Asteria
Muhozya na Samwel Mtuwa, Dodoma
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
wa Madini Tanzania (GST) inazo fursa nyingi ambazo zingeweza kuifanya kuwa
Taasisi inayoingiza mapato makubwa.
Prof. Msanjila
ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo iliyolenga
kujifunza namna GST inavyotekeleza majukumu yake, kufahamiana na watumishi wa
taasisi hiyo na kufahamu changamoto zinazoikabili.
Kutokana na fursa za kibiashara zilizopo
katika taasisi hiyo, Prof. Msanjila ameishauri kujikita katika kutoa huduma za
kibiashara kutokana na uwezo iliyonayo na huduma inayotoa kwa jamii hususan
wadau wa Sekta ya Madini nchini.
Amesema
umuhimu wa GST bado haujatumika katika namna inavyotakiwa na kueleza kuwa,
kutokana na Mabadiliko yaliyofanyika katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010,
yamelenga kuipa uzito taasisi hiyo.
Pia, Prof.
Msanjila amewataka watumishi wa GST kuwa na udhubutu na kila mmoja kuwajibika
kikamilifu katika eneo lake analofanyia kazi na pindi wanapohitaji mwongozo
kutoka wizarani, wasisite kufanya hivyo.
Katika hatua
nyingine, Prof. Msanjila ameipongeza taasisi hiyo kutokana na mafanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza kuwa, Wizara ya
Madini imepata sifa kubwa kutokana na namna GST ilivyotekeleza majukumu yake
kikamilifu.
“Taasisi yenu
imechangia sana kwenye sifa ilizopata wizara wakati wa uwasilishaji wa Bajeti
yake mwezi Mei, nawapongeza sana kwa utendaji kazi, matokeo yenu tunayaona,”
amesisitiza Prof. Msanjila.
Vilevile,
ameishukuru kutokana na namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa wizara na
kusema kuwa, “ kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya wizara na taasisi. Mimi,
Waziri na Naibu Mawaziri tunashukuru,”
Akizungumzia suala
la kuwaendeleza watumishi, amesema kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha kwamba
watumishi wanajiendeleza kielimu na kuongeza kuwa, tayari imeanza mchakato ili
watumishi waweze kupata nafasi za ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali.
“Tunakamilisha suala la kupata ufadhili. Wenye nia ya kusoma nafasi zitakuwepo.
Binafsi napenda sana watu waende shule na hasa vijana,” amesema Prof. Msanjila.
Katika ziara
hiyo, Prof. Msanjila ametembelea Idara mbalimbali za GST ikiwemo maabara mbalimbali
za utambuzi wa madini na utengenezaji wa ramani mbalimbali za madini.
Awali, Prof.
Msanjila alifanya kikao na Menejimenti ya GST, pamoja na kuzungumza na watuishi
wa taasisi hiyo. Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu ameambatana na Mkurugenzi wa
Utawala na RasilimaliWatu, Issa Nchasi.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof.
Simon Msanjila akiangalia sampuli za madini kupitia darubini ndani ya Maabara
ya Utafiti wa Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST). Katibu Mkuu amefanya ziara GST ya kuangalia kazi mbalimbali zinazofanywa
na taasisi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof.
Simon Msanjila akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini Tanzania (GST) baada ya kutembelea kazi mbalimbali zinazofanywa na
Taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment