Friday, June 8, 2018

Kampuni ya Auxin ya China yaonesha nia kuwekeza kwenye kiwanda cha Baruti


Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amekutana na Wawakilishi wa Kampuni ya Auxin ya China ambao wameonesha nia ya Kujenga Kiwanda cha Baruti nchini.

Ujumbe wa kampuni hiyo umemweleza Waziri Kairuki lengo la kukutana naye kuwa ni kutaka kujua taratibu mbalimbali ikiwemo za Kisheria ili kujua namna ambavyo kinaweza kujenga kiwanda hicho nchini.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Kairuki amewaeleza wawakilishi hao kuwa, endapo kampuni husika itapata fursa ya kuwekeza nchini suala la ajira kwa watanzania linatakiwa kuchukuliwa kwa umuhimu wake ili kuhakikisha kwamba watanzania wanapata ajira.

Pia, amewataka watendaji hao kusoma na kuelewa kipengele cha uwezeshaji wazawa na maeneo ambayo shughuli zao zitafanyika ili kuelewa namna ambavyo watahakikisha watanzania wananufaika na uwekezaji wao katika maeneo ambayo shughuli zao zitafanyika.

kikao hicho kimehudhuriwa  pia na  Kaimu  Kamishna  Msaidizi wa  Madini anayeshughulikia masuala ya Baruti, Chiku  Juma, Wataalam wa Wizara ya Madini na  Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kampuni hiyo inafanya shughuli kama hizo katika nchi za Congo DRC, Uganda, Namibia na Guinea.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisisitiza jambo wakati wa kikao na Kampuni ya Auxin ya China ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa Kiwanda cha Baruti nchini.


Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia masuala ya Baruti, Chiku Juma akiongea jambo katika kikao hicho. Wengine wanaofuatilia ni Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki (katikati) katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Kampuni ya Auxin ya nchini China.  Wa pili kulia ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia masuala ya Baruti, Chiku Juma. Wa pili kulia ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia mfano wa vifaa vinavyotengenezwa na kampuni Kampuni ya Auxin ya nchini China.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiongoza kikao kati ya Wizara ya Madini na Wawakilishi wa Kampuni ya Auxin ya nchini China.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia mfano wa vifaa vinavyotengenezwa na kampuni Kampuni ya Auxin ya nchini China.

No comments:

Post a Comment