za kukata na kung’arisha madini ya vito, tunataka
madini haya yaongeze thamani ndani ya
nchi ili kuongeza mapato serikalini,” alisema Biteko.
Aidha,
Biteko alimtaka Afisa Madini wa Tunduru Mjiolojia Abraham Nkya kwa kushirikiana
na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Zuberi Homera na Vyombo vya Ulinzi na
Usalama vya Wilaya kufanya ukaguzi kwenye maduka ya wanunuzi watakaopewa leseni
mpya ili kubaini kama wana mashine za kukata na kung’arisha vito na kuchukua
hatua za kisheria kwa wanunuzi watakaobainika kutokuwa na mashine hizo ikiwa ni
pamoja na kuwaandikia hati za makosa na kuwanyang’anya leseni.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wanunuzi wa kigeni wanaofanya
biashara kwa ubia na watanzania kuhakikisha wanawashirikisha kwa kila jambo
kama mikataba yao inavyotaka.
Aliendelea
kusema kuwa Sheria ya Madini inamtaka
mzawa kuwa na umiliki wa isiyopungua asilimia
25 kwa kuwa hana uwezo wa kifedha na teknolojia na raia wa kigeni kuwa na
asilimia 75 na kusisitiza kuwa ni vyema wakashirikiana kwa kila hatua kwenye
biashara ya madini.
“Haiwezekani mbia wa Tanzania hatembelei kabisa eneo la biashara hali
inayopelekea kutofahamu kabisa mwenendo
wa biashara na kumwacha mbia ambaye ni raia wa kigeni akifanya kila kitu, hii
inapelekea hata madini kutoroshwa nje ya nchi,” alisisitiza Biteko.
Aidha,
aliwataka wanunuzi wa madini kuweka kumbukumbu za mauzo za kila siku ili kuweza
kufanya ulinganisho wake na madini yanayosafirishwa nje ya nchi ili
kujiridhisha na uwiano wake.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri Biteko mbali na kutembelea
baadhi ya migodi iliyopo katika kijiji cha Ngapa Mtoni kilichopo wilayani
Tunduru mkoani Ruvuma alikutana na wachimbaji wadogo lengo likiwa ni kukusanya na kutatua kero mbambalimbali.
Akizungumza
kwa niaba ya wachimbaji hao wa madini ya vito, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo
wa Madini katika kijiji cha Ngapa Mtoni, Abel Kasibila alieleza changamoto hizo
kuwa ni pamoja na kutumia nyenzo duni katika uchimbaji wa madini ya vito,
kutokuwepo kwa watafiti ambao wangerahisisha kwenye ugunduzi wa madini na miundombinu ya barabara
kutokuwa rafiki kwenye usafirishaji wa madini.
Alisema
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na malipo ya leseni kufanyika kwa fedha za
kigeni na uwepo wa leseni kubwa bila ya wahusika kufahamika.
Awali
akielezea hali ya uzalishaji wa madini ya vito na ujenzi katika wilaya ya
Tunduru kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Zuberi Homera
alisema takwimu za usafirishaji wa madini ya vito katika kipindi cha Julai 2017
hadi Juni, 2018 zilionyesha kuwa jumla ya gramu 24,279.416 zenye thamani ya
Dola za Marekani 108, 807 zilisafirishwa na kulipiwa mrabaha wa shilingi milioni 14.6.
Aliongeza
kuwa jumla ya gramu 1196.01 zenye thamani ya shilingi milioni 160.9
zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa awali wa shilingi milioni 9.6 katika Ofisi ya Madini Tunduru.
Aliendelea
kufafanua kuwa jumla ya tani 1,882 za madini ya ujenzi (mchanga) zenye thamani ya shilingi milioni 33.9
zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa shilingi milioni 1,050,000.
Aidha
alisema kuwa wilaya ya Tunduru ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni
85.1 kati ya shilingi milioni 100 iliyopangiwa kukusanya kwa mwaka 2017/2018
sawa na asilimia 85.16.
Akielezea
mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli, Homera alisema kuwa wilaya yake imepanga kutoa huduma za ugani kwa kutoa
ushauri kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu uchimbaji bora, salama na
unaozingatia utunzaji wa mazingira na kuishauri Wizara ya Madini kutoa mafunzo kupitia Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO), Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa
wachimbaji wadogo na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yenye madini ili waweze
kuelewa Sheria Mpya ya Madini na kanuni zake.
Aliitaja
mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuiomba Tume ya Madini kutenga eneo la Ngapa
kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini katika wilaya ya Tunduru, kufanya
kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya machimbo na kuhamasisha wenye uwezo
kuanzisha viwanda vya kusanifu madini ya vito.
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia madini aina ya vito kwenye mchanga
kwenye eneo la uchenjuaji katika Mgodi wa Monica Gem uliopo Ngapa Mtoni
wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko akifafanua jambo kwenye mkutano wake na
wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji cha Ngapa Mtoni wilayani Tunduru
mkoani Ruvuma.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiangalia uchenjuaji wa madini ya
vito unaoendelea katika Mgodi wa Monica Gem uliopo Ngapa Mtoni wilayani Tunduru
mkoani Ruvuma tarehe 19 Julai, 2018.
|
No comments:
Post a Comment