Veronica Simba na
Samwel Mtuwa, Dodoma
Kamati ya Jamii na
Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la Ghanteng, Afrika Kusini, wametembelea
Wizara ya Madini kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu namna sekta husika
inavyoendeshwa nchini.
Wawakilishi hao wa
wananchi wa Afrika Kusini, walipokelewa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki,
Naibu Mawaziri Doto Biteko na Stanslaus Nyongo pamoja na Katibu Mkuu Prof Simon
Msanjila, jana Juni 19, 2018, Makao Makuu ya Wizara Dodoma.
Akizungumzia nia ya
ujio wao, Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye ndiye pia Mwenyekiti wa Kamati husika,
S. Khanyile alisema kuwa, walipenda kupata uzoefu wa Tanzania katika kusimamia
uchimbaji mdogo wa madini pamoja na mbinu za udhibiti wa uchimbaji haramu wa
madini.
Akiwasilisha Mada kwa
Ujumbe huo kuhusu maeneo husika; Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi David
Mulabwa, alieleza kuwa, katika kusimamia uchimbaji mdogo, Serikali kupitia
Wizara ya Madini inatekeleza mambo kadhaa muhimu ambayo ni pamoja na
kuhakikisha wachimbaji wote wanarasimishwa kwa kupatiwa leseni.
Kamishna Mulabwa
alieleza kuwa, pamoja na kuwarasimisha wachimbaji, Serikali pia inatoa mafunzo
mbalimbali kwao kwa lengo la kuwajengea uelewa, inatenga maeneo ya uchimbaji
kwa ajili yao pamoja na kujenga vituo vya mfano kama vile Mgodi wa Mfano wa
Lwamgasa ambao pia utakuwa na Mtambo wa Uchenjuaji madini.
“Vilevile,
tunasimamia pia suala la makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali stahiki kutoka
kwa sekta hii ya uchimbaji mdogo. Ili suala hili liwe na mafanikio, ni lazima
kuhakikisha wachimbaji wanawezeshwa ipasavyo kupitia mafunzo na mambo
mbalimbali kama nilivyoeleza awali,” alifafanua.
Aidha, aliongeza
kuwa, Serikali imekuwa ikiwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia ruzuku
lakini akabainisha kuwa utaratibu huo umesitishwa kwa muda baada ya kujitokeza
changamoto kadhaa, na utarejeshwa tena baada ya kuaandaa utaratibu mzuri zaidi
na wenye tija katika kuendesha zoezi hilo.
Kuhusu suala la
udhibiti wa uchimbaji haramu wa madini, Mhandisi Mulabwa alieleza kuwa, Tanzania
imeweka mfumo mzuri wa kisheria ambao unamtaka yeyote anayejishughulisha na
uchimbaji madini kuwa na leseni halali.
Alisema kuwa,
Serikali pia imeweka utaratibu wa kusimamia kwa karibu shughuli zote za
uchimbaji ikiwemo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Vilevile, alisema kuwa kuimarisha mawasiliano
kuanzia ngazi ya chini yaani Serikali ya Kijiji, Wilaya na hatimaye Ofisi za
Madini ni muhimu sana katika udhibiti wa uchimbaji haramu.
“Kupitia mawasiliano
hayo tunafanikiwa kupata taarifa zote mara moja na hivyo inatusaidia kuchukua
hatua stahiki na kwa wakati stahiki.”
Kwa upande wake,
Waziri Kairuki aliwashukuru wabunge hao kwa kufanya uamuzi wa kuja kujifunza
Tanzania na kuomba ushirikiano baina yao uendelezwe. Wabunge hao pia
walishukuru kwa ushirikiano waliopata na kusema kuwa wamefurahi kupata uzoefu
wa Tanzania ambao utawasaidia katika uboreshaji wa sekta hiyo nchini kwao.
Waziri wa Madini,
Angellah Kairuki, akifafanua jambo, wakati wa kikao na Wajumbe wa Kamati ya
Jamii na Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la Ghanteng, Afrika Kusini
(hawapo pichani), waliofika Makao Makuu ya Wizara – Dodoma, Juni 19, 2018
kujifunza na kupata uzoefu namna sekta husika inavyoendeshwa nchini.
|
Kutoka Kulia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Jamii na Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la
Ghanteng, Afrika Kusini, S. Khanyile, Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko,
wakifurahia jambo, wakati Kamati hiyo ilipotembelea Makao Makuu ya Wizara –
Dodoma, Juni 19, 2018 kujifunza na kupata uzoefu namna sekta husika
inavyoendeshwa nchini.
|
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Profesa Simon Msanjila (kulia) na Makatibu wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini, wakifuatilia Mada zilizokuwa zikiwasilishwa na
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi David Mulabwa (hayupo pichani), wakati
Wajumbe wa Kamati ya Jamii na Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la Ghanteng,
Afrika Kusini, walipofika Makao Makuu ya Wizara – Dodoma, Juni 19, 2018
kujifunza na kupata uzoefu namna sekta husika inavyoendeshwa nchini.
|
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki (mwenye nguo ya kitenge), Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus
Nyongo (kushoto kwa Waziri) na Doto Biteko (kulia kwa Waziri), wakibadilishana
mawazo na Wajumbe wa Kamati ya Jamii na Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la
Ghanteng, Afrika Kusini, waliofika Makao Makuu ya Wizara – Dodoma, Juni 19,
2018 kujifunza na kupata uzoefu namna sekta husika inavyoendeshwa nchini.
|
No comments:
Post a Comment