· Aaagiza
sampuli kukabidhiwa GST na wahusika kutafutwa popote.
Na Greyson Mwase, Songea
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo tarehe 16 Julai, 2017 amefanya ziara katika
mkoa wa Ruvuma lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini
zinazofanywa na wachimbaji wadogo pamoja na kusikiliza kero mbalimbalimbali.
Katika
ziara yake aliambatana na wataalam
kutoka Wizara ya Madini, Maafisa Madini
wa Songea, Kulwa Kabadi na Mhandisi George Wandinha, Mkuu wa Wilaya ya Songea,
Pololet Mgema pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.
Akiwa
katika eneo la Madiba lililopo wilayani Songea mkoani Ruvuma, Naibu Waziri
Biteko alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa mwananchi mmoja, Allan Mbilinyi
kunakoelezwa kuhifadhiwa masanduku 209 ya sampuli za madini ya aina
mbalimbali na kushuhudia masanduku hayo
yakiwa yametelekezwa bila kuwa na dalili za aina yoyote ya usafirishwaji.
Awali
Naibu Waziri Biteko alipewa taarifa na wananchi ambao ni wasamaria wema kutoka
katika eneo la Madaba juu ya uwepo wa sampuli za madini hayo na kusisitiza
kuwa hatua hiyo inatokana na kuunga
mkono kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano
kupitia Wizara ya Madini kwenye
ulindaji wa rasilimali za madini.
Walisema
kuwa, tofauti na sampuli za masanduku 209 ya madini ya aina mbalimbali
yaliyotelekezwa, kipindi cha nyuma walishuhudia mzigo mkubwa wa masanduku yenye
sampuli za madini ya aina mbalimbali yakisafirishwa kutokea eneo
yalipotelekezwa masanduku husika.
Naye
Naibu Waziri Biteko aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa za madini
yaliyotelekezwa alielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia na kumpatia
taarifa kabla ya kufika na kuthibitisha na kusisitiza kuwa aliamua kufika ili
kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua za kisheria.
Hata
hiyo baada ya kufika eneo husika, Waziri Biteko aliangalia mkataba uliosainiwa
kati ya kampuni ya Sino Hydro kutoka China na Allan Mbilinyi kuhusu uhifadhi wa
madini hayo na kubaini kutokuwepo kwa kibali cha serikali jambo ambalo ni
kinyume na sheria za nchi.
“Ni
kosa la kisheria kuhifadhi madini ya aina yoyote ndani ya mahali popote bila ya
Serikali kuwa na taarifa, faini yake ni kubwa pamoja na kifungo,” alisema
Biteko
Biteko
alielekeza sampuli za madini kuwa chini ya uangalizi wa vyombo vya ulinzi na
usalama vya Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema kabla ya
kukabidhiwa kwa Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa
ajili ya uchunguzi ili kubaini thamani halisi.
Alisisitiza
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo makini katika ufuatiliaji wa madini na
kusisitiza kuwa Serikali itahakikisha wahusika wanakamatwa sehemu yoyote na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Mtepa kilichopo Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma,
Biteko mbali na kuwapongeza wananchi kwa uzalendo wa kutoa taarifa kuhusiana na
uhalifu unaofanywa na watu wasio waaminifu kwenye sekta ya madini, aliwataka
wananchi hao kuendelea kulinda rasilimali za madini na kusisitiza kuwa Serikali
ipo tayari kushirikiana nao ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa kwenye
ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha
Naibu Waziri Biteko akizungumza kwa nyakati tofauti katika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina
Mdeme alisema kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa katika kuhakikisha kuwa
Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa ikiwa ni pamoja na maboresho ya Sheria
ya Madini inayomtambua mtanzania kama mmiliki wa madini na kudhibiti
utoroshwaji wa madini nje ya nchi.
Aliwataka
wachimbaji madini wanapopata leseni kujitambulisha kwanza kwa viongozi kuanzia
ngazi ya Mkoa, Wilaya na kijiji pamoja na kulipa fidia kwa wananchi kabla ya kuanza shughuli zozote za madini.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisema kuwa atafuatilia kila hatua ya namna
taarifa zilivyofikishwa Serikalini kuhusu madini yaliyotelekezwa na hatua
zilizochukuliwa pamoja na wahusika wote kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
Wakati
huohuo Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa
kazi kubwa ya usimamizi wa sekta ya
madini ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu shughuli za madini kwa kila
mkoa na kuchukua hatua stahiki pale
inapohitajika.
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia sehemu ya sampuli za madini yaliyotelekezwa.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na wananchi wa Madaba
wilayani Songea mkoani Ruvuma.
|
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Christina Mndeme (kulia) kabla ya kuanza ziara yake katika mkoa huo.
|
No comments:
Post a Comment