Na Mwandishi wetu, Dodoma
Ziara ya Kamati ya
Jamii na Masuala ya Usalama ya Bunge la Jimbo la Ghanteng, Afrika Kusini, ambao
wapo nchini kujifunza na kupata uzoefu namna Tanzania inavyoendesha sekta ya
madini, imeendelea kwa wabunge hao kuwatembelea wachimbaji wadogo wa dhahabu
waliopo eneo la Nori, wilayani Bahi.
Wakiongozwa na Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Wabunge hao walifanya ziara hiyo Juni 20, 2018,
ambapo walipata fursa ya kujionea shughuli za uchimbaji wa dhahabu unaofanywa
na wachimbaji wadogo katika eneo hilo na kuzungumza nao kuhusu uzoefu wao
katika kazi husika.
Akizungumza kwa niaba
ya wenzake, Kiongozi wa Ujumbe huo, S. Khanyile alikiri kuwa, ziara husika
imewawezesha kujifunza mambo mengi na kwamba watatumia uzoefu walioupata
kuboresha na kuimarisha zaidi sekta ya madini nchini kwao.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri Nyongo aliwahakikishia Wabunge hao kuwa Tanzania itaendeleza
ushirikiano kati yake na nchi ya Afrika Kusini, hususan katika sekta ya madini.
Alisema, ushirikiano
wa nchi hizo mbili katika sekta ya madini, utasaidia kuimarisha na kuboresha
zaidi sekta husika na hivyo kuziwezesha kuwa za mfano katika uchangiaji wa Pato
la Taifa na kuimarisha uchumi wa nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Juni 19, mwaka huu,
Wabunge hao walifika Makao Makuu ya Wizara ya Madini jijini Dodoma, ambapo
walipokelewa na Waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki. Katika siku hiyo ya
kwanza ya ziara yao, walipata fursa ya kujifunza kuhusu sekta husika kupitia
uwasilishwaji wa Mada mbalimbali uliofanywa na Kamishna wa Madini, Mhandisi
David Mulabwa.
Pichani ni matukio
mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment