Wednesday, July 18, 2018

Biteko afanya ziara Mgodi wa Tancoal


·        Aagiza  mgodi kulipa kodi stahiki kwa mujibu Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017 badala ya Sheria ya Madini ya Mwaka 1998
·        Alishauri shirika la NDC kupeleka haraka mwakilishi wake kwenye mgodi huo

Na Greyson Mwase, Mbinga

Naibu Waziri wa Madini,  Dotto Biteko leo tarehe 17 Julai, 2018 amefanya ziara katika mgodi wa Makaa ya Mawe wa Tancoal uliopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Katika msafara wake aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya
ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Maafisa Madini wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga,  pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Mbinga.

Mara baada ya kufika katika mgodi huo na kupewa taarifa  juu ya shughuli za uendeshaji  wa mgodi huo,  Naibu Waziri Biteko aliagiza mgodi huo kuhakikisha unalipa kodi stahiki ya madini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si hapa mgodini, na ninatoa mwezi mmoja mhakikishe mmerekebisha kasoro zote na fedha ambazo hazikulipwa zilipwe. Ninatamani mimi niwe wa mwisho kuliongelea suala hilo, migodi mingine yote imeshaanza kutekeleza sheria hii sijui kwanini mmebaki ninyi,”alisema Biteko.

Alisema ni wakati sasa kwa wananchi wa Tanzania kunufaika na rasilimali za madini kupitia kodi stahiki ambazo zinatumika katika kukuza sekta nyingine ikiwa ni pamoja na   huduma za kijamii.

Alisisitiza kuwa, endapo hatua husika hazitachukuliwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaandikia mgodi hati ya makosa itakayopelekea kunyang’anywa leseni ya uchimbaji na uuzaji wa madini.

Aliongeza kuwa ni jukumu la kampuni ya Tancoal kusafirisha madini hadi eneo la wanunuzi kwa kuwa wana leseni za uchimbaji na uuzaji na si wanunuzi wasio na leseni hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria za Madini.

Pamoja na kuitaka kampuni ya  Tancoal kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria alishauri kampuni hiyo kufanya kazi kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na mbia wake ambaye ni Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kupitia usimamizi  wa uzalishaji, upimaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Aidha, Naibu Waziri  alisikitishwa na kitendo cha NDC kutokuwa na mwakilishi wake hapo mgodini toka mwaka 2016 baada ya afisa aliyekuwepo kustaafu.

“ Ninajua NDC hampo Wizara ya Madini, lakini mpo Serikalini na mimi ni Naibu Waziri wa Serikali hii ninawashauri mlete haraka mwakilishi kwenye mgodi huu ili kuwepo na jicho la NDC kama mbia kwenye mgodi huu badala ya kutegemea taarifa za mbia wenu tu ambaye ni Tancoal,”alisisitiza.

Wakati huo huo akizungumza katika mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini, Naibu Waziri Biteko alisema kuwa  mara baada ya taratibu kukamilika leseni za biashara ya madini zinatarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwezi huu na kuwataka kujiandaa na soko litakalotokana na wanunuzi wengi watakaojitokeza.

Katika hatua nyingine, Biteko aliwataka maafisa madini nchi nzima kusikiliza kero za wachimbaji wadogo wa madini pamoja na kuzitafutia ufumbuzi.

Aliwataka wachimbaji madini kuhakikisha wanafanyia leseni zao kazi na zile ambazo zitaonekana hazifanyiwi kazi kwa muda mrefu zitafutwa na kupewa wachimbaji wadogo.

Aidha alisisitiza wamiliki wa migodi ya madini  nchi nzima kuajiri watanzania wenye uwezo kama  Sheria ya Madini inavyofafanua badala ya kuajiri raia wa kigeni tu.

Aidha, Naibu Waziri Biteko mbali na kumpongeza Rais John Magufuli kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi, aliwataka wachimbaji wa madini kumuunga mkono kupitia uzalendo kwenye usimamizi wa madini kwa manufaa ya Taifa.

“Tunataka madini haya baada ya miaka kadhaa yalete matunda kama vile huduma za jamii hususan elimu, hospitali, barabara nzuri n.k” alisisitiza Biteko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme mbali na kumpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa anayofanya katika usimamizi wa sekta ya madini alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga kupima maeneo  maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara kati ya wachimbaji hao na wakulima au wafugaji.


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kulia mbele) na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme (katikati) wakiendelea na ziara katika eneo la mgodi wa Tancoal uliopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 17 Julai, 2018.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiangalia moja ya jiwe la makaa ya mawe. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akitoa maelekezo kwa baadhi ya watumishi wa kampuni ya Tancoal.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini (hawapo pichani) katika eneo Masuguru lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini katika eneo Masuguru lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakifuatilia  ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (hayupo pichani).

No comments:

Post a Comment