Na Veronica Simba, Dodoma
Balozi wa Australia
nchini Tanzania, Alison Chartres, amemtembelea Waziri wa Madini Angellah
Kairuki na kuzungumzia ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya madini.
Akiongoza Ujumbe wa
Umoja wa Kampuni za Madini na Nishati za Australia, Juni 13, 2018 Makao Makuu
ya Wizara Dodoma; Balozi Chartres alimweleza Waziri Kairuki kuwa nchi yake
inapenda kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo
sekta ya madini.
Kwa upande wake,
Waziri Kairuki; pamoja na kumhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea
kutoa ushirikiano kadri inavyotakiwa kwa Australia, lakini pia alitumia fursa
hiyo kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa nchi hiyo, waendelee kuja kuwekeza
katika sekta ya madini nchini na katika sekta nyingine pia.
“Ni matumaini yetu
kuwa, nchi zetu zitaendeleza ushirikiano katika sekta ya madini na sekta
nyingine mbalimbali kama ambavyo tumekuwa tukifanya,” alisisitiza Waziri.
Aidha, Waziri Kairuki
aliuelekeza Ujumbe huo kutoka Australia, kuwasilisha mapendekezo rasmi kwa
Serikali ikiwa kuna eneo lolote katika sekta ya madini, wanalodhani linahitaji
kufanyiwa marekebisho ili wataalam wayapitie na kuona endapo yana tija kwa
pande zote mbili, na kisha kufikia maamuzi.
“Niweke wazi kuwa,
Serikali ya Tanzania imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya madini inawanufaisha
wananchi wake ipasavyo. Kwa hiyo, kila tutakapobaini kuwa liko eneo ambalo
halituridhishi, hatutasita kufanya marekebisho kwa manufaa ya Watanzania wote.”
Kikao hicho pia
kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Kamishna wa Madini
Tanzania Mhandisi David Mulabwa pamoja na maafisa mbalimbali waandamizi kutoka
Wizara ya Madini na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment