Na Veronica Simba, Dodoma
Wataalam mbalimbali
kutoka sekta ya madini nchini wameshiriki warsha maalum iliyotolewa na wataalamu
kutoka Australia, kwa lengo la kujifunza uzoefu kutoka nchi hiyo ambayo imepiga
hatua kubwa katika sekta husika.
Naibu Waziri wa
Madini Doto Biteko alifungua rasmi warsha hiyo ya siku mbili, Juni 4 jijini
Dodoma na kusema kuwa Tanzania inahitaji kujifunza zaidi kutoka nchi
zilizofanikiwa katika sekta ya madini kama Australia, ili iweze kukuza zaidi
mchango wake katika katika Pato la Taifa.
“Wenzetu Australia,
sekta yao ya madini ina mchango mkubwa sana; zaidi ya asilimia 40 kwenye Pato
lao la Taifa. Kwa hiyo, tunakutana nao kubadilishana uzoefu, ni namna gani wao
wamefanya kuwezesha sekta husika kuchangia kwa kiasi hicho kwenye Pato la
Taifa.”
Aidha, Naibu Waziri
alisema kuwa, suala muhimu ambalo Wizara ya Madini inalisimamia ni kuhusu
usimamizi wa rasilimali za madini.
Biteko alitumia fursa
hiyo kuiomba serikali ya Australia kuangalia uwezekano wa kuendesha warsha
husika kwa wachimbaji wadogo nchini ili wapate maarifa ya namna bora ya
usimamizi wa rasilimali za madini.
Akizungumzia mchango
wa sekta ya madini kwenye uchumi wa viwanda, Biteko alieleza kuwa, rasilimali
za madini ni tegemeo kubwa katika kukuza uchumi huo.
“Ndiyo maana mtaona
kwamba tunayo miradi mikubwa ya makaa ya mawe, ambayo inazalisha nishati ya
umeme utakaotumika kwenye viwanda vyetu. Kwa hiyo lazima tuisimamie vizuri,”
alifafanua.
Aidha, aliongeza
kwamba, Tanzania ina madini mengi ya teknolojia yakiwemo ya Neobium
yanayohitajika sana duniani kwa ajili ya viwanda.
Alitaja madini
mengine muhimu kwa viwanda kuwa ni Graphite pamoja na Marble, ambayo yote
yanapatikana kwa wingi Tanzania.
Kwa upande wake,
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi David Mulabwa, alisema kuwa, warsha hiyo
ni muhimu sana katika kuwaongezea watumishi ujuzi na maarifa kwa ajili ya
kukabiliana na changamoto za kisekta.
“Kuna mambo ya
mazingira, tozo na kodi mbalimbali katika sekta. Kwa hiyo, jinsi watumishi
wanavyokuwa na ujuzi na maarifa, tunaamini watakuwa katika nafasi nzuri ya
kufanya ya kufanya maamuzi ambayo yatasaidia kuhakikisha kwamba rasilimali za
nchi hii zinalinufaisha Taifa ipasavyo.”
Awali, mmoja wa
waratibu wa warsha hiyo, ambaye ni Afisa kutoka Ubalozi wa Australia kutoka
Ofisi ya Nairobi, Deanna Simpson, alieleza kuwa; Serikali ya nchi yake imekuwa
ikitoa warsha za aina hiyo katika nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Kenya,
Madagascar, Ethiopia na Sudan.
Aidha, aliongeza
kuwa, Australia Magharibi ina kampuni zaidi ya 100 zinazoendesha miradi
mbalimbali ya madini zaidi ya 350 katika nchi za Afrika takribani 30 ikiwemo
Tanzania.
Warsha hiyo ya madini
imehitimishwa Juni 5, mwaka huu.
Mtaalamu wa Madini kutoka Australia, Rick Rogerson, akiwasilisha mada katika warsha ya wataalam wa madini nchini (hawapo pichani), iliyofanyika Juni 4 na 5 mwaka huu, jijini Dodoma. |
No comments:
Post a Comment