Na
Samwel Mtuwa, Dodoma
Katibu Mtendaji wa
Tume ya Madini Prof. Shukran Manya leo tarehe 28 Juni, 2018, amepokea ripoti ya
Ukaguzi Maalum wa Migodi ya Madini ya Vito na Madini ya Kinywe (Graphite)
kutoka kwa Mwenyekiti wa Timu ya Ukaguzi Profesa Justinian Ikingura.
Ripoti hiyo imetokana
na Tume Maalum ya Wataalam Sita iliyoundwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini
Prof. Manya tarehe 17 Juni, 2018 ikilenga kufanya ukaguzi maalum katika maeneo
ya uchimbaji wa madini ya Vito na Kinywe katika wilaya ya Ulanga Mkoani
Morogoro.
Aidha, ukaguzi huo
ulilenga kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko aliyoyatoa
hivi karibuni wakati wa ziara yake mkoani Morogoro.
Katika ziara ya Naibu
Waziri Biteko mkoani humo, alipokea malalamiko kutoka kwa wachimbaji wadogo wa
madini ya vito ambao ni wanakijiji wa kijiji cha Epanko kilichopo katika eneo
la mradi wa madini hayo.
Aidha, kufuatia malalamiko hayo Naibu Waziri
aliahidi kuunda timu ya watalaam wa madini itakayofanya kazi ya ukaguzi maalum
kwa lengo la kutathmin uendeshwaji wa migodi ya madini ya vito na kinywe pamoja
na biashara ya madini kulingana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 pamoja na
marekebisho yake.
Katika ripoti hiyo, timu
ya wataalam wa madini imetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo Serikali kupitia
Wizara ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)
kuweka mkakati wa kufanya Utafiti na tathmin ya madini adimu ya vito katika
eneo la Mahenge na maeneo mengine nchini ili kuwepo na takwimu sahihi za
kuvutia wawekezaji katika uchimbaji wa madini hayo.
Pendekezo jingine ni
Mamlaka husika kuweka mpango wa kutoa huduma ya uthaminishaji wa madini ya vito
katika maeneo ya wachimbaji wadogo ili kuwezesha wachimbaji hao kupata bei
stahiki ya madini wanayozalisha na hivyo kuongeza kipato chao na kulipa tozo
stahiki kwa Serikali.
Wajumbe wa timu hiyo
walitoka katika Taasisi ya Jiolojia ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Chuo
cha Madini Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Ukaguzi wa
Migodi na Afisa Madini Mkazi wa Dodoma.
Mwenyekiti
wa Timu Maalumu ya Ukaguzi wa Migodi ya Vito na Madini ya Kinywe (Graphite)
Profesa Justinian Ikingura akikabidhi Ripoti ya Ukaguzi huo kwa Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini Profesa Shukrani Manya, makabidhiano haya
yamefanyika tarehe 28/6/2018 katika ukumbi wa mikutano wa GST. Wengine
wanaoshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula
na Profesa Abdukarim Mruma pamoja na watalam wa timu hiyo.
Mwenyekiti
wa Timu ya Ukaguzi wa Migodi ya madini ya Vito na Kinywe Profesa Justinian
Ikingura aliyekaa (katikati) akimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa
Idris Kikula mara baada ya kumaliza uwasilishaji wa mada nzima ya Ripoti ya
Ukaguzi kwa Tume ya Madini.
|
No comments:
Post a Comment