ü Aikabidhi Vitendea kazi
ü Prof. Kikula asisitiza uadilifu
Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amezindua Tume ya Madini sambamba na kukabidhi vitendea Kazi
kwa Mwenyekiti wake Prof. Idris Kikula pamoja na Makamishna wa Tume hiyo.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi huo, Waziri Kairuki alisisitiza kuwa, ni imani yake, imani ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli na Watanzania wote kuwa Tume hiyo itabadilisha simulizi za
Sekta ya madini kutoka kuwa za kukatisha tamaa na kuwa za matumaini na hivyo
kuibadili historia ya sekta ya madini kutoka kuwa ya miguno na manung'uniko na
kuwa ya kujipongeza na kujivunia.
"Nataka mtambue
kuwa ninyi sasa ndiyo macho, masikio, pua na mikono yetu kwenye sekta ya
madini," alisisitiza Waziri Kairuki.
Aliongeza
kuwa,Watanzania wana matarajio makubwa na Tume hiyo na kueleza kuwa, wanataka
kulala usingizi wakiamini kuwa sekta ya madini iko katika mikono safi na salama
kwa kuwa wanaamini Tume itatenda haki,
itasimamia ukweli na kuzingatia maslahi ya
kesho, kesho kutwa na vizazi vijavyo.
Aidha, Waziri Kairuki
alitumia fursa hiyo kuishauri Tume ya Madini kuyafanyia kazi masuala kadhaa
ambayo yatakuwa na tija kwa sekta ya Madini na kuyataja kuwa ni pamoja na kukamilisha kwa wakati zoezi la kupitia
maombi ya leseni huku akisisitiza zoezi hilo kuendana na upekuzi wa kina juu ya
waombaji wa leseni ya haki miliki ya madini ili kujiridhisha na kuhakikisha
kwamba wanaopatiwa leseni ni wale tu wenye sifa, vigezo na uwezo wa kuwekeza.
"Zoezi hili
lihakikishe kwamba kila anayefanya biashara ya madini ana leseni na leseni hai
iliyolipiwa," alisisitiza Kairuki.
Pia, aliishauri Tume
kuhakikisha inawadhibiti watu au makampuni ambayo yanashikilia leseni
walizopewa kwa muda mrefu bila kuziendeleza kinyume na masharti waliyopewa
wakati.
Ushauri mwingine
nikuhakikisha kwamba mrefu awadhibiti watu au makapuni ambayo yanashikilia
leseni walizopewa kwa muda mrefu bila kuziendeleza kinyume na msharti
waliyopewa wakati wa kuidhinishiwa leseni.
Vilevile,
alishauri muhimu wa kuwepo uataratibu wa
kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuona maendeleo ya uwekezaji katika migodi
ambayo imepatiwa leseni.
"Kwa kufanya
hivyo mtaweza kujiridhisha kwamba mlichoahidiwa na mwekezaji ndicho kinachofanyika
na pia mtaweza kushughulikia changamoto mapema," alisisitiza Kairuki.
Pamoja na hayo
alishauri kuhusu uwezekano wa kuweka utaratibu wa kutoa bei elekezi za madini
aina mbalimbali iwe madini ya ujenzi, madini ya viwandani na mengine na kuongeza
kuwa, utaratibu huo utasaidia sana
wachimbaji wadogo na wa kati." Zoezi hili liende na kuhakikisha kwamba
tunasimamia vyema uwasilishaji wa taarifa za mienendo ya biashara ya madini na
uzalishaji," aliongeza Kairuki.
Ushauri mwingine
ulitolewa kuwa, Tume iangalie uwezekano wa kuanzisha rejista za uzalishaji
unaofanyika na pia kuwa na rekodi za maafisa madini wanaokagua uzalishaji na uthamini wa madini.
Akizungumzia upande
wa vibali alishauri mauzo ya madini nje ya nchi ni vyema yakafanyika kwa
mapitio ama vibali ili kuhakikisha panakuwepo maelezo na taarifa za kina za
madini yanayosafirishwa kuhusu yalikotoka.
"Vilevile kwa
kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tuangalie mbinu za kisasa za kudhibiti utoroshaji wa madini ili
kudhibiti biashara haramu ya madini," alisema Waziri Kairuki.
Halikadhalika,
alizungumzia kuhusu Serikali kupata mapato stahiki ambapo alishauri kufanyika
ukaguzi na uhakiki wa kiasi na ubora wa madini yanayozalishwa na migodi
mikubwa, ya kati, na midogo na
kuhakikisha wachimbaji wadogo ambao
wanafanya uchimbaji bila kutambulika wafanyiwe utaratibu ili warasimishwe.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idrisa Kikula aliwataka watumishi wa Tume
kuwa waadilifu na kuonesha weledi kwenye utendaji wao ili kulinda heshima
iliyopewa Tume.
Aliongeza kuwa, Tume
imepokea kwa dhati maelekezo yote na maangalizo yote muhimu ambayo yameshauriwa
kufanyiwa kazi ili sekta ya madini ilete tija iyokuwa kusudiwa.
Pia, aliongeza kuwa,
tayari Tume imepokea taarifa nyingi hasa
za migogoro ambayo kiuhalisia inatakiwa kupata ufumbuzi na kuongeza kuwa, Tume
itatengeneza kanzidata ya migogoro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini Dustan Kitandula alisema kuwa, watanzania wana matumaini makubwa na
sekta ya madini baada ya kuundwa Tume na kuamini kuwa, itawaondoka kwenye
umaskini.
Uzunduzi wa Tume ulifanyika tarehe 30 Mei, 2018 jijini Dodoma. Kwa
mujibu wa maelezo ya Waziri Kairuki, Tume inaundwa na Ofisi za madini zilizoko
Mikoani, ofisi zitakazokuwa migodini, Maabara na Makao Makuu ya Tume.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya Pamoja na Makamishna wa Tume ya Madini. Wengine ni Naibu Mawaziri wa Wizara ya Madini na |
Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya Pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri kutoka Wizara mbalimbali walishiriki uzinduzi wa Tume. |
Waziri wa Madini Angellah Kairuki kushoto akimkabidhi Vitendea kazi Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idrisa Kikula. |
No comments:
Post a Comment