Monday, June 4, 2018

Waziri Kairuki afunga Maonesho ya Madini


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amefunga rasmi Maonesho ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Bunge jijini, Dodoma kuanzia tarehe 30 Mei hadi tarehe 1 Juni, 2018.

Akifunga maonesho hayo, Waziri Kairuki aliwashukuru washiriki wote wa maonesho hayo ambayo yalizishirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa (TME) na kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji na uongezaji thamani madini na kueleza kuwa, yametoa elimu kubwa kuhusu Sekta ya madini kwa Wabunge waliyotembelea.

“Yamekuwa ni maonesho ya kipekee na yametoa elimu kubwa kwa wabunge walioyatembelea,”aliongeza Kairuki.

Aliwataka washiriki hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kisekta na kuongeza kuwa, yuko tayari kuwapokea wadau wote kwa ajili ya ushauri na majadiliano lengo likiwa ni kuboresha Sekta ya madini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Stanslaus Nyongo alisema kushiriki kwao katika maonesho hayo ni ishara ya ushirikiano na kuongeza kuwa, maonesho hayo yamekuwa kivutio kikubwa tofauti na maonesho mengine ambayo yamekuwa yakifanyika katika Viwanja hivyo vya Bunge.

Aliwataka washiriki kujipanga kwa maonesho mengine kama hayo na kueleza kuwa, awamu nyingine utawekwa utaratibu wa kumpata mshindi kama mwoneshaji bora wa maonesho hayo.

Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi tarehe 31 Juni, 2018 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, na kufungwa tarehe 1 Juni, 2018 na Waziri wa Madini, Angellah kairuki.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akizungumza jambo wakati akifunga Maonesho ya Madini. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki akitoa Cheti kwa mmoja wa Washiriki wa Maonesho ya Madini. Wanaofuatilia ni kushoto ni Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila na wa Kwanza Kuli ni Mtaalam kutoka Wizara ya Madini, Assah Mwakilembe.

No comments:

Post a Comment