Na Greyson Mwase, Morogoro
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko amekamata madini ya vito aina ya Rhodilite yenye uzito wa
takribani tani saba yaliyokuwa yamefichwa nyumbani kwa mchimbaji wa madini
hayo, Juvenal Mnene ambaye ni mmiliki wa kampuni ya J. J. Mnene & Partners
na kuamuru kukabidhiwa Serikalini pamoja na mmiliki huyo kufikishwa mahakamani.
Naibu
Waziri Biteko amekamata madini hayo katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya
ya Gairo mkoani Morogoro lengo likiwa ni kukagua shughuli za wachimbaji
wadogo wa madini ya vito na ujenzi na
kutatua changamoto mbalimbali.
Katika
ziara hiyo, Biteko aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Madini, Tume ya
Madini, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya ya Gairo, Madiwani na Mwakilishi wa Mbunge wa Gairo.
Mara
baada ya kuwasili katika mgodi wa mchimbaji huyo uliopo eneo la Rubeho, Bitteko
alibaini kuwa mchimbaji huyo alikuwa
amelipa mrabaha wa shilingi 400,000 tu tangu mwaka 2013 ndipo akataka kupewa
taarifa ya uzalishaji na kiasi cha
malipo yaliyolipwa serikalini ikiwa ni pamoja na kodi mbalimbali ambapo
alielezwa na mmiliki wa mgodi huo Juvenal Mnene kuwa taarifa ya uzalishaji wa madini hayo na
vielelezo vya malipo yaliyofanyika serikalini ipo nyumbani.
Naibu
Waziri Biteko pamoja na msafara wake alielekea nyumbani kwa mmiliki wa mgodi
huo, ambapo alishuhudia madini ya vito aina ya Rhodilite yakiwa yamerundikwa
kwenye chumba kimoja na kufungwa kwa kufuli bila kuwekwa lakiri (seal) ya
serikali kinyume na sheria ya madini inavyotaka.
“Huu
ni utoroshwaji wa madini kwasababu haiwezekani madini yahifadhiwe ndani ya
chumba bila serikali kufahamu na kuweka lakiri, na kama serikali hatuwezi
kukubali kuona madini yakitoroshwa nje ya nchi na wachimbaji wa madini wasio
waaminifu,” alisema Biteko
Katika
hatua nyingine, Biteko alibaini mchimbaji huyo alikuwa na mtambo wa kuchenjua madini
hayo nyumbani kwake kwa nyuma bila kuwa
na leseni ya uchenjuaji madini kama sheria ya madini inavyotaka.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo, Naibu Waziri Biteko alimwagiza
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Musa Mwakasula kwa kushirikiana na Afisa Madini
Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kukamata madini hayo kuyapima ili kujua kiasi chake
halisi na kisha kumfikisha mtuhumiwa katika vyombo vya sheria.
Aliongeza
kuwa Wizara ya Madini itawachukulia hatua kali za kisheria watu wote
waliohusika na mchakato mzima wa kuficha madini hayo.
“
Haiwezekani kabisa juzi juzi tumekamata
madini yenye uzito wa tani 75 jijini Dar es Salaam, ni lazima tuhakikishe
tunalinda rasilimali za madini kwa nguvu zote ili ziwe na mchango mkubwa katika
ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisisitiza Biteko.
Wakati
huo huo, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani
Gairo mkoani Morogoro, Naibu Waziri Biteko alisema Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kupitia Wizara ya Madini imeweka
mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango
mkubwa wa uchumi wa nchi kwa kuboresha sheria za madini.
Alifafanua
kuwa, Wizara ya Madini ipo katika mchakato wa kurasimisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni mara baada ya taratibu kukamilika ili
kuondokana na umaskini kutokana na kujiajiri
Alisema
kuwa, awali rasilimali za madini zilichukuliwa kama umiliki wa wawekezaji wa
nje ya nchi lakini mara baada ya maboresho ya Sheria ya Madini wananchi sasa
wana haki zote za umiliki wa rasilimali za madini.
Akizungumzia
suala la bei elekezi kwenye madini ya ujenzi, Biteko alisema Serikali ipo
katika mpango wa kukaa na wanunuzi wa madini hayo hasa wenye viwanda vya
kutengeneza marumaru( tiles) na kukubaliana bei ambayo itafanywa kuwa bei
elekezi ya madini hayo ili wananchi wanufaike.
Katika
hatua nyingine, Biteko aliwataka wachimbaji hao kulipa kodi mbalimbali na
kufuata kanuni na sheria za uchimbaji madini.
Wakati
huo huo akizungumza katika mkutano huo, Mkuu
wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe alieleza changamoto mbalimbali katika
uchimbaji madini katika wilaya yake kuwa ni pamoja na wachimbaji wadogo wa
madini kutokuwa na leseni kwa kisingizio wameshawasilisha maombi yao kwenye
ofisi za madini, kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa uchimbaji madini na
kutokuwepo kwa sehemu za kuhifadhia madini.
Aliendelea
kusema changamoto nyingine kuwa ni
pamoja na ukosefu wa mitaji hususan kwa wachimbaji wadogo wa madini na
upatikanaji wa soko la uhakika la madini hayo.
Mkuu
wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe (kushoto) akielezea shughuli za uchimbaji
madini katika wilaya yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati)
kwenye ziara yake katika eneo la Rubeho wilayani Gairo mkoani Morogoro tarehe
11 Julai, 2018.
Mchimbaji
madini aliyekamatwa akiwa amehifadhi madini aina ya Rhodilite yenye uzito wa
takribani tani saba nyumbani kwake, Juvenal Mnene (katikati) akionyesha nyaraka
mbalimbali kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko.
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akimhoji Mchimbaji madini
aliyekamatwa akiwa amehifadhi madini aina ya Rhodilite yenye uzito wa takribani
tani saba nyumbani kwake, Juvenal Mnene (kulia).
Sehemu
ya madini ya vito aina ya Rhodilite yaliyokamatwa nyumbani kwa mchimbaji Juvenal Mnene katika mtaa wa
Magoweko kwenye halmashauri ya mji wa Gairo mkoani Morogoro.
Naibu
Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kichangani
kilichopo wilayani Gairo mkoani Morogoro (hawapo pichani)katika mkutano wa
hadhara.
Sehemu
ya na wananchi wa kijiji cha Kichangani kilichopo wilayani Gairo mkoani
Morogoro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani)
kwenye mkutano wa hadhara.
No comments:
Post a Comment