Na
Fredy Mgunda, Morogoro
Naibu Waziri wa Madini
Mhe Doto Mashaka Biteko amesema kuwa ataunda tume maalumu kwa
ajili ya kuchunguza migodi yote nchini ikiwa ni pamoja na utambuzi wa aina ya
madini yanayopatika katika migodi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya
Ulanga Mkoani Morogoro kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania haiendelei kuibiwa
na wawekezaji katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa ziara
ya siku mbili Mkoani Morogoro Mh Biteko alisema kuwa madini yote yaliyopo
katika ardhi ya Tanzania ni mali ya watanzania hivyo yanapaswa kuwanufaisha
watanzania kwanza ndipo watu wengine wafuate.
“Naombeni watanzania wote
mjue kuwa madini haya ni mali ya watanzania wote hivyo tunapaswa kuyalinda na
kutoa taarifa sahihi kwa serikali kama kuna mtu anaiibia serikali kwa namna
moja au nyingine ili serikali iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi yake, Na
mimi nawaambieni watanzania tuache uoga tuseme ukweli kama Rais wetu Mhe Dkt
John Pombe Magufuli anavyosisitiza utendaji wa uwazi na uwajibikaji katika
serikali” Alikaririwa Mhe Biteko
Biteko amepiga marufuku
wawekezaji kutumia fedha zao kuwanyanyasa wananchi waliopo kwenye maeneo ambayo
kuna migodi kwa ajili ya kuwaibia watanzania ambao bado wana kipato cha chini
katika maeneo yanapopatikana madini.
“Najua hawa wawekezaji
wanapesa nyingi sana hivyo isiwe sababu ya kuwarubuni baadhi ya wananchi na
kuwatesa wananchi wengi hususani waliopo kwenye maeneo ya madini na leo nataka
niwaambie ukweli wawekezaji wote nchini najua ambavyo mnatumia pesa zenu
kuwanyanyasa wananchi, sasa ndio mwisho wenu maana serikali ya awamu ya tano
inataka haki kwa kila mwananchi” Alisisitiza Biteko
Naibu Waziri wa Madini Mhe
Doto Mashaka Bitoke alifanya ziara ya kikazi katika kijiji cha Ipanko kilichopo
katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kugundua kuwa kuna wawekezaji
wanaidanganya serikali na wananchi kwa kutoweka wazi kiasi gani ambacho
wanakipata kwenye migodi iliyopo katika kijiji hicho.
“Jamani wana Ipanko nchi
hii tumeibiwa sana sasa ifike mwisho tusema hapana haiwezekani tena kwenye
serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli tuendelee
kuibiwa madini yetu na kuwanufaisha watanzania ambao wapo nje ya nchi yetu,
Rais kashasema na sisi wasaidizi wake tunaungana naye kwamba iwe mwisho
kuchezewa kwa rasilimali zetu”
“Chonde chonde nyie
viongozi wetu wa ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa tunaomba
msituangushe kwa kupokea rushwa kutoka kwa wawekezaji na kuisaliti nchi yako
kuendelea kuibia kirahisi namna hii” alisema Biteko
Biteko alieleza kuwa
serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inawapenda sana
kuwa na wawekezaji wengi wenye tija ambao sio wababaisha na ambao wamekuja nchi
kuiba rasilimali za watanzania.
Aidha, Biteko alisema kuwa
haiwekani muwekezaji akawekeza Bilioni 42 halafu akachangia madawati na mifuko
ya saruji katika jamii kama ndio mchango wake, haiwezekani wanapaswa kuchangia
kulingana na kiasi ambacho wamewekaza kwa faida na manufaa ya wananchi.
“Mimi binafsi hainiingi
akilini kuona muwekezaji amewekeza pesa nyingi kama hizo halafu kwenye shughuli
za kimendeleo amechangia kiasi kidogo namna hiyo kwangu nasema haiwezekani na
nchi hii kwa sasa sio yakuchezewa tena” alisema Biteko
Lakini pia Naibu waziri
huyo alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe Goodluck Mlinga kwa
kuwapigania wananchi wake kwa kuzifikisha kero mahali husika na kutafutiwa
ufumbuzi.
Nao baadhi ya wananchi
akiwemo Pangarasi Kanyali, Cyprian Kanyali, Micky Sengo, Doedatus Moholeli,
Hilda Linoma na Fredrick Kazimoto walimpongeza Naibu Waziri wa
Madini Mhe Biteko kwa kufika kijiji hapo na kusiliza kero zao kwani wana amini
zitatafutiwa ufumbuzi kwa kufuata sheria na katiba ya nchi.
“Toka sisi tuzaliwe
hatujawahi kutembelewa na waziri na kusikiliza kero zetu kama ambavyo wewe
umefika kijijini kwetu leo hii tunajisikia wenye amani na furaha kwa kuwa
tunajua kero zetu tunazifikisha moja kwa moja kwa kwa Rais wetu kupitia wewe
waziri” Walisema wananchi hao
Awali Mbunge wa Jimbo
la Ulanga Goodluck Mlinga alisema kuwa lengo la waziri kufika katika
kijiji hapo ni kujionea kero wanazokumbana nazo wananchi kupitia wawekezaji wa
sekta ya madini na kuzitafutia ufumbuzi.
“Huku ni mbali sana Mheshimiwa
Naibu Waziri lakini kuna madini mengi ambayo ndio utajiri wa nchi hii hivyo
tunapaswa kuwa makini na hawa wawekezaji maana wamekuwa wakiibia sana serikali
yetu” Alisema Mlinga.
Baadhi ya wananchi
kijijini Ipanko wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto
Mashaka Biteko alipokuwa katika ziara ya kikazi katika Wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro kukagua shughuli za utendaji wa wawekezaji wa migodi .
|
Naibu Waziri wa
Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi kijijini Ipanko Wilaya
ya Ulanga wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro ya kukagua
shughuli za uwekezaji wa migodi.
|
No comments:
Post a Comment